Hata hivyo niseme
kwamba, moja ya kasoro (weakness) ambazo zaweza kujitokeza kwa wazi kwa mtu wa
aina ya HP, ni pale ambapo kipaji kilekile chenye manufaa makubwa kinapoweza
kutumika kuinyume na hivyo kuweza kupotosha pia badala ya kujenga.
Hii yaweza
kutokea ama kwa makusudi au kwa kutokukusudia kwa vile pamoja na vipaji vyake
bado yeye ni mwanadamu na hana ukamilifu katika mambo mengi hata katika yale
anayoyasimamia. Hiki ndicho nilichokiona kwenye mijadala ya Ndugu HP katika
vipindi hivi vya Mada Moto.
Sina hakika kama nilichokiona kimetokana na
umakusudi au ubahati mbaya, lakini kuna namna ambavyo HP katumia nafasi yake
isivyo na hivyo kuharibu dhana nzima ya hoja zake na mimi kama Mtanzania
mzalendo kama yeye ninashawishika kutoa maoni angu juu ya maoni na mtazamo
wake.
Nitatoa maoni au mtazamo
(reflection) wangu kuhusu maeneo matatu niliyoyaona yanahitaji ama mjadala au
ufafanuzi mbadala wa ule uliotolewa na Bwana HP. Maeneo hayo ni Maadili;
Ukweli na Haki; pamoja na dhana ya Mabadiliko na Mageuzi (change
and transformation). Leo nitaanza na Maadili.
Katika uwasilishaji wake
HP amejitambulisha kama mzalendo, mtetea haki za wanyonge, mkweli,
muungwana na mchukia maovu ya aina zote. Hizi ni tunu na sifa
njema kwa raia yeyote anayeitakia nchi yake mema. Hata hivyo kujitambulisha kwa
sifa hizi na kuziishi kwa vitendo ni mambo mawili tofauti.
Katika kumsikiliza
na kuchanganua kauli za HP, nimeona kuna utata juu ya kile anachojitambulisha
nacho na kile anachokisimamia kupitia kauli na hisia zake. Kwa nini nimesema
haya?
1.
HP anatumia vibaya
kukubalika kwake mbele ya hadhira ya watanzania kupitia ushiriki wake katika
mchakato wa mapendekezo ya katiba. Kwa kuwa kajitambulisha katika misingi ya
maadili, kwa maadili hayohayo, sidhani kama ni sahihi kwake kwenda kwenye
runinga na kuanza kuchambua uovu wa mtu mwingine kwa nguvu kubwa ya ushawishi
wake.
Nadhani tafsiri halisi ya maadili, aliyonayo inamlazimisha kutomuhukumu
mtu mwingine (raia wa Tanzania) bila vielelezo na kwa habari za kusikia,
kuambiwa, na shutuma za kisiasa. Maadili anayoyasimamia, yanamlazimisha
kuheshimu na kustahi watu wengine huku akitambua wana haki, uhuru na wanalindwa
na sheria kama ilivyo kwake.
Kwa kwenda kutangazia dunia ubaya/uovu wa mtu
mwingine kwa kigezo cha uzalendo, kupenda maadili, na uanaharakati wake ni
kinyume na misingi ya sheria na kimaadili anayoisimamia yeye mweyewe.
Nina
hakika kabisa kwa uelewa wake HP anajua misingi ya "natural justice"
na imani ya dini yake haimpi kibali cha kukalia "kiti cha enzi cha
hukumu" kuwahukumu watenda dhambi kwa majina yao.
Kama jamii itaanza
kuruhusu mambo ya mambo kama haya basi nchi haitakalika maana kwa namna moja au
nyingine kila mmoja anajua uovu/ubaya/mapungufu ya wengine. Kama maadili
anayosimamia HP ndio haya, basi tutegemee kesho ataibuka na kuanza kumchambua
mwingine na mwingine.
HP anajua hii ilivyo mbana na inavyoweka kumuumiza
mwingine kwani pale Mch Msigwa alipoamua kumtajia shutuma zake, alikua mkali na
kutaka kujibu hapohapo kila kitu ingawa haikua sehemu ya mada. HP anafikiri ni
watu wangapi watapata nafasi kama yake kwamba wanapohutumiwa ovyo kwenye
runinga nao watapata "airtime" kama yake ya kwenda kujibu?
