KUSHAMBULIWA KITUO CHA POLISI WILAYANI BUKOMBE:-Ni Ugaidi asilimia Mia Moja. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, September 09, 2014

KUSHAMBULIWA KITUO CHA POLISI WILAYANI BUKOMBE:-Ni Ugaidi asilimia Mia Moja.

Damu ya maaskari iliyomwagika kwenye shambulia hilo la kigaidi. 

 Tukio la kutisha la kushambuliwa kwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ambapo askari wawili walipoteza maisha na silaha kadhaa kuporwa, limeelezwa kuwa kwa kiwango cha asilimia mia moja, jambo hilo ni ugaidi wa dhahiri.

Jumamosi iliyopita Septemba 06,2014, majira ya saa sita  usiku, watu wasiojulikana, walikivamia kituo hicho kwa mabomu na silaha zingine nzito zinazosadikika kuwa ni za kivita, wakafanya mauaji na kujeruhi watu wengine kadhaa kabla ya kupora bunduki na silaha zilizohifadhiwa kituoni hapo.
Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, kilichoshambuliwa kwa mabomu. 

“Huu siyo ujambazi wa kawaida uliozoeleka, ni kweli kuna wakati matukio yanatokea kuwa ya kutisha sana, lakini aina hii ya mashambulio siyo kawaida, tena kituo cha polisi? Hawa watu ni dhahiri walihitaji kupata silaha tu, sasa sijui zinakwenda kutumika wapi na tuna shaka kama hawa si Watanzania,” alisema Zebareta Shayo, mkazi wa Sinza, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Ernest Mangu (mwenye suti nyeupe) akiwa eneo la Tukio.

Bw.Waziri Salum, mwanasheria na wakili wa kujitegemea  alisema tukio hilo ni vizuri kama lingeifanya serikali kutazama upya mipaka yetu kwani kuna kila dalili kuna baadhi ya wageni wanaingia kirahisi na kufanya unyama huo bila kujulikana.
Muonekano wa silaha zilizoibwa na Majambazi katika kituo cha Polisi Bukombe Septemba 06,2014 zikiwa zimekamatwa.

Askari waliopoteza maisha katika shambulio hilo wametajwa kuwa ni Uria Mwandiga mwenye namba WP 7106 na Dustan Kimati mwenye namba G 615 PC. 

Majeruhi ni David Ngupama Mwalugelwa (44) namba E 5831 APL na Mohamed Hassan Kilomo (25) namba H 627 PC.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) nchini Tanzania,Bw. Isaya Mngulu.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Ernest Mangu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) Isaya Mngulu kuwasili tangu Septemba 07,2014, mkoani Geita, askari zaidi kutoka Mikoa ya Tabora, Shinganya na Mwanza wanaendelea kuwasili.

Msako mkali unaendeshwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kuweza kuwabaini wahalifu hao huku Kamanda wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo akiwataka wananchi kutoa taarifa mara moja watakapotilia shaka nyendo za mtu yeyote ili kurahisisha zoezi hilo alilodai lazima lifanikiwe.

Juni 10, mwaka huu, tukio kama hilo likihusisha majambazi waliokisiwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo na kujeruhi mgambo mwingine kisha kupora bunduki tano na risasi 60.

Stori na:- Jaed Kimaro, Bukombe/Global Publisher's.

UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
 
 Like ukurasa wetu wa facebook  ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu BONYEZA HAPA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad