![]() |
|
Kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
Kabwe Zitto dhidi ya chama hicho, imeahirishwa hadi Mei 29 mwaka huu,
itakapotajwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
|
Msajili wa Mahakama Kuu, Amir Msumi aliahirisha kesi hiyo jana kwa kuwa
Jaji John Utamwa anayeisikiliza, anaumwa.
Katika kesi hiyo, Zitto anaomba Mahakama itoe zuio kwa Kamati Kuu au
chombo chochote cha chama, kujadili uanachama wake hadi atakapokata rufaa ya
kupinga uamuzi uliomvua uongozi wa chama. Anaomba Mahakama imwamuru Katibu
Mkuu, Dk Willbrod Slaa.
Ampe nakala zinazotoa sababu za uamuzi wa kumvua uongozi katika kikao
kilichofanyika Novemba 22 mwaka jana, ili akate rufaa katika Baraza Kuu la
Chama.
Aidha, anaomba mahakama iamuru Chadema isiingilie kazi zake za ubunge
wala uanachama wake.
Zitto amefungua kesi hiyo dhidi ya Baraza la Wadhamini la chama hicho na
Dk Slaa. Kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa, Mahakama ilitoa amri kwa Kamati
Kuu au chombo chochote cha Chadema, kutojadili uanachama wa Zitto hadi kesi
hiyo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika uamuzi huo, mahakama ilikubali ombi la Zitto, ambaye ni Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, kwa kuwa hoja zake zimekidhi matakwa ya kisheria ya kutolewa
kwa zuio la muda la kujadiliwa kwa uanachama wake.
Jaji Utamwa alisema Zitto amekidhi matakwa ya kisheria, kwa kuwa zuio hilo
lisipotolewa na akavuliwa uanachama, atapoteza nafasi ya ubunge na kushindwa
kutumikia wananchi waliomchagua na pia atapoteza nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge
wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali.
Zitto alivuliwa wadhifa wake Chadema, sambamba na aliyekuwa mjumbe wa
Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba,
kwa kilichodaiwa ni usaliti kwa chama hicho.






No comments:
Post a Comment