Baadhi ya
wajumbe wa Bunge Maalum la Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wameondoka kwa hasira katika kikao cha bunge hilo leo(April 16,2014) kinachoendelea mjini
Dodoma. |
Wajumbe wa
bunge hilo ambao ni kutoka upande wa upinzani chini ya umoja unaojulikana kama
UKAWA, yaani Umoja wa Katiba ya Wananchi, wameamua kutoka nje kupinga kile
wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya wananchi wanaotaka muungano wa
muundo wa serikali tatu kama yalivyopendekezwa katika rasimu ya katiba hiyo.
Kilio cha Mwananchi
Akichangia
katika kikao cha bunge hilo Jumatano jioni, mmoja wa wajumbe Profesa Ibrahim
Lipumba amelalamikia kauli za ubaguzi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe,
hususan wanaotaka muundo wa muungano wa serikali mbili, alieleza sababu za
kutaka serikali tatu kuwa zitasaidia kutatua matatizo yaliyopo katika muundo wa
sasa.
Hata hivyo
hakusita kupinga kile anachokiita kauli za ubaguzi kutoka kwa wajumbe
wanaopinga mawazo ya wachache bungeni humoi.
"Hatuwezi
kuwa kama kundi la wapiganaji linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili
hatulikubali, hatulikubali, hatulikubali, watu wote tunaotaka katiba ya
wananchi tunawaachia muendelee na kikao chao.Ahsanteni sana".
Mara baada
ya kusema hivyo, wajumbe waliounga mkono kauli yake waliinuka na kutoka nje.
Hata hivyo,
kikao cha bunge hilo kiliendelea baada ya makamu mwenyekiti wa bunge hilo
kusema idadi ya wajumbe waliobaki walitosha kuendelea na kikao hicho.
Muundo wa
Serikali
Wanaounga
mkono muundo wa serikali tatu, wanasema muundo wa sasa wa serikali mbili
umeshindwa kutatua masuala yenye mgogoro katika muungano, maarufu kama kero za
muungano, hivyo kudhoofisha muungano huo.
Hata hivyo
wajumbe wanaounga mkono serikali mbili, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanasema muundo wa serikali tatu
ni kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia itakuwa gharama kuiendesha
serikali ya tatu.
Bunge hilo
lenye zaidi ya wajumbe mia sita linaundwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Baraza la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201
walioteuliwa na rais wa Tanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
Wajumbe 191
kutoka upinzani walitoka nje ya bunge kupinga mwenendo wa bunge hilo katika
kujadili rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment