SOMA:-Mahakama Mkoani Kagera imewavua nyadhifa za udiwani madiwani 6 kwa kosa la kutohudhuria vikao vya Kikanuni vya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, June 21, 2014

SOMA:-Mahakama Mkoani Kagera imewavua nyadhifa za udiwani madiwani 6 kwa kosa la kutohudhuria vikao vya Kikanuni vya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.


Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Kagera imewavua nyadhifa za udiwani madiwani 6 kati ya 8 waliokuwa wakishitakiwa kwa kosa la kushindwa kuhudhuria vikao vya Kikanuni vya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani humo.

Akisoma Hukumu, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Bw Charles Uwisso amesema madiwani hao wamevuliwa udiwani baada ya mahakama kuridhika na ushahidi wa pande zote mbili uliotolewa mahakamani hapo.

Amesema walalamikiwa hao wameshitakiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya, Elimu na Uchumi ya Halmashauri hiyo Bw Chifu Kalumuna ambaye ni Diwani wa kata ya Kahororo kupitia Chama cha Mapinduzi ( CCM ) aliyelalamika kuwa madiwani hao hawajahudhuria vikao vilivyoitishwa July 19, August Mosi, September 23, November 11 na Novemba 14 mwaka jana.
 
Kalumuna pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Manispaa ya Bukoba.

Madiwani walalamikiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Diwani Yusuph Ngaiza (Kashai -CCM), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo -CCM), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo -CCM) na Deusdedith Mutakyahwa wa Kata ya Nyanga -CCM.

 Wengine ni Richard Gaspar (Miembeni -CCM), Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu CCM), Israel Mulaki (Kibeta -CHADEMA) na Rabia Badru (Viti Maalumu -CUF).

Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kusoma taarifa ya ukaguzi kwenye manispaa hiyo, madiwani walitakiwa kuanza vikao mara moja.

Walalamikiwa walikuwa wanatetewa na Wakili Mathias Rweyemamu, huku mlalamikaji ukiwakilishwa na Wakili Aaron Kabunga.

Chanzo cha kesi hiyo ni mgogoro ambao umechukua muda mrefu na kusimama kwa maendeleo kati ya Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa hiyo, Dk Anatoly Amani.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa madiwani hao walikataa kuhudhuria vikao hivyo muhimu vya kamati hiyo hali iliyosababisha kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad