Faustina Selali, akiwa katika maumivu makali
baada ya kushambuliwa na mumewe.
|
DAH! Inasikitisha sana jamani. Faustina Selali, 38, mkazi wa Mgeta, Mvomero mkoani Morogoro, yupo kwenye mateso makali akijiuguza kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa mumewe wa ndoa aliyemtaja kwa jina la Lugasiani John Miasiku, kisa kikiwa ni mumewe huyo kutaka kuoa mke wa pili.
Mwanamke
huyo amelazwa katika wodi nambi 3 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro, ambapo amesimulia kisa chote mbele ya kamera ya Uwazi.
KISA
CHENYEWE.
Akizungumza kwa tabu, Faustina alisema tukio hilo lililobadilisha historia ya maisha yake na kumwachia machungu moyoni mwake, lilitokea Juni 25, mwaka huu majira ya saa nne usiku ndani ya nyumba yao.
“Mimi na mume wangu tumeishi kwenye ndoa kwa muda wa miaka 20 na kufanikiwa kupata watoto watano. Kwa kipindi kirefu nilihisi ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, wakati naendelea kumchunguza, mume wangu akaniambia anataka kuoa mke wa pili,” alisema Faustina kwa uchungu na kuongeza:-
“Nikamhoji
mume wangu, dini yetu hairuhusu jambo hilo na zaidi ya yote anachotafuta kwa
huyo mke wa pili ni kitu gani wakati tayari mimi nimeshamzalia watoto watano na
bado naendelea kuzaa?
“Hakuwa na jibu la maana, akaendelea kushikilia msimamo wake. Mwisho nikaona nisimlazimishe sana, nikamwambia kama hivyo ndivyo basi tugawane mali ili mimi niondoke aje huyo mwenzangu kwani sitakuwa tayari kuishi maisha ya uke wenza.
Kwa kweli hakuwa na jibu la maana.”
Akionyesha sehemu ya jeraha.
|
HARUFU YA
KIFO.
“Ugomvi huo ulitokea Jumanne, kesho yake yaani Jumatano (siku ya tukio) mume wangu alivyorudi shamba nilimtengea ugali kama kawaida.
Alikula vizuri tu...
tukapanda kitandani kulala, kama unavyojua tena wanandoa muda wao wa kuzungumza
kwa utulivu ni usiku, nikaamua kuutumia muda huo kumwuliza mwenzangu.
“Nikamwambia
kama bado ana msimamo wake uleule, anipe sehemu yangu niondoke zangu. Hapo
nikawa nimechokoza moto.
Ilikuwa ghafla tu, aliamka kitandani na kuchukua
nyundo kisha akaileta kichwani na kunipiga nayo, baadaye akanipiga mdomoni na
kuning’oa meno mawili ya mbele kwa kutumia ile nyundo.
“Hakuishia
hapo, akanitoa panga kisha akanicharanga mikono yote, palepale damu zikaruka
kama kachinja ng’ombe.
Nilihisi maumivu makali sana, sikuwahi kupata maumivu
makali kama yale. Kusema ukweli nilichanganyikiwa kabisa na kile kipigo.”
ATUMIA
UJANJA KUJIOKOA.
“Wakati akiendelea kunipiga bila huruma, alikuwa akisema dawa yangu mimi ni kufa ili aweze kumchukua huyo mwanamke wake bila usumbufu. Nilivyosikia hivyo ikabidi nitumie akili; nikajiangusha chini na kujifanya nimekata kauli ili nisiendelee kuumia.
“Alipoona
hivyo kweli akaniacha. Akavaa nguo zake na kukimbia. Mwanangu mdogo Nesto
akanisaidia kunikongoja hadi kwa jirani yetu Mzee Chota ambaye naye aliita
majirani haraka, ilikuwa ni saa sita usiku, wakanikimbiza hadi Zahanati ya
Mlali lakini nikapewa rufaa ya kuletwa hapa kutokana na hali yangu kuwa mbaya.”
Kwa mujibu
wa Bi. Faustina, licha ya mume wake kumfanyia ukatili huo, ndugu wanaofika
hospitalini hapo kumjulia hali, wanasema mumewe bado hajakamatwa na amekuwa
akiendelea kutoa vitisho dhidi yake.
Uwazi
lilifunga safari hadi kijijini Mgeta kwa lengo la kuhojiana na mtuhumiwa huyo
na kufanikiwa kumkuta lakini alipomuona mwandishi wetu, Miasiku alitimua mbio
akidhani alifuatwa na askari.
No comments:
Post a Comment