2.
HP angetusaidia
watanzania wengi kama mimi ambao kwa miaka mingi tunasumbuliwa na utata wa
Edward Lowasa (the question of Edward Lowasa...aka EL).
Kwa miaka mingi tumekua
tukisikia habari za Mzee Lowasa kwamba ni mtu mchafu, tajiri mwenye pesa nyingi
za kununua watu na mengine mengi. Jambo hili limeongolewa kiasi kwamba
limeingia ndani mwa masikio ya wengi kiasi kwamba kuna watoto wamezaliwa na leo
wana miaka 8 ukiwauliza tafisiri ya neno Fisadi wanasema ni Lowasa.
Mimi
kama mtu ninayependa kujiaminisha vitu kwa vielelezo (hata kama sio kwa 100%)
nimekua nikitamani sana kukubaliana na shutuma na dhana hii dhidi ya mtazania
huyu mwenyeji wa Monduli lakini kwa ushahidi/vielelezo.
HP angetusaidia
na kututendea haki watu kama mimi kama angekuja na ushahidi unaonesha mambo
yafuatayo:-
a.
Atutajie sheria ambazo
EL amevunja na kumfanya kuwa mtu asiyekubalika kwenye jamii
b.
Maadili ya uongozi
aliyokiuka katika nafasi alizopewa
c.
Wizi wa mali ya umma na
za wengine alizohusika
d.
Ufisadi alioshiriki na
yanayofanana na jinsi alivyoshiriki
e.
Atuambie EL ana mali
zisizokua na maelezo (labda mwizi, halipi kodi, kapora mahali, nk)
f.
Atuambie hizo mali ni
zipi, ni kiasi gani na ziko wapi
g.
Kisha atuambie hizo njia
ovu ambayo Mzee huyo kazitumia
3.
HP kuja tu na shutuma za
jumla huku akitumia kipaji na uwezo mkubwa wa kuongea na kushawishi kumpaka
raia mwingine matope usoni na kumvua nguo mbele ya familia yake, ndugu zake na watanzania
kwa ujumla, ni kinyume kabisa na misingi ya kisheria, haki na kimaadili
anayoisimamia HP
4.
Pamoja na namba 2 na 3,
HP angetutendea haki sisi wenye udadisi wa kutaka kuujua "ukweli
wote" kwa kuziweka shutuma za Mzee EL katika muktadha wa kitaasisi na
kisheria (justifications of the stated accusations in the context of
intuitional and legal perspective). Mzee EL ni raia wa nchi hii na yuko
chini ya mifumo ya kisheria na kiutawala inayongoza nchi yetu. Nilitegemea
Ndugu HP:-
a.
Atuambie ni kwa nini
huyu mtu anayemwelezea kama mchafu na gwiji ya ufisadi hajawahi chukuliwa hatua
za kisheria
b.
Atuambie ni kwa nini
serikali na vyombo vyake vimeamua kumfumbia macho mtu mmoja aishi kama vile
yuko kisiwani ndani ya taifa linaloongozwa na serikali inayojinasifu kwa
utendaji wake na misingi ya sheria
c.
Atuambie ni kwa nini
serikali ambayo kiaina inaonekana anaitetea, imehifadhi tu kumbukumbu za uovu
wa Mzee EL lakini haimchukulii hatua stahiki ili kuleta usawa na haki mbele ya
sheria
d.
Atuambia ni adhabu gani
anaipa serikali ambayo inaficha waovu na nani anatakiwa kuwajibisha kwa uovu
huu mkubwa wa kuhifadhi waovu
e.
HP haoni kwamba wa
kuhojiwa zaidi kuhusu anachokiita uovu na ufisadi wa Mzee EL ni serikali na
vyombo vyake ambavyo tumevipa mamlaka ya kisheria kutulidha dhidi ya maovu na
waovu?
5.
HP anatumia vibaya
nafasi aliyopewa na Rais kwa niaba ya watanzania kuchafua majina ya wengine
kwenye jamii. Nadhani nafasi yake kama mjumbe na kamishna wa tume ilikua chini
ya kiapo ambapo pamoja na mambo mengine ni kutunza siri na mambo binafsi.
Sidhani kama ni sahihi kwake kuja leo na kusema Mwalimu MM alipokuja kwenye
mazungumzo ya faragha na tume kwa nafasi yake kama kiongozi alisema muungano
uvunjwe au tuhamishie visiwa vya Zanzibar kwenda ziwa Victoria au tupeleke
Kisiwa cha Ukerewe karibu na Pemba ili kuimarisha muungano.
Kutumia
nafasi yake ya ujumbe wa tume kumsulubisha raia waliyempa nafasi kama kiongozi
mstaafu kutoa maoni yake, ni ukiukwaji wa maadili kwa nafasi aliyopewa.
Kwa
hili namfananisha HP na kasisi anayeletewa kesi za ndoa na mambo mengine
binafsi na kisha kwenda kuyatumia baadaye kunapokua na sababu ya kutofautiana
na hao aliowasaidia kama mshauri wao.
HP amekwenda mbali kudai kwamba sio tu
alipata huo muda wa kuongea na EL na kuijua dhamira yake mbaya, bali kwa kuwa
alikua serikalini aliona mengi yanayomuhusu EL.
Sidhani kama hii ndio misingi
ya maadili anayoisimamia na kama ni hivyo kwa nini asiwaulize huko serikali
sababu inayowafanya watunze maovu ya EL badala ya kumwajibisha? Je HP kaona
maovu ya watanzania wangapi "huko serikalini" alikokua na
kapanga kwenda kuyatumia wapi na wakati gani? Haya ni maadili gani?
6.
HP angetutendea mema
kama angetumia uzito wa maneno yaleyale aliyoyatumia kwa Mzee EL kuwasema wote
waliopinga matakwa ya katiba ya wananchi.
Kule bunge la katiba walikuwepo
wajumbe zaidi ya mia nne nadhani ambao kwa mshikamano wao sio tu walipinga
aliyoiita "katiba ya wananchi" bali wako waliosindikiza misimamo yao
na kaauli za kutisha kidola, matusi na kejeli nyingi dhidi ya walioiunga mkono.
HP kapanga na hawa kuja kwenye runinga na kuwachambua uovu wao lini ikiwa ni
pamoja na ule aliouona "kule serikalini"? Najiuliza tu kwamba
kwani kazi ya tume ya Jaji Warioba ilikua ni nini? Ilikua ni kukusanya maoni
yanayofanana kwa watanzania wote?
Na kama ilikua ni hivyo wangeyajuaje na kwa
nini walipoteza muda kuwasikiliza ambao walikua na mawazo ya tofauti? Kwani
ilikua ni masharti ya Tume kwamba kila anayekwenda akaongee yale yalikubalika
na wengi?
Mbona Mh Rais wetu alipinga mambo kadhaa kwenye katiba ile hadharani
na sijamuona HP akimchambua kwa ubaya na uovu wake kwa kupinga kauli za
wananchi? Haya ndio maadili ya Ndugu HP?
7.
HP kajitangaza kama
mfalme aliyejitawaza mwenyewe miongoni mwa watanzania (He has declared himself
as a self-appointed king).
Amejipa uhalali na mamlaka kwamba yeye anaweza
kuwaambia/kuwashawishi kitu watanzania na wakamsikiliza. Kwamba watu wengine
wafanye maamuzi kwa kuogopa kukosa "support" yake au
"kulizwa" na maamuzi yake iwapo hamutamtii.
Nani kamwambia kwamba
yeye akiikubali CCM au UKAWA au wagombea wao basi watanzania watamsikiliza na
kumtii?
Yeye ni nani kuiambia timu yenye mapenzi makubwa na panga la
"kukata" iliyokua imeketi Dodoma kwamba wafanye maamuzi katika uteuzi
wa wagombea ubunge kwa kufuata matakwa yake?
Pamoja na uwezo wake na mchango
wake mzuri kwenye jamii, nadhani huu ni mtazamo usiyo sahihi kwa kujipa mamlaka
na utisho wa kuwapa wengine masharti.
Nadhani angetoa mchango mkubwa na wenye
heshima zaidi kama mawazo yake yangejengwa kwa hoja na kutuaminisha juu ya yale
anayoyasimamia bila vitisho iwapo watu hawatatii mtizamo wake. Kwa lugha ya
kawaida mtu atajiuliza HP ni nani hata awe na sauti ya aina hii?
8.
HP kaonesha kwamba hana
misingi na hana maadili katika ukamili anayotuaminisha kua nao. Katika tungo
yake ya mwisho ya kumalizia kipindi siku alipokua na Mch Msigwa, anasema iwapo
CCM watafanya yale aliyoyatamka yuko tayari kumuunga mkono mgombea wao na itakua
kinyume chake wasipofanya hivyo.
Hii inaonesha kuna shida katika misingi yake.
Kwamba mgombea wa chama chetu kikuu anaweza kuwa msafi au mchafu mbele zake
kutegemeana tu na iwapo "mamlaka yake ya kifalme aliyojipa"
yatasikilizwa na kutekelezwa.
Kwenye moja ya makala zake alizoandika kwenye
blog yake mara baada ya uteuzi wa Dodoma, ameonesha kabisa kwamba anakubaliana
na na uteuzi wa Dr. Magufuli na anamuunga mkono ikimanisha hatambui iwapo ana
uchafu kama ambavyo amekua akichambua uchafu wa EL.
Siku EL apohamia
CDM," Profesa wa Elimu aliyebobea na kujulikana na watanzania katika
maswala ya kisiasa kuliko ya taaluma yake", yaani Prof. Kitila Mkumbo,
alihojiwa na kituo cha BBC na alitakiwa kutoa uchambuzi wake wa tukio lile.
Pamoja na mambo mengine, Profesa huyo alisema kitendo cha Chadema kumpokea na
kumpa nafasi ya kuwa mgombea mtu ambaye waliwekeza kumchafua wao wenyewe kwa
muda mrefu ina tafsi kuu mbili. Moja ni ushindi kwa EL kwamba
walimchafua sasa wanamsafisha, na pili ni fundisho kwa Chadema na
mwenendo mzima ya siasa za Tanzania zilizojikita katika shutuma za kuokota
barabarani.
Kwamba watu waache siasa za kuchafuana na kushutumiana ovyo kwa
mambo yasiyo na ushahidi na wasiyo na uwezo wa kuyathibitisha pasipo shaka.
Nasikitika kwamba tatizo hilo limemvaa HP. Ninaamini HP angeweza kuongelea
dhana ya maadili katika uongozi na nafasi yake katika uchaguzi unaofuata bila
kumdhalilisha EL au raia mwingine yeyote yule na ingekua na tija zaidi kuliko
alivyofanya.
Bila kutazama kauli za
kisiasa na mchakato wa uchaguzi ambao hamunyang'anyi mtu haki yake ya kikatiba,
ninamtazama Mzee EL kama mtanzania mwingine yeyote yule mwenye haki ya
kuheshimiwa, kuthaminiwa na kuhukumiwa anapofanya makosa kwa misingi ya
kitaasisi na kisheria tuliyojiwekea kama taifa.
Tunapofurahi leo anachokifanya
ndugu HP dhidi ya EL, kesho itakua ni kwa mwingine na mwingine na tunaelewa
vema mambo kama haya yatatufikisha wapi. Kuna njia za kuonyesha machungu,
mapenzi, na hofu zetu dhidi ya watu lakini nasita kama hii ya HP ni mojawapo
tunayoweza kuikumbatia
Nitaendelea na sehemu ya
pili.
Rejea:
a.
Siku
ya 2 ya Mjadala wa HP na Mch Msigwa: sehemu ya kwanza: https://www.youtube.com/watch?v=-KvqAyxnWkU
na sehemu ya pili: https://www.youtube.com/watch?v=fteTqyCOcrI
b.
Siku
ya 3 ya mjadala wa HP na ndugu Mtatiro: sehemu ya kwanza: https://www.youtube.com/watch?v=GBhYacfvGuc na
sehemu ya pili: https://www.youtube.com/watch?v=8E-5WxBxzfQ
Mwalimu MM ni mhadhiri Katika kitengo cha Sayansi ya ya Kompyuta
ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mtafiti wa mifumo ya TEHAMA (ICT) katika
Huduma za Afya (Health Informatics). Unaweza kuwasiliana naye kupitia mmmwalimu@gmail.com Blog: http://mwalimumm.blogspot.com
PAPO KWA PAPO Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo
na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia
tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment