MAGAZETINI JULAI 06,2015:-Mume kumnyonga mjamzito, wiki ngumu CCM na Mwenyekiti wa Kijiji (CHADEMA) ahukumiwa kifungo cha miaka miwili jela - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, July 06, 2015

MAGAZETINI JULAI 06,2015:-Mume kumnyonga mjamzito, wiki ngumu CCM na Mwenyekiti wa Kijiji (CHADEMA) ahukumiwa kifungo cha miaka miwili jela

NIPASHE

Zikiwa zimebakia siku sita kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, kura ya maoni iliyoendeshwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inamweka kileleni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa changuo la kwanza la wengi kwa kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho.

Wakati Lowassa akiwafunika watia nia wenzake ndani ya CCM, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, anawafunika wenzake kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akiwa changuo la wengi kwa asilimia 23.1.

REDET wamesema kuwa matokeo ya utafiti huo yanaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti.

“Sampuli iliyotumika katika utafiti huu kwa kiwango cha kutosha ni wakilishi na ina akisi hali halisi ya Watanzania,”  imesisitiza ripoti hiyo iliyojatwa kuwa ni maoni ya wananchi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2015, mwaka huu.

Katika utitiri wa watia nia ndani ya CCM, kati ya wahojiwa 1,250 waliohojiwa, Lowassa alipigiwa kura na watu 338, wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akipata asilimia 8.2 akichaguliwa na watu 103.

Utafiti wa REDET ulifanyika katika wilaya moja moja kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara baada ya wahojaji kukataliwa ruhusa ya kufanya utafiti wao katika mikoa mitano ya Zanzibar.

Utafiti huo uliokuwa umedhaminiwa na kampuni ya Business Times Limited, ulifanyika kati ya Juni 23-26, mwaka huu na kila wilaya ilikuwa na wahojiwa 50.

Kwa upande wa CCM watia nia wengine ni Mizengo Pinda nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; John Magufuli nafasi ya nne akipata asilimia 6.6 akipigiwa kura na watu 83 na Charles Makongoro Nyerere nafasi ya tano akipigiwa kura na watu 54.

Wengine ni Mark Mwandosya nafasi ya sita akipata asilimia 3.1 akichaguliwa na watu 39; Dk. Harrison Mwakyembe nafasi ya saba akiwa na asilimia 1.4 akichanguliwa na watu 18; Frederick Sumaye nafasi ya nane akipata asilimia 1.4 akichaguliwa na watu 17; nafasi ya tisa imekamatwa na Jaji Augustino Ramadhani akiwa na asilimia 1.2 akichaguliwa na watu 15 na nafasi ya 10 amekamata Mwigulu Nchemba akiwa na asilimia 1.0 akichaguliwa na watu 13.

Wengine na idadi ya waliowachagua na asilimia zao kwenye mabano ni January Makamba nafasi ya 11 (asilimia 0.8, watu 10); Dk. Asha-Rose Migiro nafasi ya 12 (asilimia 0.7, watu tisa); Samuel Sitta nafasi 13 (asilimia 0.6. watu wanane); Lazaro Nyalandu nafasi ya 14 (asilimia 0.4, watu watano).

Pia wamo Prof. Sospeter Muhongo nafasi ya 15 (asilimia 0.4, watu watano); Balozi Amina Salum Ali nafasi ya 16 (asilimia 0.2, watu wawili); Dk. Mohammed Gharib Bilal nafasi ya 17 (asilimia 0.2, watu watatu); Stephen Wasira nafasi ya 18 (asilimia 0.2, watu 3) na William Ngeleja nafasi ya 19 (asilimia 0.2, watu wawili).

Wengine ni Balozi Ally Karume nafasi ya 20 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Amos Siyantemi nafasi ya 21 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Joseph Chagama nafasi ya 22 (asilimia 0.1, mtu mmoja); na Mwele Malecela nafasi ya 23 (asilimia 0.1, mtu mmoja).

Katika kura hiyo, watia nia 14 ambao wamejitosa kwenye urais kupitia CCM hawakutajwa kabisa na watoa maoni ambao ni Balozi Augustine Mahiga; Boniphace Ndengo; Eldophonce Bihelo; Godwin Mwaipopo; Dk. Hamis Kigwangalla; Dk. Hans Kitine; Joseph Chagana; Leons Mulenda; Luaga Mpina; Maliki Marupu; Mathias Chikawe; Monica Mbega; Titus Kamani na Balozi Patrick Chokala.

Kwenye kundi la Ukawa, namba mbili amechukua Prof. Ibrahim Lipumba akiwa na asilimia 13.6 akichaguliwa na watu 170; Freeman Mbowe ameshika nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; James Mbatia amekamata nafasi ya nne akiwa na asilimia 3.2 akichaguliwa na watu 40; Emmanuel Makaidi akishikilia nafasi ya tano kwa asilimia 0.6 akichaguliwa na watu 8, huku George Kahangwa akishika nafasi ya sita kwa asilimia 0.2 akichaguliwa na watu wawili.

Swali la msingi lililokuwa linaulizwa lilisema: “Kama wewe leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, kati ya wanachama wake 37 waliokwishajitokeza, ungemchagua nani apeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 2015?”

Pia swali kwa Ukawa lilikuwa: “Kama wewe leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kati ya wanachama wake waliokwishakutangaza nia na wanaotarajia kutangaza nia ungemchagua nani apeperushe bendera ya Ukawa katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 2015?”

Ripoti ya REDET imesema kuwa kwa maswali yote, mhoji alitakiwa kutomtajia majina mhojiwa, bali mhojiwa aliombwa ataje jina alilonalo kichwani mwake.

NIPASHE

Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia,  amesema hakuna Spika aliyewahi kuonyesha udhaifu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyoonyesha Anna Makinda.

Amesema Makinda ameligawa vipande vipande Bunge la 10 na kutumiwa na mhimili wa utawala.

Mbatia alisema badala ya Bunge kuisimamia serikali, lakini Makinda ameshindwa kuliongoza Bunge hilo kutokana na shinikizo la mhimili wa utawala na kulazimika kufuata matakwa ya CCM na hivyo kuliongoza kwa ubabe.

Alisema tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha  Samuel Sitta na Pius Msekwa ambao walionyesha weledi na kuliongezea heshima Bunge, lakini Makinda ameriharibu kutokana na kuacha kusimamia Katiba ya nchi katika kuliongoza Bunge hilo.

“Siku zote mwanamke ndiye huwa ni mtu wa mwisho kuligawa Taifa, lakini limekuwa ni jambo la ajabu sana kuona mwanamke huyo ambaye angekuwa mstari wa mbele katika kuitetea nchi hii, lakini ameamua lifie mikononi mwake, hata bila kuficha ameonyesha wazi kwamba anatumika na serikali na CCM, Makinda yeye siyo kiranja wa bunge  ni mratibu tu,” Mbatia.

Aliongeza: “ Badala ya Bunge kusimamia serikali kama Mhimili unaojitegemea, limejivua kazi yake na kuwa kiungo cha serikali na inalisimamia, na ndiyo  maana hata juzi mlisikia Serikali inasema imeoliongezea Bunge siku, badala ya Bunge lijiongezee lenyewe, hii ni fedheha.”

Mbatia alisema suala la kupelekwa bungeni kwa hati ya dharura na kujadiliwa miswaada mitatu ya mafuta na gesi ni ajenda ya siri ya kutaka kuiweka gesi kama dhamana ya CCM ya kupata fedha ya uchaguzi na  kwamba hicho ni kiashiria cha kuanza kuiuza nchi rejareja.

“Raslimali hizi badala ya kuwa neema kwa Watanzania, sasa inakuwa balaa, watu wachache wanataka kuwaibia Watanzania, hivi unawezaje kuwekaje miswaada hii muhimu kujadiliwa kwa pamoja na kuipeleka harakaharaka hivyo, sisi tumesema hatukubali kuona hujuma hizi zinafanyika dhidi ya rasilimali na Taifa,”Mbatia.

Mbatia alisema msimamo wa Wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) uko wazi, kwamba hawako tayari kujadiliwa miswaada hiyo kwa hati ya dharura na pia hawatashiriki wakati wa kuvunjwa bunge hilo Julai 9, mwaka huu.

Pia aliongeza kuwa hata wakiitwa katika meza ya maridhiano na Makinda hawatakuwa tayari kushiriki.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kwamba chama hicho kina  ajenga ya siri ya kuifanya gesi kusaidia kuwa dhamana  katika uchaguzi, alijibu kwa kifupi kwamba ni uzushi.

HABARILEO

Mlinzi wa usiku katika Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Florence Kazonde  amejinyonga baada ya kumuua kikatili kwa kumkaba koo mkewe aliyekuwa na ujauzito wa miezi tisa, Emilia Mzui.

Chanzo cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi. Tukio hilo limethibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, majirani na ndugu wa karibu wa familia ya marehemu hao waliokuwa wanaishi katika Kitongoji cha Namlangwa mjini Matai yalipo makao makuu ya wilaya ya Kalambo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Ramadhan Juma, alikiri kuwa Kazonde alikuwa mlinzi wa ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo zilizopo nje kidogo ya Mji wa Matai, lakini hakuwa mwajiriwa wa halmashauri hiyo.

