|
NIPASHE.
Serikali ya
Tanzania imesema itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na wageni wanaokuja
kutembelea vivutio vya kitalii kutumia viwanja vya ndege vilivyopo nchini
ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.
Hatua hiyo
imechukuliwa kufuatia Kenya kuendelea kuzuia magari ya kitalii yaliyosajiliwa
Tanzania kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa ajili
ya kuchukua na kushusha watalii.
Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, ( Pichani juu) alisema
jana Februari 10,2015, kuwa serikali imesikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na Kenya
kwani uamuzi wake hauendani na dhamira njema ya mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
“Tanzania
haitazuia magari ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nyingine
yoyote kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii
wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi hizo:-Mwakyembe.
Alisema
Tanzania itaheshimu na kuzingatia mkataba huo ili kulinda undugu na urafiki
uliopo kati ya nchi hizo wakati ikiendelea kutafakari hatua za kuchukua ili
kuondoa bughudha kubwa itakayotokea kwa watalii na wasafiri wanaopitia uwanja
wa Jomo Kenyatta.
NIPASHE.
Mkazi wa
Ilala Sharifu Shamba, jijini Dar es Salaam, anatuhumiwa kumuua rafiki yake
kisha kumfukia kwenye shimo alilochimba na kulisakafia uani kwenye nyumba
aliyokuwa akiishi mtuhumiwa.
Mauaji hayo
yanadaiwa kufanywa Julai, mwaka jana 2014, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kushindwa
kumlipa rafiki yake huyo Sh. milioni 35.
Inadaiwa
kuwa marehemu alimpa mtuhumiwa huyo fedha hizo ili akamnunulie gari na kwamba,
baada ya kudaiwa muda mrefu, ndipo alipoamua kufanya ukatili huo.
Habari
zinaeleza kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa alimpigia simu rafiki
yake huyo na kumtaka aende bandarini kuchukua gari hilo kwa madai kwamba,
lilikuwa limewasili.
Kwa mujibu
wa habari hizo, wakati huo mtuhumiwa alikuwa bandarini akimsubiri rafiki yake
huyo. Inadaiwa rafiki yake huyo alikwenda hadi bandarini na kuonana na
mtuhumiwa huyo.
Hali hiyo
ilimfanya rafiki yake huyo kulazimika kuondoka baada ya kushindwa kuhimili
mzunguko waliokuwa wakifanyiwa na mtuhumiwa.
Baada ya kushindwa kupata gari
alilolitarajia, mtuhumiwa aliamua kurudi na rafiki yake huyo nyumbani kwake
(mtuhumiwa), Ilala ambako alitekeleza mauaji hayo na kumzika.
MWANANCHI.
Mtafiti
mwandamizi wa taasisi ya maendeleo ya kimataifa ‘SID’ Edmund
Matotay, amesema kuimarika kwa uchumi wa nchi hakujasaidia kuondoa hali
ya umaskini wa wananchi.
Amesema
licha ya mageuzi makubwa ya makusanyo ya pato la Taifa na kuongezeka kwa
uzalishaji katika sekta mbalimbali bado wananchi wengi wanaishi katika hali ya
umaskini mkubwa.
“Bado
Tanzania inategemea misaada kutoka nje kwa asilimia 41 kutokana nakutokuwepo
usimamizi mzuri wa kukusanya kodi:- Matotay.
Alisema kwa
kawaida ukuwaji wa uchumi wa nchi yoyote lazima uendane na mabadiliko ya maisha
ya wananchi lakini kinachoshuhudiwa nchini ni tofauti.
MWANANCHI.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe (Pichani kulia ) ameuvunja uongozi wa chama hicho
kwenye majimbo ya Ukonga na Ilala kutokana na kutoelewana kwa muda mrefu baina
ya viongozi na kutofanya vizuri kwa chama hicho kwenye Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana 2014.
Habari
zilizothibitishwa na Mbowe zinaeleza kuwa mwenyekiti huyo aliuvunja uongozi huo
wiki mbili zilizopita baada ya kikao cha siri na viongozi wa majimbo hayo
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Klabu ya Billicanas iliyopo katikati ya jiji.
Pamoja na
CCM kuibuka na ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo wa ngazi ya mwanzo ya
uongozi, CHADEMA iliongoza kwa upande wa upinzani ingawa haikuwa na matokeo
mazuri kwenye majimbo hayo mawili.
Katika
uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa asilimia 79.4 katika nafasi ya uenyekiti wa
mitaa, Chadema asilimia 15.1 na CUF asilimia 4.6. Vyama vingine kwa ujumla
vilipata asilimia 0.9.
MWANANCHI.
Taasisi ya
Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) imembadilishia hati ya mashtaka
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la
kupokea rushwa ya Sh 323 milioni toka kwa James Rugemalira fedha ambazo ni
sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Esrow.
Katika hati
mpya iliyosomwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Leonard Swai
mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Emillius Mchauru aioneshi tena
kuwa fedha zilizopokelewa na Mujunangoma toka kwa Rugemalira ni sehemu ya fedha
za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Swai kupitia
hati hiyo mpya alidai kuwa Februari 5, 2014 Mujunangoma akiwa mtumishi wa
serikali kama Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma alipokea rushwa ya Sh Sh 323 milioni
kupitia akaunti yake namba 00120102602001 iliyopo kwenye benki ya
Mkombozi .
Alidai kuwa
mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard
Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na
mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa
kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
MTANZANIA.
MCHAKATO wa
kupata Katiba Mpya ya nchi unadaiwa kugubikwa na wingu la ufisadi hali
iliyosababisha Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuhoji
tenda ya uchapwaji wa nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa kwa
gharama ya Sh bilioni 6.
Hatua hiyo
inakuja huku Watanzania wakiwa wanasubiri kupiga kura ya maoni inayotarajiwa
kufanyika Aprili 30, mwaka huu, ambapo inaelezwa taratibu za manunuzi
zilikiukwa kwa baadhi ya kampuni zilizopewa kazi hiyo kuwa na walakini.
Kwa mujibu
wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, taasisi zote za umma zinatakiwa
zitangaze zabuni kabla ya kutoa zabuni husika.
Kutokana na
sheria hiyo, inaelekeza taarifa za zabuni husika hutangazwa kupitia jarida na
tovuti ya PPRA jambo ambalo linadaiwa halikufanywa na Wizara ya Katiba na
Sheria.
Kwa mujibu
wa taarifa hizo, kila nakala ya Katiba Inayopendezwa inachapishwa kwa gharama
ya Sh 3,000.
“Kwenye
hizo kampuni zilizopewa hiyo kazi, nyingine hata uwepo wake una walakini, hii
haikuwa kazi ya dharura kiasi hicho, lakini pia kutoa zabuni ya Sh bilioni 6 za
umma kwa kujuana tu bila kufuata taratibu ni jambo la kushangaza,”
kilipasha chanzo chetu.
HABARI LEO.
TAASISI ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) imesema imejipanga
kikamilifu kuhakikisha inashughulikia vitendo vya utoaji na upokeaji rushwa
katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza
jana wakati wa ufunguzi wa jengo la taasisi hiyo mkoani Kigoma lililogharimu Sh
bilioni 1.2, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea alisema
anasubiri kuanza kwa ratiba ya Tume ya Uchaguzi ili iweze kuanza kutekeleza
jambo hilo kwa kufuata sheria za uchaguzi.
Alisema
taasisi yake imeshaanza kuona viashiria vya utoaji rushwa vinavyofanywa na
baadhi ya watu walioonesha nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutoa
vitu mbalimbali zikiwemo fulana, chupa za chai na vitu vinavyofanana na hivyo.
Hata hivyo,
alisema kwa sasa haitaweza kuwakamata wala kuwahoji watu hao kwa kuwa si
wagombea rasmi kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, lakini alibainisha kuwa
vijana wake wanafuatilia kwa karibu nyendo zinazofanywa na watu hao.
Sambamba na
kujipanga, Hosea alitoa wito kwa wananchi kuchukia vitendo vya kupokea rushwa
wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu kwani vinawapotezea haki ya kuchagua
mgombea mwenye sifa badala yake hushawishiwa kuchagua kwa rushwa.
Source:-Millardayo.
|
No comments:
Post a Comment