Mhe. Cheyo aliendelea kwa kusema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika mwezi Aprili 2015.
“Kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa Sheria iliyotajwa, kura itarudiwa
mwezi Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa
livunjwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2015 na ili Katiba Mpya
itumike katika uchaguzi Mkuu utakaokuja, itabidi uhai wa Bunge na Serikali
uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo hatuliungi mkono”, alisisitiza Mhe. Cheyo.
Mhe. Cheyo amesema kuwa Bunge Maalum la Katiba kwa sasa linafanya kazi kwa
mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na 254 lililotolewa na Mhe.
Rais Kikwete tarehe 1 Agosti, 2014.
“Tangazo hilo litatumika hadi tarehe 4 Oktoba, 2014 ambapo Katiba
inayopendekezwa inategemewa kupatikana, Wajumbe walikubaliana hatua hii iachwe
ifikiwe”, alisema Mhe. Cheyo.
Kuhusiana na Kura ya maoni, Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba baada ya Bunge hilo kumaliza kutunga Katiba, ingefuata
hatua ya kura maoni kuthibitisha Katiba.
“Kwa kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015
kuahirishwa, basi hatua hii iahilishwe, na mchakato wa Katiba uendelee baada ya
Uchaguzi Mkuu wa 2015”, alisema Mhe. Cheyo.
Sambamba na hayo, Mhe. Cheyo ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria ili
matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa, yaanze haraka
iwezekanavyo ili uchaguzi ufanyike mapema hapo mwakani.
Aidha, amegusia kuhusu Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya 1977 akasema kuwa, kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015 utafanyika kwa
kutumia Katiba ya 1977, kuna umuhimu kufanya mabadiliko kidogo (minimum
reforms) katika Katiba pamoja na sheria ya Uchaguzi yatayowezesha nchi kufanya
uchaguzi huru na wa haki.
“Tayari mambo yafuatayo yamekubaliwa, kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia
uchaguzi, Mshindi wa Uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50%
(50%+1)”, alisema Mhe. Cheyo.
Viongozi hao Wakuu wa Vyama wamempongeza Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
kwa ujasiri wake na imani yake katika kuimarisha demokrasia nchini na kuanzisha
mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi.
“Tunampongeza kwa kukubali kukutana na kushauriana nasi kuhusu mambo ya muhimu
kwa mustakabali wa taifa letu kwa lengo la kudumisha amani, upendo na
mshikamano ili nchi yetu iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya kujivunia yenye
amani, mshikamano na itakayokuwa na Uchaguzi Huru na wa haki, lakini pia
tunajipongeza sisi wenyewe Wakuu wa Vyama kwa kuwa tumetoka mbali na misimamo yetu,
lakini utaifa umetufanya tukubaliane katika mambo ya msingi wa Taifa letu”,
alipongeza Mhe. Cheyo
|
No comments:
Post a Comment