|
Mtoto mwenye
umri wa miezi mitatu, mkazi wa Buza, Dar es Salaam amebainika kuwa mwathirika
wa dawa za kulevya.
Damu na
mkojo vya mtoto huyo (jina tunalihifadhi) vilichukuliwa na kupimwa katika
maabara ya Hospitali ya Mwananyamala na baada ya saa mbili, majibu yalitoka na
kuthibitisha kwamba alikuwa na chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroini.
Taarifa za
kitabibu zinaonyesha kuwa kuwapo kwa heroini mwilini mwa mtu, huweza kuonekana
katika mkojo ndani ya siku mbili hadi nne iwapo dawa hizo zilitumiwa na mhusika
kwa kati ya saa mbili hadi tano.
Hatua ya
kumfanyia vipimo mtoto huyo wa kiume, inatokana na jitihada za gazeti hili
kutaka kufahamu jinsi utumiaji wa dawa za kulevya kwa wanawake wajawazito na
wale wanaonyonyesha unavyoweza kumwathiri mtoto akiwa tumboni au anayenyonya
maziwa ya mama mwathirika.
Mtaalamu wa
tiba katika Hospitali ya Mwananyamala, Dk Elifasi Mritu anasema: “Ni kweli
ukitumia dawa za kulevya wakati unanyonyesha au wakati wa mimba, mtoto naye
huathirika.”
Kauli ya Dk
Mritu ambaye ni daktari katika kitengo cha tiba ya methadone hospitalini hapo,
inaungwa mkono na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), Dk Frank Mushi ambaye anasema mama anayetumia dawa za
kulevya akiwa mjamzito humwathiri pia mtoto.
Mama wa
mtoto azungumza
Mama wa
mtoto, Zena maarufu Zerish, mkazi wa Yombo Buza alikiri kwamba alipata ujauzito
wakati akitumia dawa za kulevya na kwamba hadi sasa anavuta dawa hizo huku
akiendelea kumnyonyesha mtoto huyo.
Anasema
baada ya kujifungua hakukaa ndani kwa siku 40 kama wafanyavyo wanawake wengi wa
Kitanzania, kwa sababu mwili wake ulikuwa unahitaji ‘unga’ vinginevyo hali yake
huwa mbaya.
Anasema
baada ya kujifungua alianza kuzunguka huku na kule akiwa na mtoto mgongoni,
huku akiwa amebeba mfuko wake wa plastiki wenye mahitaji muhimu ya mtoto kama
nepi na nguo.
Anasema
anapovuta au kujichoma dawa, mtoto wake pia hupata ‘stimu’ kwa sababu hupata
dawa hizo za kulevya kupitia maziwa anayonyonya na hivyo wote wawili kulala
fofofo sehemu yoyote ile.
Hata hivyo,
kwa Zerish na mwanaye, anapofikia hali ya kuwa ‘alosto’ (wakati dawa za kulevya
zinapoisha mwilini na hivyo kuhitaji tena), huwa ni adhabu kali mno.
Anasema dawa
zinapoisha mwilini na mtoto naye huwa katika hali hiyo na hivyo hulia sana.
Hali hiyo humfanya akimbie kutafuta dawa ili ‘kujinusuru’ yeye na mwanaye.
Uwezekano
wa tiba
Dk Mushi
anasema watoto wanaoathirika kwa dawa kupitia mama zao, hulia sana na
kujinyonganyonga hali inayoashiria wanapata maumivu ya tumbo.
“Lakini
tumaini lipo kwa watoto hao, kwani hupewa dawa aina ya morphin ambayo hukata
ulevi huo taratibu. Baada ya muda hupona kabisa,” anasema.
Hata hivyo,
alisema iwapo mtoto ataendelea kunyonya maziwa bila kupata tiba huku mama naye
akitumia dawa hizo, huweza kuwa mtumiaji wa dawa hadi anapokuwa mkubwa.
Katika
hospitali za Muhimbili na Mwananyamala, wanawake wenye watoto walio na uraibu
wa dawa za kulevya hutakiwa kuhudhuria kliniki kila siku bila kukosa.
Mwanamke
anayetumia dawa za kulevya hutibiwa kwa dawa aina ya methadone na mtoto hupewa
morphin.
Chanzo:-Gazeti la Mwananchi.
|
No comments:
Post a Comment