Baadhi ya noti bandia walizokutwa Nazo. |
Naibu kamishna wa jeshi la polisi Mkoani Simiyu Charles
Mkumbo akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) baadhi ya pesa bandia
ambazo zilikamatwa askari wa jeshi la polisi
|
Jeshi la polisi mkoani Simiyu linawashikilia askari wawili wa
jeshi la magereza na polisi kwa kukutwa na noti bandia ikiwa ni pamoja na sare
za jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ).
Akitoa taarifa za kukamatwa kwa askari hao Naibu Kamishna wa
jeshi la polisi Mkoani Simiyu Charles Mkumbo alisema kuwa askari hao
walikamatwa juzi majira ya saa 9 mchana katika mtaa wa Old Maswa kata ya
Nyakabindi Wilayani Bariadi.
Alisema askari hao walifika kwenye kibanda cha M-pesa
kinachomilikiwa na Mwalimu wa Shule ya sekondari Old Maswa Kassian Luhende
(29), wakiwa na pikipiki yenye namba za usajili T-403 CXW aina ya Sunlg kwa
lengo la kuweka fedha hizo kweye simu.
Alisema baada ya Mwalimu huyo kupokea fedha kiasi cha noti 10
zenye thamani ya Shilingi 10,000 alizitilia shaka ambapo alipoendelea kuzikagua
zaidi alizigundua kuwa siyo fedha halali.
Mkumbo alieleza kuwa Mwalimu huyo baada ya kugundua fedha
hizo kuwa ni feki, alichukua jukumu la kuwajulisha majirani zake ili kuomba
Msaada wa kuweza kuwakamata askari hao baada ya kugundua siyo watu wema.
Aidha alieleza kuwa baada ya mwalimu kutoa taarifa kwa
majirani, wananchi walikusanyika na kuanza kuwahoji askari hao, ndipo askari
mmoja alipotoa kitambulisho kuwa yeye ni askari na mwingine kujitambulisha kuwa
ni dereva bodaboda.
Alibainsiha kuwa wananchi baada ya kuambiwa hivyo waliwatilia
shaka zaidi ambapo walitoa taarifa Kituo cha polisi Bariadi, na askari kwenda
kuwakamata.
Mkumbo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari mwenye namba H
2420 PC Seleman Juma (25) ambaye ni askari wa kikosi cha kutuliza gasia FFU
Mkoani Simiyu, na askari namba B.6499 WDR Edmund Masaga (28) ambaye ni askari
Magereza wilayani Bariadi.
Kamanda Mkubo alieleza kuwa baada ya askari hao kukamatwa
mmoja wao PC Selemani Juma alipopekuliwa katika mfuko wa suruali yake alikutwa
na noti zingine za Bandia za elfu kumi kumi na jumla yake kama zingelikuwa
halali zingelikuwa na thamani ya Shilingi 1,920,000.
Mbali na hilo Mkumbo alieleza kuwa Askari huyo alipokwenda
kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na sare za JWTZ ambazo ni Pensi 4, T-shirt
2, Kombati 1 pamoja na Kitambaa.
Hata hivyo Mkuu huyo wa polisi alieleza kuwa uchunguzi zaidi
unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani ya mkoa
huo, huku akieleza kuwa mara baada ya uchunguzi kukamilika askari hao
watachuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kisheria.
Alitoa onyo kwa askari Mkoani Simiyu kuacha tamaa ya pesa na
badala yake waridhike na ajira zao zinazowapatia pesa halali, huku akieleza
kuwa kwa atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheraia na nidhamu.
Pata
Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia
tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment