SOMA RATIBA HII YA UCHAGUZI TANZANIA:-Ni ule wa Serikali za mitaa sasa Kipenga chake ni Desemba 14,2014. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Sunday, September 14, 2014

SOMA RATIBA HII YA UCHAGUZI TANZANIA:-Ni ule wa Serikali za mitaa sasa Kipenga chake ni Desemba 14,2014.

Kipenga cha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, kinatarajiwa kupulizwa Novemba 30 mwaka huu na uchaguzi kufanyika Desemba 14,2014,chini ya sheria zilizopo.

 Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyotumwa katika vyombo vya habari jana, ilifafanua kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia masharti ya sheria za serikali za mitaa na kanuni za uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, sheria hizo zimetungwa na ofisi yake, baada ya kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, asasi za kiraia na wadau mbalimbali.

Kwa uamuzi huo, wagombea wa nafasi zinazowaniwa za mwenyekiti wa mtaa, kijiji na kitongoji na nafasi za ujumbe wa serikali za vijiji na kamati za mitaa, wametakiwa wawe wanachama na wadhaminiwe na chama cha siasa chenye usajili wa kudumu.

RATIBA.

Katika ratiba iliyotolewa sambamba na taarifa hiyo, wasimamizi wa uchaguzi wameelekezwa kutoa tangazo la majina na mipaka ya mitaa, vijiji na vitongoji, siku 50 kabla ya siku ya uchaguzi kwa kuzingatia Kanuni ya 6 ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa ya mwaka 2014.

Baada ya hatua hiyo, wasimamizi hao wa uchaguzi watateua majina ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi mara baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika eneo lake, msimamizi wa uchaguzi atatoa maelekezo ya uchaguzi siku zisizopungua 28 kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni ya 7(1), 8(1) ya kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2014.

Aidha msimamizi wa uchaguzi atateua ofisa wa umma mwenye sifa na uadilifu, atakayeandikisha na kuandaa orodha ya wapiga kura siku 21 kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni 8 na 9 ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.

Uteuzi wagombea Baada ya hatua zote hizo za awali kufanyika, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atabandika orodha ya wapiga kura mahali pa matangazo ya uchaguzi na kutunza kumbukumbu zake, baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi na kufanya uteuzi wa wagombea siku zisizopungua 20 kabla ya siku ya uchaguzi.

Ratiba iliyotolewa pia inaonesha kwamba Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, katika muda wa siku mbili tangu siku ya uteuzi kufanyika, atasikiliza na kutoa uamuzi katika muda usiozidi siku mbili kwa mapingamizi mbalimbali, kuanzia siku ya kupokea pingamizi husika.

Aidha kutakuwepo na Kamati ya Rufaa, ambayo wajumbe wake watateuliwa na Katibu Tawala wa Mkoa na katika uteuzi wake, Katibu Tawala atazingatia hali halisi ya watumishi wa umma walioko katika wilaya husika.

Kamati hiyo ya Rufaa, itateuliwa siku saba kabla ya siku za uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa Kanuni ya 16(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.

Waziri Mkuu wa Tanzania ,Bw. Mizengo Pinda.

KAMPENI.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kampeni za uchaguzi zitafanyika wiki mbili za mwisho kabla ya siku ya uchaguzi na zitafanyika kwa muda wa siku 14 na zitamalizika siku moja kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2014.

Ili kufanikisha uchaguzi huo, wananchi wametakiwa kujiandikisha katika Rejista ya Wapigakura, itakayoandaliwa siku ishirini na moja kabla ya siku ya uchaguzi na uchaguzi utafanywa kwa kutumia karatasi maalumu za kupigia kura.

Aidha kura zitapigwa na kutumbukizwa kwenye masanduku ya kupigia kura na kama kawaida, uchaguzi utafanyika katika ngazi ya kitongoji na mitaa katika sehemu ya faragha na hakutakuwa na mikutano ya uchaguzi katika ngazi za vijiji.

Uchaguzi uliopita Katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa, CCM kilipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa, hatua iliyochukuliwa na wachambuzi wengi kuwa ni dalili kuwa chama hicho kilikuwa kinakwenda kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Uchaguzi wa mwaka huu, mbali na kuendelea kutumika kutoa ishara za uchaguzi mkuu ujao, pia utakuwa na umuhimu wa ziada katika kupima uimara wa makubaliano ya vyama vikubwa vya siasa, vilivyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakati wa mchakato wa Katiba mpya na kukubalika kwao kwa wananchi.

Tayari viongozi wa vyama hivyo, Chadema, CUF na NCCRMageuzi, walishatoa kauli ya kuhoji kwa nini uchaguzi huo unachelewa, wakihofia kuwepo wanachoita mchezo mchafu wa kuwashitukiza.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alinukuliwa akidai Serikali imeshindwa kutangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo, lakini pamoja na hitilafu hiyo, chama hicho kimeshatoa taarifa kwa wanachama wake kujiandaa kugombea.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, alinukuliwa akidai kwa kuwa uchaguzi huo hufanyika Septemba kila mara na kwa kuwa mwaka huu kuna Bunge Maalumu la Katiba linalomalizika Oktoba, Serikali ilitakiwa kulitambua hilo na kutoa ratiba mapema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema, John Mnyika alisema kutokana na mchakato wa kupata Katiba mpya kusuasua, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi vinatakiwa kushirikiana ili kushinda viti vingi.

UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
 
 Like ukurasa wetu wa facebook  ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu BONYEZA HAPA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad