|
KESI ya
mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Mkoani Iringa na
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Daudi Mwangosi
inaendelea kusikilizwa kuanzia leo, Februari 12 hadi Februari 18,2015.
Kesi hiyo
inayomkabili aliyekuwa askari wa jeshi la Polisi, Pacificius Cleophace Simoni
itaendelea kusikilizwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa,
Mary Shangali baada ya upande wa mashtaka kuileza mahakama hiyo kwamba
uchunguzi wake umakamilika.
Jaji
Shangali aliahidi kuwaruhusu wanahabari kushiriki kikamilifu katika kesi hiyo
ikiwa ni pamoja na kupiga picha kabla shughuli za mahakama hiyo hazijaanza.
Uamuzi huo
wa Jaji unalenga kumaliza kitu kinachoonekana kama ghasia zisizo na maana
wanazofanyiwa wanahabari wakati mtuhumiwa huyo anapofikishwa mahakamani.
Mbali na
kufikishwa mahakamani hapo akiwa katika magari tofauti na yale yanayotumika
kubeba watuhumiwa wengine, baadhi ya Polisi wanaofuatilia kesi hiyo wamekuwa
wakimzingira mtuhumiwa huyo ambaye mara zote amekuwa akivaa vazi linaloficha
sura yake na wakati huo huo wamekuwa wakiwafukuza na kuwazuia wanahabari kupiga
picha za mtuhumiwa huyo.
Wakati
ikisikilizwa kwa mara ya kwanza Februari 13, mwaka jana 2014, Wakili wa upande wa
mashtka, Adolph Maganga alisema, kwa kukusudia mtuhumiwa Pacificius Cleophace
Simoni anatuhumiwa kumuua Mwangosi kinyume na kifungu cha sheria ya kanuni ya
adhabu namba 196 sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Alisema katika
tukio hilo lililotokea Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilayani
Mufindi mkoani Iringa, mshtakiwa alifyatua bunduki yake na kusababisha kifo cha
marehemu, papo hapo.
Alisema siku
ya tukio marehemu alikuwa Nyororo kwa ajili ya kuripoti na kutoa taarifa kwa
umma juu ya mkutano uliokuwa ufanywe na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa.
Alisema
mshtakiwa akiwa mmoja wa wafanyakazi wa Polisi, waliwasihi Chadema wasifanye
mkutano huo kabla wafuasi wake hawajaanza kurusha mawe kwa Polisi na baadhi yao
kupata majeraha.
Kutokana na
mzozo huo, wakili huyo wa serikali alisema polisi walipiga mabomu ya machozi
ili kuwatawanya wafuasi hao kabla mshtakiwa huyo hajamfyatulia bomu marehemu.
Wakili huyo
aliwasilisha ramani ya eneo la tukio, ripoti ya mtaalamu wa milipuko na ripoti
ya daktari aliyechunguza mwili wa marehemu Mwangosi na gazeti la Mwananchi la
Septemba 3, 2012 lililochapisha picha ya
tukio hilo katika ukurasa wa mbele kama vielelezo vinavyohusiana na kesi hiyo.
Wakili wa
upande wa utetezi Lwezaula Kaijage alitaja mambo wanayokubaliana katika kesi
hiyo kuwa ni jina na anuani ya mshtakiwa na kwamba marehemu Mwangosi alikufa
kifo ambacho si cha kawaida.
Na kwamba
mshtakiwa Simoni alikamatwa na amefikishwa mahakamani akihusishwa na mauaji
hayo.
Wakili
Kaijage alisema vielelezo vingine vilivyoletwa na upande wa mashtaka
hawakubaliani navyo kwakuwa vinahitaji ushahidi kutoka kwa wahusika.
|
No comments:
Post a Comment