UGONJWA WA EBOLA :-Sasa Ni Tishio la AMANI na USALAMA wa Kimataifa. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, September 20, 2014

UGONJWA WA EBOLA :-Sasa Ni Tishio la AMANI na USALAMA wa Kimataifa.


Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mwezi wa Septemba, Muwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Balozi Samantha Power akizungumza wakati wa Mkutano wa Dharura wa Baraza Kuu la Usalama, uliofanyika Alhamisi September 18,2014, kwa lengo la kukusanya nguvu za Jumuiya ya Kimataifa katika kuukabili mlipuko wa Ebola ambao sasa unaangaliwa katika jicho la kuwa tishio la amani na usalama wa Kimataifa.


Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama wakipiga kura ya kuunga mkono azimio namba 2177( 2014) kuhusu ugonjwa wa Ebola, azimio hilo linaelezwa kuwa huenda ndio likawa azimio la aina yake kupata uungwaji mkono mkubwa. Zaidi ya Mataifa 131 yameunga mkono azimio hilo ambalo linaweka mikakati ikiwamo ya vitendo na kisiasa ya kushughulikia mlipuko wa Ebola.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida katika historia ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limekasimiwa majukumu na dhamana ya masuala yote yanayohusiana na Amani na Usalama wa Kimataifa, jana alhamisi limelazimika kukutana kwa dharura kujadiliana na kuweka mikakati ya kuukabili mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na ambalo kwa mwezi huu wa Septemba lipo chini ya Urais wa Marekani, lilikutana chini ya kichwa cha habari kilichosema “ Amani na Usalama katika Afrika: Ebola”.

Kwa tafsiri ya haraka ni kuwa, Ugonjwa huo wa Ebola ambao umeshapoteza idadi kubwa ya maisha ya watu katika nchi kadhaa za Afrika ya Magharibi kwamba, sasa siyo tu unachukuliwa kama janga la kiafya, kibinadamu na kiuchumi bali umekuwa ni tishio kwa Amani na Usalama wa Jumuiya ya Kimataita.

Ni kwa sababu hiyo basi, Jumuiya ya Kimataifa kwa maana ya Umoja wa Mataifa wenyewe wanachama 193 imeamua kuuangalia kwa jicho pana zaidi mlipuko huo wa Ebola na kuutafutia ufumbuzi.

Katika mkutano huo wa dharura na ambao kama ilivyoelezwa hapo juu uliandaliwa na Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu (Marekani), licha ya kusikiliza hotuba au maelezo kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo akiwamo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataita, Mkurugenzi Mkuu wa WHO na wawakilishi kutoka mataifa ambayo yameathiriwa na mlipoko huo, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja Azimio namba 2177.
 
Azimio hilo ambalo limeungwa mkono na zaidi ya mataifa 131 ikiwamo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaelezwa kama Azimio ambalo limepata uungwaji mkono mkubwa zaidi pengine kuliko azimio lolote ambalo limewashi kuwasilishwa katika Baraza hilo.

Nchi ambazo hadi sasa zimeathirika kwa kiasi kikubwa na mlipuko huo wa Ebola ni Liberia, Sierra Leone na Guinea. Zikiwamo Nigeria na nchi nyingine Cote d’ Ivoire na Senegal ambazo nazo zimeeleza kukumbwa na mlipuko wa Ebola

Inaelezwa kuwa asilimia zaidi ya 50 ya wahanga wa mlipuko huo ni wanawake, ambao kimsingi kutokana wa majukumu yao ndio walezi na watoa huduma ya kwanza kwa wanafamilia wanaokumbwa na ugonjwa huo.
 
Katika mkutano huo wa dharura kila mjumbe aliyepata nafasi ukiacha wale waliotoa ahadi za kutoa misaada ya hali na mali ikiwamo ya kibinadamu na fedha kwa nchi ambazo zimeathirika na mlipuko huu, wametoa wito kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa na nchi zote bila ya kujali ukubwa au udogo wake kuchukua hatua madhubuti za muda mfupi na muda mrefu kuukabili mlipuko wa Ebola ambao hadi sasa hauna tiba.

Vile vile, wazungumzaji kadhaa wamezipongeza nchi ambazo zimekabiliwa na mlipuko huo kwa hatua mbalimbali ambazo hadi sasa zimechukua katika kuukabili ugonjwa.

Aidha baadhi ya wazungumzaji wamesisitia haja na umuhimu wa kutozitenga au kuzinyanyapaa nchi ambazo zimeathirika kwa kile walichosema kinachotakiwa si kuzitenga bali kuzisaidia ili kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huu hatari.

Mwakilishi wa Tanzania akichangia majadiliano hayo, alirejea ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa hivi karibuni katika mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyia Malabo, Equitoria Guinea kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana kwa hali na mali na AU na washirika wengine katika kuukabili mlipuko wa Ebola.

Umoja wa Mataifa umekwenda mbali zaidi kwa kuanzisha Kituo cha Kwanza cha aina yake kuratibu dharura ya Mlipuko wa Ebola na kuipandisha hadhi Misheni ya Kulinda Amani nchini Liberia ili pamoja na mambo mengine iweze kuratibu na kusimamia misaada inayohusiana na Mlipuko wa Ebola.

Katika kile kinachoonekana kwa Ebola ni tishio kwa amni na usalama , nchi kama vile Marekani, Uingereza na Cuba na nyinginezo zenyewe zimeamua kuyahusisha majeshi yake katika utoaji wa misaada, mafunzo na ujenzi wa vituo vya afya kama hatua ya kukabiliana na Ebola.

 UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
 
 Like ukurasa wetu wa facebook  ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu BONYEZA HAPA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad