TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI.
Ndugu zangu wanahabari;-
Napenda
nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi wa taharuki iliyotokea jana tarehe 02
Januari, 2015 katika jiji la Dar es Salaam ikiwahusisha baadhi ya vijana
wanaojikusanya kwenye vikundi na kujiita Panya road na pengine kusababisha hofu
kubwa kwa wananchi.
Chanzo cha
taharuki hiyo, kulitokana na kuuawa kwa kijana mmoja ajulikanae kwa jina la
Mohamed Ayub na wananchi tarehe 01/01/2015 katika maeneo ya Tandale kwa Mtogole
kwa tuhuma za wizi wakati wa mkesha wa sikukuu ya mwaka mpya.
Tarehe 02/01/2015
majira ya saa tisa mchana yalifanyika mazishi ya kijana huyo katika makaburi ya
Kihatu Kagera Mikoroshini na taarifa zilizokuwa zimelifikia Jeshi la Polisi
Kanda ya Dar es Salaam ni kwamba baada ya mazishi hayo vijana wenzake na
marehemu walijipanga kufanya fujo ili kulipiza kisasi cha mwenzao kuuawa.
Aidha, kabla vurugu hizo hazijafanyika na kwa vile Polisi walishaona dalili ya
vurugu hizo, tayari walifanikiwa kuzidhibiti.
Baada ya
vurugu hizo kudhibitiwa na Polisi, vijana hao walitawanyika kwa kukimbia katika
maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi
kwamba huenda kila walipokimbilia wanampango wa kuwafanyia fujo raia wema,
jambo ambalo wasingeweza kulifanya kwa vile Polisi walikuwa wameimarisha ulinzi
katika maeneo yote ya jiji.
Kufuatia
hali hiyo na Jeshi la Polisi nchini likiwa linaendelea na msako mkali wa
kuwabaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na uhalifu huo, tunawaomba wananchi
watulie, wasiwe na hofu na waendelee na majukumu yao kama kawaida.
Mpaka sasa
tunawashikilia watuhumiwa 36 kwa mahojiano na uchunguzi utakapokamilika
tutawafikisha mahakamani mara moja.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa vijana hao wananojihusisha na vikundi
hivyo kuacha tabia hiyo mara moja. Tumejipanga vizuri katika mikoa yote
kuhakikisha kwamba nchi inaongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, hatutamwonea
muhali mtu yeyote ama kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na
kutia hofu wananchi.
Wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa kupitia namba ya simu 0754 78 55 57, namba za makamanda au
katika kituo chochote cha Polisi.
Imetolewa na:-
Advera John Bulimba - SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
|
No comments:
Post a Comment