“Kazonde alikuwa anatoka katika kampuni moja ya ulinzi…hakuajiriwa na Halmashauri hii,“ alisisitiza Juma.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alieleza kutokuwa na taarifa za mkasa huo kwamba akizipata atazitolea taarifa.

Hata hivyo taarifa kutoka Jeshi hilo la Polisi mkoani humo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Kweli kuna hilo tukio limetokea wilayani Kalambo … taarifa zipo tayari lakini kwa kuwa mie si msemaji wa Jeshi hili siwezi kutoa maelezo zaidi ya kina lakini nikiri kuwa tukio hilo limetokea …Kwa utaratibu wa Jeshi letu ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ndiye msemaji na si vinginevyo.

Baadhi ya majirani na ndugu wa karibu kwa masharti ya kutoandikwa gazetini walieleza kuwa walibaini vifo hivyo baada ya kufika nyumbani kwa wanandoa hao ili kuwasabahi lakini walikuta milango ya nyumba hiyo imefungwa kwa ndani.

“..Tulihisi labda walikuwa bado wamelala lakini kila tukibisha hodi ni watoto tu waliokuwa wakiitikia …… “Mazingira hayo yalitutia mashaka makubwa tukahisi kuwa kwa kuwa mke wake siku zake za kujifungua zilikuwa zimekaribia tuliamini kuwa walikuwa wamekwenda hospitali na kuwaacha watoto wakiwa wamejifungia ndani na kushindwa kufungua milango hiyo, “ alisema mtoa taarifa.

Ilielezwa kuwa ndugu na majirani hao waliamua kufungua mlango kwa nguvu ili wawatoe watoto hao wadogo nje ambao walikuwa wawili.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa baada ya kufungua mlango wa nyumba hiyo kwa nguvu mmoja wa watoto hao aliwaonesha ishara kuwa chumbani kwa wazazi wao kuna kitu cha kutisha ndipo walipolazimika kuingia chumbani humo na kuona mwili wa Kazonde ukiwa umening’inia darini ukiwa na kamba ya katani shingoni ambapo mwili wa marehemu mkewe ulikuwa kitandani.

“Inatisha na kusikitisha sana ….tuligundua kuwa wote wawili walikuwa wafu tukatoa taarifa mara moja katika Kituo cha Polisi hapa mjini Matai …… askari Polisi walifika na waganga ambao walifanyia uchunguzi miili hiyo na kuthibitisha kuwa Kazonde alikuwa amejinyonga baada ya kumuua mke wake kikatili kwa kumkaba koo,” aliongeza mmoja wa ndugu wa karibu.

Taarifa kutoka eneo hilo la tukio zinaeleza kuwa kwa muda mrefu wanandoa hao walikuwa wakigombana mara kwa mara ambapo mume alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine na kwamba kati ya watoto wao wawili mmoja sio wake ni wa mwanamume mwingine.

HABARILEO

Mahakama ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbende, Alei Charles (CHADEMA) kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukiri kumlinda mshtakiwa Wenceslaus Namwanda “Pepea” anayemiliki shamba la bangi.

Mshitakiwa Namawanda ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Mbende anakabiliwa na kosa la kumiliki shamba la bangi.

Hakimu wa mahakama hiyo, Adam Mwanjokolo alitoa adhabu hiyo baada ya mshtakiwa huyo mwenye miaka 30 kukiri kutenda kosa hilo mahamakani hapo .

Nimelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia kama yako (Alei)… hivyo utatumikia kifungo cha miaka miwili jela,“ Hakimu Mwanjokolo.

Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 14 , mwaka huu katika kijiji cha Mbende , saa 3 usiku.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa usiku huo wa tukio Alei aliwadanganya maofisa wa polisi kuwa mshtakiwa Namwanda hakuwa mkazi wa kijiji hicho hivyo aliwaelekeza kwa Mwenyekiti wa kijiji cha jirani.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka, maofisa hao walithibitishiwa na Mwenyekiti wa kijiji cha jirani kuwa mshitakiwa wanayemtafuta anaishi katika kijiji cha Mbende ambapo aliongozana nao hadi nyumbani kwake.

“Maofisa wa Polisi walipofika nyumbani kwa mshtakiwa Namwanda walipobisha hodi ghafla alitoka mtu baada ya kuona askari alitimua mbio, askari walifanikiwa kumkamata na ikagundulika kuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbende ambapo alikiri kuwa alifika nyumbani kwa mshtakiwa na kumtaarifu atoroke kwa kuwa alikuwa akitafutwa na Polisi,” alieleza Mwendesha Mashtaka.

Akijitetea mshitakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza. Pia ana watoto wategemezi wawili wa marehemu dada yake ambapo mama mzazi anaishi naye baada ya mumewe kufariki dunia.

Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad