Ikiwa imesalia miezi kumi kabla ya
kufanyika Uchaguzi Mkuu 2015,unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hadi sasa
majimbo sita yako wazi baada ya wabunge wanaoyaongoza kutangaza kutogombea tena
ubunge.
Ni wazi kuwa
uamuzi wa wabunge hao, wengi wao wakiwa wameamua kupumzika baada ya kushikilia
viti hivyo kwa vipindi zaidi ya viwili, utaibua ‘vita kali’, vikianzia ndani ya
vyama wakati wa kura za maoni na baadaye baina ya vyama wakati wa kuomba ridhaa
kwa wananchi.
Mbunge
aliyetangaza kuachia jimbo hivi karibuni ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye
amekuwa mbunge wa Katavi kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 2000 akisema
anakwenda kufanya kitu kingine.
“Wapo ambao
hawatagombea sababu wanataka kuwania urais. Wapo waliotangaza kutogombea sababu
tu ya demokrasia na kutaka kuwapisha wengine. Hilo ni jambo zuri,” alisema
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala.
Profesa
Mpangala alikumbushia pendekezo lililokuwapo katika Rasimu ya Katiba
iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilipendekeza kuwa mwisho
wa kugombea uwe vipindi vitatu.
“Pendekezo
lile lilikuwa zuri ili kuwaondoa wanaokaa madarakani zaidi ya miaka 50, ila
wapo wanaotangaza kutogombea kwa sababu tu za kisiasa,” alisema.
Vyama vya
upinzani pia safari hii vitakuwa na kazi ngumu ya kuteua wagombea baada ya
kufikia makubaliano chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kusimamisha
mgombea mmoja kutoka miongoni mwao katika ngazi zote kuanzia Serikali za Mitaa.
Vyama
vilivyo chini ya mwavuli huo ni NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD, wakati chama
kipya cha ACT - Tanzania kilionyesha nguvu katika uchaguzi wa viongozi wa
Serikali za Mitaa na kama hakitamaliza mgogoro, kinaweza kuwa tishio wakati wa
kutafuta kura za wananchi utakapowadia.
Bernard
Membe (Mtama)
“Unajua
nimekuwa mbunge wenu kwa vipindi vitatu. Hivi leo ninawaaga rasmi kuwa
sitagombea tena nafasi hii ya ubunge,” alisema Membe katika hafla ya Mwaka Mpya
aliyoandaa nyumbani kwake Januari, 2013.
Membe ni
miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania urais, ingawa amekuwa
akieleza kuwa anasubiri “kuoteshwa”. Iwapo atajitosa kugombea kuwania nafasi
hiyo ya juu nchini, jimbo hilo litabaki wazi na tayari linawaniwa na kiongozi
mmoja wa juu wa CCM.
Hezekiah
Chibulunje (Chilonwa)
Kiongozi
huyo alitumia staili nyingine kutangaza uamuzi huo. Alichagua Desemba 26, mwaka
jana kufanya ibada ya kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kuwa Mbunge wa Chilonwa
tangu 1995 na akatangaza kutogombea kwa maelezo kuwa umefika wakati wa
kupumzika na kuwapisha wengine.
Chibulunje
amewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula; Viwanda na Biashara; Kazi;
Miundombinu na Ushirika na Masoko.
“Katika
nafasi hizi zote za ubunge na unaibu waziri, sijawahi kupata misukosuko,”
alisema.
Mizengo
Pinda (Katavi)
Agosti 17,
2010, Waziri Mkuu Pinda, ambaye tayari ameshatangaza nia ya kugombea urais
kimyakimya, alieleza kwa mara ya kwanza kuwa hatagombea tena ubunge katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kauli ambayo wakati huo haikuhusishwa na mbio za
urais na aliirudia hivi karibuni katika mkutano wa hadhara jimboni kwake
akisema muda wa kuwa mbunge umetosha na sasa anatafuta kitu kingine cha
kufanya.
Awali,
alisema mwaka 2010 ndiyo ungekuwa mara yake ya mwisho kugombea ubunge katika
jimbo hilo, kauli aliyoitoa kwenye Ukumbi wa Katavi Resort, Mpanda wakati wa
sherehe ya kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, John Mzurikwao, aliyekuwa
akihamishiwa Wilaya ya Sumbawanga.
Deogratias
Ntukamazina (Ngara)
Mbunge huyo
aliwaeleza wapigakura nyumbani kwake Ngara kuwa anahitaji kupumzika baada ya
kukamilisha kazi yake.
Alisema
wakati akiingia madarakani mwaka 2010, aliwaahidi wananchi wa Ngara kupata
umeme hadi vijijini na kwamba kazi hiyo ameifanya kwa kiwango kikubwa.
Anne Makinda
(Njombe Kusini)
Kwa nyakati
tofauti, Spika Makinda ambaye amekuwa mbunge wa kuteuliwa tangu 1975 kabla ya
kuchaguliwa kushika ubunge wa Njombe Kusini mwaka 1995, amekaririwa na vyombo
vya habari akisema mwaka huu hatagombea tena. Makinda amewahi kushika nafasi za
ukuu wa mkoa, uwaziri na unaibu spika.
Zitto Kabwe
(Kigoma Kaskazini)
Mbunge
ambaye ameachia ngazi kwa staili ya pekee ni Zitto, ambaye awali, alionekana
kuwa na nia ya kugombea urais lakini nia yake hiyo ilikwama kutokana na Katiba
ya sasa na Katiba Inayopendekezwa kutaja umri wa mgombea urais kuwa ni kuanzia
miaka 40. Mwaka huu Zitto anatimiza 39.
Lakini,
mbunge huyo kijana ameamua kutogombea Kigoma Kaskazini ambako ameongoza kwa
vipindi viwili, lakini atagombea jimbo la Kigoma Mjini ambalo kwa sasa
linaongozwa na Peter Serukamba (CCM).
Hamad Rashid
Mohammed (Wawi)
Kwa upande
wake, Hamad ambaye kwa sasa ana mgogoro na chama chake cha CUF ambao
umewafikisha mahakamani, amesema mara kadhaa kuwa hatarudi jimboni kwake Wawi,
Pemba. Sasa anawania urais kupitia ADC.
Habari:-Gazeti la Mwananchi Jan 14,2015.
|
No comments:
Post a Comment