“Mfano, bei za vyakula ni kubwa jijini Dar es Salaam, ukilinganisha na maeneo ya vijijini, hivyo gharama ya kulipia mlo wa mtu mmoja kwa siku ni ya juu kwa jiji la Dar es Salaam,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa hiyo inayoangalia viashiria
vya umasikini kwa kuchambua mahitaji muhimu ya mwanadamu, iliyo katika tovuti
ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), imefafanua pia kuwa mkoa huo ndio wenye
idadi ndogo ya masikini nchini.
“Kaya za
jijini Dar es Salaam zina kiwango kidogo cha umasikini wa mahitaji ya msingi,
ukilinganisha na kaya zinazoishi katika miji mingine na maeneo ya vijijini.
“Ukijumuisha
watu wote wenye umaskini wa mahitaji ya msingi nchini, inakadiriwa asilimia
mbili (1.5) wanaishi jijini Dar es Salaam, asilimia 14.4 wanaishi maeneo
mengine ya mijini na asilimia 84.1 wanaishi vijijini,” alisema.
Kuhusu
umiliki wa nyumba, taarifa hiyo imeeleza kuwa wakati asilimia 76 ya kaya nchini
zinamiliki nyumba wanazoishi, jijini Dar es Salaam ni asilimia 37 tu ya kaya
zinazomiliki nyumba wanazoishi na kaya zilizobakia, asilimia 63 ni wapangaji.
“Uwiano huu
(wa nyumba za kuishi) ni mkubwa katika maeneo ya vijijini, ambako asilimia 89
ya kaya wanamiliki nyumba wanazoishi, huku umiliki wa nyumba katika maeneo
mengine ya mijini ukiwa asilimia 58,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo
ingawa ni ya awali, lakini iliyochambua vema umasikini kwa kuangalia mahitaji
ya lazima na mahitaji muhimu ya Watanzania, imebaini hadhi za nyumba wanazoishi
Watanzania kwa ujumla imekuwa ikiboreka.
“Asilimia 66
ya kaya mwaka 2011/12 zinaishi katika nyumba zenye paa za kisasa ukilinganisha
na asilimia 55 ya kaya mwaka 2007.
“Vivyo
hivyo, asilimia 73 ya kaya zinaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa kuta imara
mwaka 2011/12 ukilinganisha na asilimia 33 za mwaka 2007,” imeeleza taarifa
hiyo.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, kuta imara zinajumuisha zilizojengwa kwa mawe, matofali ya
saruji, au matofali ya kuchoma na paa za kisasa ni zile zilizojengwa kwa
mabati.
Katika
mawasiliano, taarifa hiyo imeeleza kuwa umiliki wa simu za mkononi
unatofautiana sana kwa maeneo.
“Wakati
kiasi cha asilimia 78 ya kaya za maeneo mengine ya mjini na asilimia 88 ya kaya
za Dar es Salaam, zinamiliki angalau simu moja ya mkononi, ni asilimia 45 tu ya
kaya za maeneo ya vijijini zinazomiliki angalau simu moja ya mkononi,” ilieleza
taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo, imeeleza kuwa mstari wa masikini, unaonesha masikini wa mahitaji ya
msingi nchini na ambaye yupo katika mstari wa umasikini wa mahitaji yamsingi ni
anayepata Sh 36,482 kwa mwezi, wakati maskini wa chakula ni anayepata Sh 26,085
kwa mwezi.
“Kwa kutumia
takwimu hizi, matokeo yanaonesha kuwa zaidi ya robo (asilimia 28.2) ya watu
wote waishio Tanzania Bara, wako chini ya mstari wa kiwango cha umaskini wa
mahitaji ya msingi na asilimia 9.7 ya watu wote wapo chini ya mstari wa
umaskini wa chakula,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo,
taarifa hiyo imeonesha kuwa kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kwa
Tanzania Bara kimekuwa kikipungua kwani mwaka 2007, kilikuwa asilimia 33.6.
“Matokeo ya
awali yanaonesha kupungua kwa kiwango cha umaskini kati ya 2007 na 2011/12.
Upimaji wa mwenendo wa umaskini utaainishwa kwenye Ripoti Kuu ya Utafiti wa
Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, 2011/12,” imeeleza taarifa hiyo.
Hesabu
zilizopigwa na wataalamu wa takwimu walioandaa taarifa hiyo, zimebainisha kuwa
kunahitajika Sh bilioni 103.3 kwa mwezi (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1.2 kwa
mwaka), ili kuondoa umaskini wa mahitaji ya msingi kwa watu waishio chini ya
mstari wa umaskini Tanzania Bara.
Pia
imeelezwa kuwa kama watu wote wangegawanywa katika makundi matano yanayolingana
na ukubwa wa matumizi yao kuanzia wa chini hadi wa juu, matumizi ya watu wa
kundi la juu (matajiri sana) ni mara nne (4) ya matumizi ya kundi la chini
(maskini sana) kwa Tanzania Bara.
Katika elimu,
taarifa hizo zimeonesha kuwa asilimia 20 ya Watanzania (Tanzania Bara) wenye
umri wa miaka 15 au zaidi hawana elimu ambapo kwa mwaka 2007 ilikuwa ni
asilimia 19.
Aidha,
uandikishwaji katika shule za msingi kwa watoto wenye umri kati ya miaka 7 hadi
13, umeshuka na kufikia asilimia 78 kwa mwaka 2011/12 ikilinganishwa na
asilimia 84 katika mwaka 2007. Hata hivyo kwa upande wa sekondari, uandikishaji
umetajwa kuongezeka kutoka asilimia 15, mwaka 2007 mpaka 29, mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment