Wataalamu
tunao, tumewatelekeza- Anna Abdalah.
MBUNGE wa Viti Maalum, Anna Abdalah amesema nchi imewatelekeza wataalamu mbalimbali waliopo jeshini, ambao wanakaa kambini wakiwa hawana kazi ya kufanya. Alisema baadhi ya zana za kivita zinaweza kutengenezwa katika sehemu kama Nyumbu, lakini kutokana na ukosefu wa fedha za kuendeshea kitengo hicho, matokeo yake askari hao wameendelea kukaa kambini bila kazi na hivyo kutotumika kwa vipaji vyao.
Aidha,
mbunge huyo mkongwe alisema alama nyingi za mipakani ambazo ziliwekwa na Jeshi
zimeondolewa na hivyo kutojulikana wapi ni wapi, hasa katika mipaka ya nchi
jirani.
Wanaofariki
nje hulipwa na nani?
Wabunge wamehoji juu ya askari wanaotumika kulinda amani katika baadhi ya nchi duniani, kwamba wanalipwa na nani kati ya serikali au Umoja wa Mataifa, kwani wanapokuwa huko, hutumika chini ya kofia ya UN.
Wametaka pia
kujua idadi ya askari waliofariki dunia wakiwa katika utumishi huo nje ya nchi
na kutaka kufahamishwa jinsi familia zao zinavyolipwa fidia.
Mbona
fedha za Jeshi zinacheleweshwa?
WAbunge pia wamezungumzia suala la Wizara ya Fedha kushindwa kupeleka fedha za Wizara ya Ulinzi kwa wakati kwa visingizio kwamba fedha hakuna, wakati inajulikana kuwa fedha zipo.
Walisema ni
jambo la hatari kwa nchi iwapo askari ambao hufanya kazi usiku na mchana kwa
ajili ya kulilinda taifa lao, litachoka kusubiri fedha, wakitolea mfano kuwa
mwaka jana walipokea kiasi cha asilimia 20 tu ya fedha zao za bajeti.
Masilahi
ya wastaafu yaliliwa.
Kapteni Mstaafu wa Jeshi, John Chiligati amesema ulipwaji wa mafao ya askari wastaafu wa Tanzania hauko vizuri na kupendekeza nchi ijifunze kutoka India, kwani huko, licha ya kulipwa vizuri, lakini pia huwezeshwa kwa namna mbalimbali ili wasipate taabu katika maisha yao.
Alisema kwa
vile askari hustaafu kulingana na vyeo vyao, wale wenye ujuzi wa aina
mbalimbali, hutafutiwa kazi mbadala uraiani au kukopeshwa pesa na vyombo vya
fedha ili waweze kujiajiri kwa kutumia taaluma zao uraiani.
Maonyesho
ya Jeshi Dar yawagawa.
Katika michango hiyo ya wabunge, baadhi yao walitofautiana kuhusiana na maonyesho yaliyofanywa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam April 26 mwaka huu.
Mmoja wa
wachangiaji hao alishangaa ni kwa namna gani Jeshi hilo liliweza kuanika silaha
zake hadharani, kwani kwa kufanya hivyo, ni rahisi kwa adui kujua namna ya
kukabiliana naye. Alikifananisha kitendo hicho na mtu kuonyesha kila kitu chake
hadharani, ikiwemo nguo yake ya ndani.
Hata hivyo,
wachangiaji wengine walisema maonyesho hayo ni jambo la kawaida na kwamba
baadhi ya nchi kubwa nazo hufanya namna hiyo, wakizitaja kama China, India na
Marekani.
Wahindi
wapigwe marufuku Jeshini.
Mbunge mmoja alimtaka Waziri Mwinyi kuangalia uwezekano wa kuwaondoa wafanyabiashara wa Kihindi katika maduka makubwa yaliyo ndani ya kambi za kijeshi (Supermarkets) na kutaka kazi hiyo kupewa wazawa.
Huku
akisisitiza kuwa hakuwa mbaguzi wa rangi, alisema kazi za kuendesha maduka
hayo, tena ndani ya kambi za jeshi, inapaswa kufanywa na watanzania wazawa,
hasa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Aidha,
mbunge mwingine alishangaa na kuhoji kwa nini bei za bidhaa katika maduka ya
jeshi zimekuwa sawa na maduka ya uraiani wakati kule jeshini kuna msamaha
maalum wa kodi kiasi cha asilimia 18.
Hee,
Tanzania ya 20 nguvu za kijeshi Afrika.
Katika hali isiyotarajiwa, mbunge mmoja alisema licha ya mbwembwe nyingi zilizoonyeshwa na Jeshi la Wananchi siku ya Muungano jijini Dar es Salaam, Tanzania ni ya 20 kwa majeshi yenye nguvu barani Afrika, kwa mujibu wa mitandao inayozungumzia nguvu za majeshi duniani (hakutaja mtandao huo).
Alisema
katika mataifa yote duniani, Tanzania inashika nafasi ya 102 kwa nguvu za
kijeshi, huku akiponda kuwa nchi yetu inazidiwa hata na nchi za Uganda na
Rwanda ambazo zipo juu kimsimamo, kwa sababu ya kile alichosema serikali
kushindwa kuipa wizara husika fedha za kutosha kuweza kujitosheleza.
Wanaopitia
JKT, JKU janga la kitaifa.
Baadhi ya wabunge pia walisema kuwaacha bila kuwapa ajira vijana wanaomaliza mafunzo ya kijeshi katika majeshi ya JKT na JKU ni janga la kitaifa kwa sababu wanapofika uraiani na kukutana na ugumu wa maisha, wanaweza kufanya lolote ili kukabiliana na ugumu huo.
Walisema
wakiwa wanafahamu kutumia aina mbalimbali za silaha, ni rahisi kwao
kushawishika kwenda kushiriki matukio ya uhalifu, endapo atajitokeza mtu na
kuwaeleza juu ya uwezekano wa kupata kiasi kikubwa cha fedha.
Kwa ajili
hiyo, waliitaka wizara kuwapa kipaumbele vijana hao wanaomaliza mafunzo katika
ajira, ikiwa ni njia ya kusaidia kuokoa vijana ili wasijihusishe na vitendo vya
kihalifu.
Kupima Ukimwi
iwe lazima JWTZ.
Mbunge mwingine alisema kwa kuwa vijana wa JWTZ wana jukumu kubwa la kuhakikisha mipaka ya nchi yetu inakuwa salama muda wote, wakati sasa umefika kwa kila anayetaka kuajiriwa, lazima apimwe afya yake ili kujiridhisha.
Alisema
jambo hili linapaswa kuzingatiwa hasa kwa vile kama hali itaachwa iendelee hivi
hivi, ipo siku taifa linaweza kujikuta likimpeleka mtu mgonjwa vitani, ambaye
anaweza kufariki kabla ya kufika katika uwanja wa mapambano.
Aidha,
walisema wanajeshi wanapata ugonjwa huo kutokana na kuachwa nyuma kwa wake au
wapenzi wao wakati wanapohama kutoka kambi moja kwenda nyingine, kitu
kinachowafanya wachepuke.
No comments:
Post a Comment