HOTUBA YA
NDG. ZITTO KABWE KWA TAARIFA YA KAMATI YA KILIMO NA KAMATI YA ARDHI HIYO HAPO
CHINI
Kilimo
Mheshimiwa
Spika,
Mwaka 2014
umekuwa ni mwaka mwema kwa sekta ya kilimo nchini. Uzalishaji umeongezeka,
mazao ya chakula tumezalisha ziada kwa 125% ya mahitaji yetu ya chakula. Kwa
upande wa mazao ya biashara, zao la Korosho limeweka rekodi Mpya kwa kuzalisha
takribani tani 200,000 za Korosho.
Hata hivyo
wananchi hawana furaha na mafanikio haya kwa sababu ya kutojiandaa kwetu.
Wakulima wa mahindi hawajalipwa na bado tunahangaika na soko la mahindi na
mchele. Serikali bado inaruhusu Mchele kutoka nje kuingia nchini ilihali mchele
wetu unakosa soko. Maghala ya kuhifadhi nafaka bado kujengwa na Serikali
inasema inaongea na nchi ya Poland kupata mkopo wa kujenga maghala. Ni kama
vile Serikali haikuwa na mipango wakati inajua kuwa uzalishaji utaongezeka
zaidi ya maradufu.
Mheshimiwa
spika,
Mwaka 2014
tunaweza kuwa tumevuka $1bn ya mauzo nje katika sekta ya kilimo kufuatia
mafanikio makubwa katika Korosho na Tumbaku. 60% ya mapato ya fedha za kigeni
katika kilimo yanatokana na mazao 2 tu: Tumbaku na Korosho. Mazao haya
yanalimwa mikoa ya Tabora, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Katavi na Kigoma.
Ukitazama
takwimu za Bajeti, mikoa hii ndio yenye kupata fedha kidogo zaidi za miradi ya
maendeleo kuliko mikoa mingine nchini. Vile vile wakulima wa mikoa hii ndio
wananyonywa zaidi kutokana na mfumo mbovu wa usambazaji wa pembejeo na soko la
mazao yao.
Taarifa ya
kamati ya PAC iliyopitishwa na Bunge wiki iliyopita inaonyesha namna mfumo wa
kifisadi katika zao la Korosho unavyowaacha wakulima wa Korosho katika
umasikini wa kutupwa. Wakulima wa Lindi na Mtwara wanapewa pembejeo zilizo
expire na hakuna hatua inayochukuliwa.
Bado
tunaendelea kuuza nje Korosho ghafi na ku export maelfu ya kazi ambazo
zingefanywa na vijana na wanawake wa Mtwara. Korosho nyingi inaibiwa vijijini
na vyama vya msingi havilindi maslahi ya mkulima mdogo.
Mheshimiwa
spika, napendekeza kwamba sasa tuseme basi na kuacha kabisa kuuza nje Korosho
ghafi. Tunapoteza wastani wa dola 115m kila mwaka kwa kuuza korosho ghafi nje
ya nchi. Iwapo tungekuwa tunauza Korosho iliyobanguliwa kwenda nje Tanzania
ingekuwa na mapato ya fedha za kigeni zaidi ya dola 500m kwa mwaka kwa Korosho
peke yake.
Napendekeza
tutumie makato ya ' export levy' katika kipindi cha miaka 5 ijayo kujenga
viwanda vya kubangua Korosho vijijini kwa ushirikiano kati ya vyama vya
ushirika, serikali na sekta binafsi.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Tumbaku naomba Serikali ilieleze bunge hatua ambazo
imechukua dhidi ya viongozi wa ushirika waliotafuna fedha za wakulima wa
tumbaku mkoa wa Tabora. Naibu Waziri Kilimo alitamka hapa kwamba jalada lipo
kwa IGP, tuelezwe hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya ubadhirifu mkubwa huo na
ni namna gani wananchi wanafidiwa kutokana na upotevu huo mkubwa wa fedha.
Mheshimiwa
spika, narejea pendekezo langu kwamba Serikali ianzishe rasmi Hifadhi ya jamii
kwa wakulima ili sio tu wapate mafao ya muda mrefu na wa mfupi lakini pia
kuwezesha wakulima kufaidika na kilimo kwa kupata mikopo ya pembejeo na
shughuli za kuongeza thamani bidhaa zao.
Akiba ya
wakulima inaweza kabisa kusaidia benki ya kilimo kwa mfuko wa pensheni kwa
wakulima kuwekeza hisa zake kwenye Benki hiyo na hivyo miradi mikubwa ya kilimo
kuwa na chanzo cha fedha za maendeleo badala ya kutegemea Bajeti ya serikali.
Ardhi
Mheshimiwa
Spika,
Kamati ya
PAC imefanya uchunguzi maalumu kuhusu makusanyo madogo katika wizara ya ardhi
yanayotokana na kutokuwa na rekodi sawa sawa za viwanja nchini. Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali alieleza katika taarifa yake ya mwaka 2012/13
kwamba, viwanja zaidi ya 263,000 jijini Dar Es salaam havipo katika rekodi ya
Msajili wa hati.
Maana yake
ni kwamba Serikali inapoteza mapato zaidi ya tshs 83 bilioni Kwa mwaka. Viwanja
hivi vinashikiliwa na maafisa wa wizara ya ardhi. PAC imependekeza kwamba mara
moja Serikali ianze kutoa Hati za Ardhi za kidigiti ( digital land titles) na
kuziwianisha na nambari za utambuzi wa mlipa kodi ( TIN ).
Hatua hii
itaondoa kabisa tatizo la hati zaidi ya moja kwa kiwanja kimoja kwa mtu zaidi
ya mmoja. Mfumo huu uanze kwa Manispaa za Jiji la Dar Es Salaam na baadaye nchi
nzima. Serikali, kwa kuwa haina Bajeti, ifanye mradi huu kwa kutumia PPP kwa
kushirikisha sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika,
napendekeza kufanya marekebisho katika mapendekezo ya taarifa ya taarifa ya
kamati kwa kuweka pendekezo la kuitaka Serikali kuanza mradi huu katika mwaka
wa fedha unaoanza mwezi Julai mwaka huu.
Utalii
Mheshimiwa
Spika, taarifa ya Kamati inaonyesha kuwa Waziri wa Utalii ameshindwa kutoa
tangazo la Serikali ili tozo Mpya za concession zianze kutozwa. Tozo Mpya
hazitozwi toka mwaka 2011 na hivyo TANAPA kupoteza zaidi ya shilingi 80
bilioni.
Wafanyabiashara
walikwenda mahakamani na kushindwa kesi. Waziri miezi minne amekaa bila
kutekeleza hukumu. Waziri anapaswa kuwajibishwa kwa kupotezea mapato Serikali.
Bunge limuazimie Waziri huyu iwapo mpaka mwisho wa siku Leo atakuwa hajatoa
tangazo la Serikali.
Zitto Kabwe.
2/2/2015
|
No comments:
Post a Comment