|
Rais wa Jakaya Mrisho Kikwete akifanya
mazungumzo na Rais wa Ujerumani Mhe. Joachim Gauck pamoja na ujumbe wake Jana Tarehe.03.02.2015. (PICHA NA FREDDY
MARO).
Rais wa
Jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck ameanza ziara yake ya siku tano nchini
Tanzania Februari 03,2015, ambapo amepokewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete huku wakikubaliana kuboresha
sekta mbalimbali nchini hususani ya biashara.
Akizungumza jana
Februari 03,2015, Ikulu jijini Dar es Salaam Rais katika mazungumzo na
waandishi wa Habari mara baada ya kufanya mazungumzo ya faragha, Dkt. Jakaya
Kikwete ameiomba Serikali ya Ujerumani kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo
ya sekta ya gesi, Viwanda pamoja na Biashara ili kukuza uchumi huku akisisitiza
kuwa mahusiano ya kisiasa na kijamii kati ya Tanzania na Ujerumani yamezidi
kuimarika.
Akitoa
taarifa ya makubaliano waliyoafikiana, Rais Kikwete amesema kuwa Rais wa
Ujerumani Joachim Gauck amesema kuwa Ujerumani iko tayari kuwekeza miradi 51 ya
kiuchumi yenye thamani ya takriban Euro Milion 300 karibu Bilion 621 kama
mwanzo wa kujenga uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ujerumani.
Rais Kikwete
amesema kuwa msisitizo zaidi ameuweka katika uwekezaji kwenye sekta ya gesi
ambayo endapo itafanikishwa kuenea Tanzania itasaidia kuondoa tatizo la
uharibifu wa misitu akitolea mfano wa Jiji la Dar es Salaam ambalo hutumia
zaidi ya tani elfu 40 za mkaa kwa mwaka.
Kwa upande
wake Rais Joachim Gauck amesema kuwa Ujerumani iko tayari kushirikiana na
Tanzania kibiashara na Kiuchumi na ndiyo maana katika msafara wake ameongozana
na wadau mbalimbali wa sekta za kiuchumi kutoka Ujerumani wakiwemo
wafanyabiashara wakubwa na waziri husika kwa lengo la kujifunza na kuangalia
fursa za uwekezaji.
Rais Gauck
ameongeza kuwa anaridhishwa na jinsi Tanzania inavyosimamia haki za binadamu
pamoja na kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa, umoja wa kitaifa na maendeleo
na kwamba Ujerumani itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali
za maendeleo na Tanzania.
“Tuko hapa
kwa ajili ya kujifunza na kuangalia namna ya kusaidiana kiuchumi na kuimarisha
biashara baina ya Ujerumani na Tanzania” Amesema Rais Gauck.
Amesema
“Ujerumani na Tanzania zimekuwa na ushirikiano mkubwa wa kihistoria tangu mwaka
1961 na ndiyo maana kuna shule, makanisa n.k vilivyojengwa na wajerumani.... na
pia imekuwa ikiisaidia Tanzania kifedha”
Ameipongeza
Tanzania kwa kushiriki kikamilifu katika jitihada za kutafuta amani katika
mataifa mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kama vile Sudani
Kusini na DRC.
Wakijibu
maswali ya waandishi wa Habari, Rais Kikwete amejibu swali lililohusu mgogoro
wa mpaka katika ziwa Nyasa ambapo amesema kuwa mgogorohuo unaendelea
kushughulikiwa.
Swali
lingine lilihusu hali ya Uhuru wa vyombo vya habari ndani ya Tanzania kufuatia
kufungiwa kwa gazeti la The East African, pamoja na kitendo cha askari kuwapiga
wafuasi wa CUF waliokuwa wakiandamana January 27 mwaka huu.
........Akijibu
maswali hayo Rais Kikwete amesema “Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani
ambazo zinajali sana uhuru wa vyombo vya habari na hata sasa kuna magazeti
mengi yaliyosajiliwa na yanafanya kazi zake kwa uhuru”
Kuhusu
kufungiwa kwa gazeti la The East African Rais Kikwete amesema suala hilo
linashughulikiwa na mamlaka husika kwa sheria na taratibu stahiki za usajili wa
magazeti.
Kuhusu
kupigwa kwa wafuasi wa CUF amesema kuwa wafuasi wale akiwemo Mwenyekiti wao
Prof Ibrahim Lipumba hawakufuata taratibu za kukusanyika ndiyo maana yalitokea
yaliyotokea.
“Kwa
Tanzania tuna taratibu zetu za vyama vya siasa kukusanyika, wala hatubani haki
na uhuru wa wapinzani... tena wapinzani wanafanya mikutano mingi zaidi kuliko
chama tawala.... lakini ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha
waendelee kuvunja sheria na taratibu”
Kuhusu hali
ya usalama na tishio la ugaidi, Rais Kikwete amesema kuwa anatambua kuwa
Tanzania haiwezi kujiamini kwa asilimia 100 kuwa iko salama na haitakumbwa na
vitendo hivyo, lakini ana imani kuwa kiwango cha usalama ni kikubwa na kwamba
Tanzania ina uzoefu na matukio hayo ikikumbukwa tukio la ulipuaji wa ubalozi wa
Marekani ambapo baadhi ya waliohusika walikuwa ni wafuasi wa kundi la Al
Shabaab.
“Mara kwa
mara tupo katika tahadhari ya tishio hilo, na bahati nzuri tunashirikiana
vizuri na vyombo vya usalama vya kimataifa vikiwemo vya Ujerumani kuhakikisha
kuwa Tanzania inakuwa salama lakini si salama kwa asilimia 100” amesema Rais
Kikwete
Kwa upande
Rais Gauck ameipongeza Tanzania na kusema kuwa ni mfano wa kuigwa kwa jinsi
inavyojituma kupeleka majeshi yake katika mataifa yenye machafuko, kwani kwa
kufanya hivyo inajilinda yenyewe.
Rais Gauck
anatarajiwa pia kutembelea Zanzibar, Bagamoyo, hifadhi ya Taifa ya Serengeti na
ameomba akae Arusha kwa muda kabla ya kurejea Ujerumani.
|
No comments:
Post a Comment