Akizungumza
na waandishi wa habari Bungeni mjini Dodoma jana(May 07,2014), CAG Ludovick Utouh alivitaja
vyama ambavyo havina akaunti benki kuwa ni UMD, NLD, NRA na ADC.
“Katika
hesabu walizotuletea kulikuwa hakuna ushahidi kwamba wanaendesha akaunti benki,”
alisema huku akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume na Kifungu cha 15(1) cha
Sheria ya Vyama vya Siasa.
Halikadhalika
katika ukaguzi huo, vyama vya siasa 11 kati ya 21 vyenye usajili wa kudumu,
havikuwasilisha taarifa za hesabu za mwaka kama Kifungu cha 14(1) cha sheria
hiyo ya mwaka 1992 kinavyosema.
Alipoulizwa
baadaye vyama hivyo, Utouh alivitaja CCK, UPDP, Tadea, Demokrasia Makini,
Chausta, DP na AFP.
Vyama vya Sauti ya Umma na Chauma viliwasilisha hesabu zao
vikiwa vimechelewa.
Utouh alisema
katika ukaguzi huo, taarifa za hesabu zilizowasilishwa na vyama 10 hazikufuata
misingi ya mfumo wa utoaji wa taarifa za fedha za kimataifa.
“Tulibaini
kuwa hakuna chama cha siasa hadi sasa kilichowasilisha kwa msajili wa vyama vya
siasa tamko la mali zote zinazomilikiwa na chama husika jambo ambalo ni kinyume
cha sheria,” alisema.
Utouh
alitumia mkutano wake huo na wanahabari kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto kwa kusimama kidete kuhakikisha
vyama vya siasa navyo vinakaguliwa na CAG kama sheria inavyoelekeza.
Kwa upande
wake Zitto, naye alimpongeza CAG kwa kukagua vyama vya siasa akisema ni kati ya
maeneo yaliyokuwa na matatizo.
“Kwa kitendo
chako cha kuamua kukagua bila hata ya kupewa fedha ni kitendo ambacho
kinaonyesha uzalendo wako wa hali ya juu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Kwa sababu
tunachokitaka sisi ni kila senti ya mlipa kodi ikaguliwe na kama nilivyowahi
kusema huko nyuma kwa miaka minne vilikuwa vimepewa ruzuku ya Sh69 bilioni.”
Zitto
alihoji kama CAG anakwenda kukagua bodi za mazao nchini ni kwa nini vyama vya
siasa visikaguliwe wakati ndivyo vinavyozalisha Serikali pale vinaposhinda
uchaguzi?
Habari Na:-Mwananchi.
No comments:
Post a Comment