Baada ya
kimya kirefu, hatimaye aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi wa kwanza wa TANU na
baadaye kufukuzwa katika chama hicho mwaka 1968, Dk. Fortunatus Masha, ameibuka
na kusema matatizo yaliyokuwapo kati yake na Mwalimu Julius Nyerere yalichangia
asipate ajira ndani na nje ya Afrika Mashariki.
Dk. Masha
ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chama cha UDP, alisema hayo katika mahojiano
maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika jijini hapa ambapo pamoja na mambo mengine
aligusia uhusiano wake na Mwalimu Nyerere ulivyokuwa kabla na baada ya
kufukuzwa TANU.
Agosti 1968,
Mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU uliofanyika mjini Tanga uliridhia kwa kauli
moja kufukuzwa uanachama kwa Dk. Masha na wanachama wengine maarufu wa chama
hicho zaidi ya wanane kwa kile kilichodaiwa kulipinga Azimio la Arusha.
Pamoja na
Dk. Masha, wengine waliofukuzwa TANU wakati huo ni Oscar Kambona ambaye baadaye
alikimbilia uhamishoni nchini Uingereza, Joseph Kaselabantu, Eli Anangisye,
Wilfram Mwakitwange na wengine waliotajwa kwa majina mojamoja ambao ni Choga,
Kaneno, Bakampenja na Kiguga.
Wakati
akifukuzwa TANU, Dk. Masha alikuwa pia ni mwajiriwa wa Wizara ya Habari.
Katika
mazungumzo hayo huku akionekana kuguswa sana, Dk. Masha alisema baada ya
kufukuzwa TANU, Serikali iliagiza asipewe ajira ndani na nje ya Afrika
Mashariki na kusisitiza hiyo ni sababu iliyomfanya kuondoka nchini.
Alisema
baada ya kukosa ajira kila anapokwenda kuomba kazi ikiwamo katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki, alilazimika kurejea kijijini kwake Kamanga na kuanza kazi ya
kufuga ng’ombe na kilimo.
“Baada ya
kufukuzwa chama na kupoteza ubunge wangu wa Geita Mashariki, nilianza kutafuta
kazi, niliomba sehemu nyingine, niliomba kazi kama Afisa Mahusiano katika
Shirikisho la Viwanda lililojulikana kama National Development Cooperation
(NDC), lakini nilikuta maagizo ya Serikali kwamba nisipewe ajira hapa nchini.
“Niliambiwa
kila nilikoomba kazi kuwa maagizo toka serikalini nisipewe kazi. Nikaamua
kutoka nje ya nchi na nikaenda Jumuiya ya Afrika Mashariki kuomba ajira, nako
pia nikakuta maagizo yale yale kwamba Serikali imeleta maagizo ya kwamba
wasinipe ajira.
Dk. Masha
alisema kuwa wakati akiwa Nairobi akielekea masomoni nchini Marekani,
alimwandikia Mwalimu Nyerere barua akimwambia anakoelekea, alikopata pesa za
kumsemesha.
“Sikukimbia
na ndiyo maana nilirudi kuja kuichukua familia yangu,” alisisitiza.
UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
Like ukurasa wetu wa facebook ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu BONYEZA HAPA |
Friday, September 26, 2014
NAJUA WAJUA ILA HII HUJUI:-Dk. Masha: Nilikosa ajira sababu ya Nyerere.
Tags
# SIASA
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
SIASA
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment