KUTOKA
GAZETI LA NIPASHE.
Wabunge
wameikosoa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, wakisema haina jipya na
haitekelezeki.
Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzania bungeni, Freeman Mbowe, amesema bajeti ya serikali ya
mwaka 2015/16 haina unafuu wowote kwa Mtanzania wa kawaida, bali bajeti
iliyojaa maneno matamu ya kuhadaa umma.
“Ukipitia
baadhi ya vifungu utabaini kuwa vina lengo la kutoa kauli nzuri za matumaini na
ahadi zisizotekelezeka, ni bajeti ya kikampeni kwa ajili ya uchaguzi,” alisema
na kuongeza:-“Wamedandia
hoja ya Kambi ya Upinzani ya kutoa pensheni kwa wazee tangu bajeti 2012/13 na
serikali ikasema jambo hili halitekelezeki, leo wanazungumza wataanzisha na
hakuna sheria ya utekelezaji na haiko katika sheria zitakazoletwa bungeni,
hakuna mzee atakayelipwa pensheni katika mwaka ujao wa fedha,” alisema.
Mbowe
alisema ongezeko la kodi ya mafuta ni tishio kwa Mtanzania wa kawaida, kwani
kila kitu kitapanda gharama kwa Sh. 100 kwa dizeli na petroli, huku mafuta ya
taa ikiongezeka kwa Sh. 150, yataathiri wananchi na kuongeza gharama za maisha
Mbowe
alisema katika soko la dunia bei ya mafuta inashuka kila siku, huku Tanzania
ikiongeza badala ya kupungua.
Alisema
Watanzania wanadanganywa tena kwa fedha za kodi ya mafuta zitakwenda kwenye
mfuko wa Umeme Vijijini (Rea), kwani mwaka uliopita fedha zilizoingizwa kwenye
mifuko maalum ni fedha zilizotakiwa zisitumike, lakini imezichomoa na kutumia
kwa mambo mengine, hivyo siyo kweli kuwa zitatumika kwa umeme.
“Bajeti
inaweza ikasomwa ikaonekana ni tamu, tatizo kubwa ni utekelezaji wa bajeti,
Chama hiki (CCM) na serikali hii zimeshachoka, hakina uwezo wa kutekeleza
bajeti, wamebakiza miezi minne waondoke Ikulu, watuachie sisi tuingie,” alisema
na kuongeza:-“Inashangaza
kuona bajeti inasomwa leo, lakini nusu ya mawaziri hawapo katika bajeti ya
serikali yao, Naibu Waziri wa fedha anaingia wakati waziri anahitimisha
bajeti…wabunge wa upinzani hususan wa Chadema wote wameacha majukumu yao kuja
kusikiliza bajeti.”
Naye, Mbunge
wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema haoni kipya ndani ya
bajeti hiyo kwa sababu kila kitu ni kile kile.
“Kwa kweli
nilishindwa kufatilia kwa sababu ni maneno yale yale, ya watu wale wale ya siku
zote na ya miaka yote…wakitaka fedha ni mafuta na bia, lakini safari hii
hawakwenda kwenye maji ila yale yale tu,” alisema.
Kuhusu
kupandisha kodi ya mafuta, alisema serikali haijawahi kufikiria vyanzo vipya
vya mapato.
Alisema
hakuna mji uliojengwa na kuwa chanzo kikubwa cha mapato kama Dar es Salaam
kutokana na majengo makubwa yaliyojengwa.
“Hayo
majengo ni chanzo kikubwa cha mapato nchi nyingi zinaingiza mapato kwa kutumia
majengo makubwa yaliyojengwa,” alisema.
Mbunge wa
Vunjo (TLP), Augustino Mrema, alisema bajeti ya mwaka huu haina tofauti na
mwaka jana kwani kila kitu ni kile kile hakuna jipya.
“Ni bora
wangekaa wenyewe wakaipitisha, sisi (wabunge) tukabaki nyumbani, kwa sababu
kila tunachopitisha hakitekelezeki,” alisema.
Mbunge wa
Viti Maalum (CCM), Esther Bulaya, alisema bajeti ya serikali haiwezi kumsaidia
mwananchi wa kipato cha chini kutokana na kupandisha bei ya mafuta.
“Kwa kawaida
mafuta yakipanda ni lazima kila kitu kitapanda bei, hivyo kuwepo kwa ongezeko
la mafuta ni kuwafanya wananchi kuendelea kuwa maskini tofauti na ilivyokuwa
ikikusudiwa kuwa uenda bajeti ingekuwa ya kuwasaidia wananchi wenye kipato cha
chini,” alisema
Aidha,
alisema inashangaza kuona kuwa fedha za matumizi zimekuwa nyingi huku fedha kwa
ajili ya maendeleo zikipunguzwa.
Naye, Mbunge
wa Kisesa (CCM), Luaga Mpina, ameibeza bajeti na kudai kuwa haina jambo lolote
ambalo ni jipya kwani kila jambo linaonekana kuwa ni la kawaida.
Alisema
serikali haikuwa na sababu ya kuongeza ongezeko katika mafuta kuwa ilikuwa na
uwezo wa kutafuta vyanzo vingine vya mapato tofauti na kujielekeza katika
mafuta.
Mpina
alisema pamoja na serikali kudai kwamba wataweza kupeleka fedha za miradi
katika wakala wa Umeme vijini, lakini kimsingi pesa hizo hazipelekwi.
Waziri
Kivuli wa Fedha wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, James Mbatia, alisema:-“Ni bajeti
ya kufurahisha wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa sababu
upungufu huo unatokana na ongezeko la thamani ya Dola ya Marekani kuchupa
kutoka Shilingi 1,650 kwa mwaka jana hadi Shilingi 2,054 kwa viwango vya wiki
hii…Bajeti kwa ajili ya matumizi ya serikali ni kubwa kuliko Bajeti ya
Maendeleo.”
Mbatia
alisema bajeti ya mwaka huu, itawaumiza Watanzania kwa kuwa serikali
imepandisha kwa kiwango cha juu mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa huku
ikilenga kukopa zaidi ya shilingi trilioni sita na kuongeza kasi ya ukuaji wa
deni la Taifa.
Mbunge wa
Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji, Peter Msigwa, alisema bajeti hiyo ni ya
kiini macho na haiwezi kutekelezeka kwa kuwa hata bajeti inayoishia Juni 30,
mwaka huu imetekelezwa kwa asilimia 28 tu kutokana na wahisani wanaochangia
bajeti ya Taifa kugoma.
“Tunasikitika
bajeti hii itaiacha nchi ikiwa kapu tupu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.
Wamekuja na bajeti ya makusudi kwa sababu wanafahamu wako kwenye kupindi cha
mpito cha kukabidhi nchi kwa Ukawa…Hakuna muujiza utakaotokea na kuifanya
bajeti iliyoletwa bungeni itekelezeke,”alisisitiza Msigwa.
FELIX
MKOSAMALI
Mbunge wa
Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema bajeti iliyowasilishwa
inalenga kuwafurahisha wasanii na si wananchi kwa kuwa ni bajeti ya maigizo
kutokana na hofu ya kuanguka kwa chama tawala na si kupanua wigo wa maendeleo
ya Watanzania.
Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment