KATIBA MPYA TANZANIA:-Soma hii kutoka kwa Askofu akisema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta….Mchochezi. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, September 17, 2014

KATIBA MPYA TANZANIA:-Soma hii kutoka kwa Askofu akisema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta….Mchochezi.


Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.


MWENYEKITI mstaafu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Peter Kitula, amesema kauli za kejeli zinazotolewa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta zimejaa uchochezi.

Sitta amekuwa akishutumiwa na watu mbalimbali kutokana na kauli zake anazozitoa pindi anapoendesha Bunge hilo.

Hivi karibuni, Sitta alisema wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni waigizaji na juzi Septemba 15,2014, alisikika akisema ‘Ukawa imekula kwao’.

Akizungumza na MTANZANIA jana Septemba 16,2014, Askofu Kitula alisema Sitta anapaswa kuzungumza kwa utulivu na amani na aache kutoa kauli za uchochezi.

Kauli za Sitta zimejaa uchochezi, azungumze kwa utulivu na amani. Sisi maaskofu hatuna mwelekeo wa chama chochote, lakini tunataka amani iwepo, aheshimu mawazo ya wajumbe na kutafuta mwafaka kwa amani,” alisema Askofu Kitula.

Pia askofu huyo alishauri Bunge hilo lisitishwe kwanza kwa sababu bila kuwapo ushirikiano wa wajumbe wengine itakuwa ni kazi bure.

Kuhusu kuendelea kushambuliwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, Askofu Kitula alisema si sahihi na kwamba jaji huyo anadhalilishwa.

Tulimwamini tukamkabidhi kazi hiyo, hata kama binadamu hawezi kuwa ‘perfect’ (mkamilifu) kwa taaluma yake, lakini huwezi kumdhalilisha kiasi hicho,” alisema.

Mjada wa sura za Katiba wahitimishwa kwa mipasho.

Katika hatua nyingine, Bunge hilo limehitimisha mjadala wa Rasimu ya Katiba kwa kuwashambulia wajumbe wa Ukawa.

Pamoja na hayo, nusura mjadala huo uingie dosari baada ya Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohamed (CCM), kutaka kupigwa na wajumbe wanaotoka Zanzibar kwa kile kilichoelezwa kuwa aliwakejeli kwa maneno wakati alipokuwa akichangia rasimu hiyo.

Wakati wa mjadala huo juzi, wajumbe wengi walishindwa kujadili sura za rasimu ya Katiba na badala yake walitumia muda mwingi kuwajadili Ukawa kwa kile walichosema hawaridhishwi na mwenendo wa umoja huo.

Wajumbe hao waliwashambulia wenzao hao wakirejea mkutano mkuu wa Chadema uliohutubiwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wakati wa mkutano huo, Mbowe aliwarushia maneno wajumbe wa Bunge hilo wanaoendelea kushiriki vikao vyake mjini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, wajumbe hao walionyesha kutoridhishwa na kauli ya Mbowe aliyewataka wananchi kuandamana nchi nzima ili kupinga mchakato wa Bunge hilo unaotarajiwa kuhitimishwa Oktoba 4,2014.

Katika mchango wake juzi, mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema kinachofanywa na Ukawa hakiwezi kuvumiliwa kwa kuwa wanakiuka sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Dovutwa, Ukawa hawaridhiswi na mwenendo wa Bunge kwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta, alikataa kuwapendelea.

Pamoja na hayo, Dovutwa alizungumzia suala la maandamano yaliyoitishwa na Mbowe na kuwataka viongozi wakuu wa Ukawa, wawe mstari wa mbele wakati wa maandamao hayo aliyoyaita ni haramu.

Mjadala juu ya Ukawa haukuishia kwa Dovutwa bali pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye alijitosa kuwashambulia.

Katika mazungumzo yake, Profesa Mwandosya alisema kama kweli viongozi wa Ukawa ni wazalendo, watakapokuwa wakiandamana wawe mstari wa mbele kama ilivyo kwa Wajapani ambao hujiua kwa kujichoma kisu pindi wanaposhindwa kukubaliana na baadhi ya mambo.

Wengine waliowajadili Ukawa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdallah Bulembo, Mbunge wa Mvomero, Amosi Makala, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene pamoja na Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba.

 UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.

 Like ukurasa wetu wa facebook  ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu BONYEZA HAPA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad