Kwa wiki
kadhaa sasa, kumeibuka msamiati mpya wa kisiasa wa UKAWA uliopelekea mpaka
kuundwa kwa BARAZA KIVULI LA UKAWA pale Bungeni bila kufuata Utaratibu.
Sisi
viongozi ambao miongoni mwetu ni Wajumbe wa vikao halali vya chama ambavyo ni
Baraza Kuu na Mkutano mkuu wa chama kutoka mikoa ya Tanga, Pwani na DSM kwa
masikitiko makubwa tunasema kuwa hatupendezeshwi na mwenendo huu wa chama
unaofanywa na viongozi wetu wakuu.
KUSUSIA
BUNGE LA KATIBA.
Kwa namna
ambavyo tumepambana kwa miaka mingi kudai na kuishinikiza serikali kuridhia
uandikaji wa katiba mpya, ni mpumbavu pekee anayeweza kususia fursa ya uandishi
huo tena kupitia chombo huru (BUNGE LA KATIBA) kwa sababu tu ya mgongano wa
kimaslahi.
Tunasikitika
sana kuwaona viongozi wetu na wabunge wa chama chetu cha CHADEMA wamesahau kazi
tuliyowatuma ya kwenda kuandika katiba mpya yenye kuzingatia maslahi ya
wananchi badala yake wamekwenda kupigania vyeo.
Tumefedheheshwa
sana na namna ambavyo wawakilishi hawa wamekubali kutanguliza mbele maslahi yao
na kuyaacha maslahi ya wananchi ambao ndio waliuowatuma, kwenye Rasimu yenye sura
zaidi ya 18 ni uzezeta kususia sura 2 tu za mwanzo kisa tu maslahi yao ya
kugawana vyeo wanaona hayawezi kutekelezeka.
Tunaomba
ifahamike kwamba, hakujawahi kukaliwa kikao chochote halali cha chama chetu
kilichoazimia na kuwaagiza wajumbe wanaotokana na chama chetu wasimamie katiba
yenye SERIKALI TATU, na ikionekana haiwezekaniki WASUSE NA KUTOKA NJE YA BUNGE.
Huu ni
udhaifu unaotawaliwa na uroho wa madaraka, sisi kama viongozi halali wa
kikatiba wa chama hatujawahi kuwaza wala kuamua kuhusu ujinga huu, siku zote
tumekuwa tukiwasisitiza wajumbe wetu kwenye fursa yoyote watakayoipata kwenda
kusimamia mawazo na misimamo ya wananchi ambao ni wanyonge.
Tunawatuma
wajumbe wetu kuhakikisha tunapata katiba itakayosimamia na kuzitunza Rasilimali
zetu na wala si kweli kuwa Idadi ya Serikali kama ni 3 au 2 au 5 au zozote
inaweza kuwa muarobaini wa changamoto zetu.
Daima dumu
tumekuwa tukiamini kwenye mapambano ya Hoja ambayo ndio msingi mkuu wa
demokrasia ya kweli Tunayoisimamia kama CHADEMA.
Hivyo Basi
tunasema, si sahihi hata kidogo kwa wajumbe wetu wa Bunge la katiba kususia
vikao vile na ndio maana hata baadi ya wabunge wengi wa chama chetu wamekuwa
wakilalamika chini chini kwetu sisi wajumbe wa baraza kuu kwamba wamechoka sasa
kuburuzwa na viongozi wakuu wa chama na kwamba wao nao wana mawazo na misimamo
yao, sasa kwa niaba yao pia tumeona kama viongozi wa chama tulikemehe hili.
Nipo tayari
kuyataja majina ya wabunge hawa wanaolalamika kuburuzwa ambao ni zaidi ya
wabunge 31 wa kuchaguliwa na wa viti maalum.
Muungano
wetu huu wa UKAWA ni muungano wa kinafiki usiokuwa hata na hadidu za rejea,
hakunaga muungano duniani kote ambao waunganaji wake wanaungana kiujanja ujanja
tu kama walivyofanya viongozi wetu hawa. Hatuungi mkono na tunawataka
wasiendelee na upuuzi wao huu, warudi bungeni kama hawataki wajitoe tuchague
wabunge wengine watakaowawakilisha wananchi wanaotuamini.
Ni sawa na
ndoa ya mkeka, hakuna maridhiano, hakuna vikao, asubuhi wapenzi jioni wana
ndoa, ndoa ya namna hii kamwe haiwezi ikadumu hata kidogo.
BARAZA
KIVULI LA UKAWA.
Tunasikitika
sana na kitendo cha mwenyekiti wa CHADEMA ndugu Freeman Mbowe, kutufanya sisi
wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu hatuna maana kwenye kufanya maamuzi ya
chama.
Walituaminisha
kwamba CUF wamefunga ndoa na CCM na kwamba wao ni sehemu ya serikali hivyo
hawawezi kushirikiana na chama ambacho ni sehemu ya serikali, kwa msingi huu
tukaazimia kwenye vikao vya chama ambavyo ni halali kwamba chama chetu
hakitashirikiana na chama kingine chochote cha siasa kwa kuwa ni washirika wa
CCM na kwamba wao ni CCM-B
Tumemkashigu
na kumtuhumu James Mbatia na NCCR nzima kuwa ni Tawi la CCM na ndio maana hata
Mbatia ameteuliwa kuwa Mbunge, inakuwaje leo tunashirikiana na watu hawa ambao
wanatumiwa na CCM?.
Ni lini
Muungano wa CCM na CUF umevunjika rasmi?.
Ni lini
ushirikiano wa NCCR ya MBATIA na CCM umekufa rasmi?.
Je mazingira
yaliyofanya tuwahesabu wenzetu hawa kuwa ni CCM B leo yamebadilika?, na kama
yamebadirika yamebadilika lini na yamebadilikaje?.
Je sio kweli
kwamba tuliwatenga wenzetu na kuwakashifu kwa sababu tu ya uchu wa madaraka?.
Yaani sio
kweli kwamba tuliwafedhehesha wenzetu hawa kwa sababu ya UWAZIRI KIVULI?. Na
leo tunawasafisha wenzetu hawa kwa UWAZIRI KIVULI HUO HUO.
Kwanini
viongozi wetu wanakuwa na UCHU na UROHO wa MADARAKA kiasi hiki?.
Kama
tunaweza tukawaita wenzetu MASHETANI asubuhi na jioni tukawaita MALAIKA kwa
sababu ya UWAZIRI KIVULI, je tukipewa nchi na kushika dola, si Tutawaita
wenzetu majina mabaya zaidi?.
Si tutakuwa
na serikali mbovu nay a ajabu zaidi ya hivi sasa tulivyo kwenye siasa za
upinzani tu tulio nao?.
Kwa misingi
huu, Tunaamini kuwa UKAWA ni UNAFIKI WA KISIASA, na umebuniwa kwa sababu moja
tu nayo ni kugawana vyeo, hakuna sababu yoyote yenye mantiki iliyopo kwenye
uundwaji wa UMOJA huu na ndio maana hauna hadidu za rejea wala hauna hati za
makubaliano miongoni mwetu.
Napenda
kuwaambia watanzania kuwa sisi baadhi yab wajumbe wa Baraza kuu na mkutano mkuu
wa mikoa ya Pwani, Dsm na Tanga hatuungi mkono upuuzi wowote wenye lengo la
kusimamia ugawanaji wa vyeo na madaraka, watu wa namna hii tunawaita WALAFI wa
MADARAKA.
Tunaunga
mkono watanzania wote wanaoitakia heri Tanzania yetu.
Mungu
ibariki Tanzania
Imeandaliwa
na Baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Mikao ya Pwani, DSM na
Tanga na kusomwa na Joseph Yona Patrick ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA WILAYA
YA TEMEKE, Mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa TEMEKE
MJUMBE WA
BARAZA KUU CHADEMA TAIFA, MJUMBE WA MKUTANO MKUU CHADEMA TAIFA na MJUMBE WA
KAMATI YA UTENZAJI BAVICHA TAIFA.
No comments:
Post a Comment