Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema muundo
wa Muungano uliopendekezwa kwenye Katiba pendekezwa ‘una utata mkubwa’ hasa
baada ya kupunguza mambo ya Muungano na kwamba kunaipa nguvu Serikali ya
Jamhuri ya Muungano kuwa Serikali ya Tanganyika.
Alisema muundo
wa serikali mbili hauwezi kuendelea kwa sababu haiwezekani kuwa na serikali ya
Jamhuri ya Muungano, isiyovuka bahari.
Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam October
22,2014, Jaji Warioba alisema pia kwamba haoni kama Wazanzibari watakubali
kuipitisha Katiba pendekezwa kwa kuwa Ibara ya 294 inataka Katiba ya Zanzibar
ifanyiwe marekebisho ili iwiane na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema wananchi wa pande zote walieleza namna kero za Muungano kwa kina na
ndiyo maana Tume yake ikapendekeza muundo wa Serikali tatu kama mwarobaini wa
matatizo hayo.
MALALAMIKO YA ZANZIBAR.
Alisema malalamiko makubwa kutoka Zanzibar ilikuwa kwamba;-
La kwanza, wanaona
Tanganyika imevaa koti la Muungano kwamba kwa hali ilivyo, wanaofaidi Muungano
ni Tanganyika.
Pili, walisema kuongezeka kwa mambo ya Muungano kunapunguza mamlaka ya Zanzibar
kusimamia mambo yake.
Tatu, kufuatana na makubaliano ya hati ya Muungano, rais
wa Zanzibar awe makamu wa rais.
“Katika haya, Bunge Maalum limekubali kupunguza mambo ya Muungano; kwa hiyo
katika orodha mpya mambo yote ya uchumi yameondolewa kwenye orodha ikiwa ni
pamoja na biashara, mikopo ya nje, takwimu, utafiti na kwamba hata sensa
haitakuwa mambo ya Muungano.”
Jaji Warioba alisema sensa ndiyo msingi wa mipango ya maendeleo, lakini sasa
baada ya kuondolewa kwenye Muungano, kila upande utashughulikia sensa yake na
pia Zanzibar wameridhika na sasa watasimamia uchumi wake kikamilifu na pili
imekubalika rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
“Mimi naamini, mabadiliko haya hayataisaidia Zanzibar kwa sababu kwa kuondoa
mambo yote ya uchumi, Zanzibar ikasimamia mambo yake maana yake ni kwamba
serikali ya Muungano itakuwa inasimamia mambo ya Tanganyika tu ndiyo hapo
Tanganyika itakuwa imevaa koti la muungano,” alisema Jaji Warioba.
Aliongeza: “Haiwezekani ukasema una serikali ya muungano ambayo haivuki bahari
na ndivyo ilivyo sasa na ndiyo yalikuwa malalamiko kwa sababu Serikali ya
Muungano haivuki bahari.”
Alisema wananchi wa Bara wanajua kwamba mambo yote yanayowahusu
yanashughulikiwa na serikali ya Muungano ikiwamo elimu, afya, maji, barabara na
mambo mengine wakati sivyo ilivyo kwa wananchi wa Zanzibar.
“Kwa wananchi wa Zanzibar hakuna hata moja kati ya haya linashughulikiwa na
Serikali ya Muungano.”
Alitoa mfano kwamba ndio maana hata kama Waziri wa Ujenzi au wa Uchukuzi wa
Bara, hata kama angekuwa ni mtendaji mzuri kiasi gani, hawezi kwenda Zanzibar.
“Hujaona Waziri anavuka kwenda Zanzibar kufanya kazi. Utawaona kwa mfano
Magufuli anafanya kazi sana huwezi kumsikia amevuka kwenda Zanzibar.
Mwakyembe
atatembelea bandari ya Dar es Salaam, lakini hujamsikia amevuka kwenda
Zanzibar; kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka Zanzibar.”
Alisema: “Kwa hiyo huwezi kusema una serikali ya Muungano ambayo haina madaraka
upande wa Zanzibar.”Pili, hii serikali ndiyo inayo hodhi sovereignty, sovereignty
ya nchi iko chini ya serikali ya Muungano, ndiyo inayojulikana duniani kwamba
serikali ya Tanzania ni Serikali ya Muungano.
Alisema rasilimali za Bara ndizo rasilimali za Serikali ya Muungano, hivyo hata
inapotaka kukopa hutumia rasilimali hizo na kwamba itakopa kwa ajili ya Bara na
kutafuta rasilimali kwa ajili ya Bara pia bila kuhitaji kibali chochote.
Alisema kwa upande wa Zanzibar ni kinyume chake, kwa kuwa haina haki ya kukopa
bila kupitia Serikali ya Muungano.
Alisema hiyo ni kwa sababu rasilimali za Zanzibar haziko chini ya serikali ya
Muungano hivyo ili ikubali kukopa kwa ajili ya Zanzibar lazima itake dhamana na
kwamba hata katika Katiba pendekezwa, Zanzibar itaendelea kuwa na tatizo hilo.
Kuhusu Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, alisema
wakati waasisi wa Taifa walipokuwa wanaunganisha vyama vya Afro-Shiraz na Tanu,
waliunganisha mambo mengi yaliyolenga kuunda Serikali ya Muungano.
“Kabla ya hapo kulikuwa na rais na makamu wawili; Makamu mmoja ambaye alikuwa
makamu wa kwanza alikuwa Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu. Tukasema ukifanya
hivi hutaunganisha nchi, ni lazima anayemsaidia rais amsaidie kwa nchi nzima.”
Alisema baada ya kubaini ugumu huo, marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977, yaliondoa nafasi za makamu wawili wa rais na kuweka
sharti kwamba rais akitoka upande mmoja wa muungano, makamu wake atoke upande
wa pili.
Alitoa mfano kwamba wakati ule, rais wa Jamhuri alikuwa Hayati Mwalimu Julius
Nyerere (Bara) na Makamu wake akawa Rais wa Zanzibar na wakafuta Waziri Mkuu
asiwe makamu wa rais.
Alisema mwaka 1984, upande wa Bara ulidhani Waziri Mkuu atakuwa ni nafasi ya
Bara peke yao na wakaamua kuirudisha kwamba naye awe Makamu wa Rais.
Alisema alipoteuliwa kushika wadhifa huo nafasi hiyo mwaka 1985 ilikuwa
imerudishwa, lakini mwaka 1992, walibaini kwamba maamuzi hayo yalirudisha nyuma
azma ya Muungano, hivyo wakaamua kumwondoa Waziri Mkuu kwenye wadhifa wa Makamu
wa Rais kwa nia ya kutoa fursa kwa viongozi hao watoke upande wowote wa
Muungano.
Alisema kurudisha makamu wa rais watatu kunafanya wakati wote Rais wa Jamhuri
ya Muungano atoke Bara.Ibara ya 99 ya Katiba pendekezwa inaeleza kuwa kutakuwa
na Makamu wa Rais watatu ambao watakuwa:
(a) Makamu wa Kwanza wa Rais;
(b) Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Makamu wa Pili wa Rais; na (c) Waziri Mkuu
ambaye atakuwa Makamu wa Tatu wa Rais.
“Kwa sababu haiwezekani kwamba ukawa na marais wawili; Rais wa Zanzibar na Rais
wa Jamhuri wote wanatoka upande mmoja na hasa kwa kuwa huyu Rais wa Muungano
anashughulikia zaidi mambo ya Bara; kwa utaratibu huu ni kwamba utafanya
haitawezekana tena kupata rais kutoka Zanzibar.”
Alisema Zanzibar pia haitaweza kutoa Waziri Mkuu kwa kuwa makamu watatu
wanaliopendekezwa mmojawapo ni mgombea mwenza ambaye lazima atoke Zanzibar kwa
kuwa rais atatoka Bara, mwingine ni Rais wa Zanzibar na mwingine ni Waziri Mkuu
ambaye haitawezekana naye akatoka Zanzibar.
Alisema kwa utaratibu huo, kama taifa tunarudi nyuma kwa kuwa ile dhana ya
kiongozi atoke upande wowote ule kiuhalisia haitawezekana.
“Kwa hiyo kwa kufanya hivi mimi sioni kama Zanzibar wamepata faida yoyote.”
Alisema katika mambo ya Muungano, suala la kodi ya mapato yanayolipwa na watu
binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa amabzo zimekuwa za
Muungano.
Alisema mgogoro wa kwanza kuhusu Muungano ulitokana na masuala ya mapato na
sababu zake zinaeleweka.
“Zanzibar imepewa mamlaka kuendesha uchumi wake, kwa hiyo ni lazima iwe na
mapato. Vyanzo vikubwa vya mapato ni hivi vilivyotajwa; kodi ya mapato, ushuru
wa bidhaa na ushuru wa forodha. Huwezi kuipa madaraka kisha ukainyang’anya
uwezo wa kifedha hiyo ndiyo inayoleta mgogoro.”
Alisema mwaka 1977 iliamuliwa kwamba kodi hizo zinazopatikana Zanzibar
zisiletwe kwenye serikali ya Muungano na kwamba ndivyo ilivyo hadi sasa.
Alisema Zanzibar haitaweza kujiendesha bila kodi kwa kuwa nusu ya mapato yao
yanatokana na kodi hizo na kwamba mapendekezo yaliyopo kwenye Katiba
hayatatekelezeka.
“Na Zanzibar watalikataa. Mimi nadhani hapa wamekosea (BMK). Tume ilipendekeza
ushuru wa bidhaa ndiyo iwe kodi ya Muungano kwa sababu kwa upande wa Bara ndio
chanzo cha pili kwa ukubwa.”
Alisema mwaka 2012/13; ushuru wa bidhaa uliingizia Bara mapato ya Sh. trilioni
1.3 lakini Zanzibar ilikusanya Sh. bilioni 11 na kwamba fedha hiyo ni kidogo
ambayo Zanzibar ingeweza kuchangia kwa kuzingatia kuwa masuala mengi ya
Muungano yapo zaidi Bara kama jeshi.
“Matatizo ya Zanzibar hasa kuhusu mikopo na misaada yatakuwa makubwa zaidi, Uhuru wa mahusiano wa mahusiano ya kikanda na kimataifa nao utakuwa mdogo;
Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa
Afrika, Sadc, OIC, UN na mashirika yake, kwani uanachama unahitaji
sovereignty,” alisema.
MALALAMIKO YA BARA.
Alisema wakati wa kukusanya maoni, wananchi wengi wa Bara walilalamikia
mabadiliko makubwa ya Katiba ya Zanzibar kwamba imeingilia Katiba ya Muungano
kwa kuwa sheria zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri haziwezi kutumika Zanzibar
bila kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi.
Pili, alisema wananchi wa Bara hawana haki ya kumiliki ardhi Zanzibar na pia
hawana haki ya kuchaguliwa au kupiga kura; wakati ni kinyume chake kwa wananchi
wanaotoka Zanzibar ambao wanaishi Bara.
Kadhalika, Mahakama ya Rufani haina madaraka Zanzibar, mashauri yanayotokana na
haki za binadamu na Mahakama za Kadhi. Pia Katiba ya Zanzibar inavitambua
visiwa hivyo kama nchi kamili.
Hata hivyo, alisema inawezekana wajumbe wa BMK walikubaliana ndani ya Bunge
mambo kadhaa ambayo hawakutaka kuyaweka hadharani hasa suala la kuirekebisha Katiba
ya Zanzibar.
Ibara ya 294 ya Katiba pendekezwa inaeleza kuhusu mambo ya mpito ikiwamo:
(a) kurekebisha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 ili kuwiana na masharti ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2014;
(b) kutunga na kurekebisha sheria mbalimbali za Jamhuri ya Muungano, sheria
ambazo si za Muungano zinazohusu Tanzania Bara na sheria za Zanzibar ili
kuwiana na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2014.
“Kwa kuwa ardhi imeingizwa kwenye Katiba basi Zanzibar italazimika kubadili
sheria yake ili raia wote wawe na haki sawa. Pia sheria za uchaguzi nazo
zitabadilika ili raia wote wawe na haki za kiraia. Kama mabadiliko hayo
yamekubalika Zanzibar basi wananchi wa Tanzania Bara hawatakuwa na malalamiko
yoyote ya msingi,” alisema.
Jaji Warioba aliongeza: “Tatizo ninaloliona mimi ni ugumu wa kufanya mabadiliko
haya. Katika taarifa ya Tume tulisema kama kuna jambo ambalo tuliona
Wanzanibari wameungana ni Zanzibar kuwa nchi. Ili mabadiliko yafanyike kwenye
Katiba ya Zanzibar ni lazima yapatikane maridhiano, pasipo na maridhiano Baraza
la Wawakilishi halitapata kura za kutosha kupitisha marekebisho.”
“Hali itakuwa ngumu zaidi kwenye kura ya maoni kama Katiba ya Zanzibar
inavyotaka. Kazi kubwa ipo katikakusuluhisha makundi ya Zanzibar kwa suala
hili.
Uhasama unaoonyeshwa hadi sasa unatia wasiwasi, kama marekebisho
hayatafanywa, Katiba inayopendekezwa itabaki ni Katiba ya Tanganyika; Zanzibar
itabaki ni nchi yenye mamlaka na madaraka makubwa na Tanganyika ndiyo itakuwa Muungano.”
Chanzo:-
NIPASHE
|
No comments:
Post a Comment