Waraka huo wa kurasa 22 unaoainisha
mambo yenye masilahi kwa chama hicho, unawataka wajumbe wake kuutetea bungeni.
Gazeti hili limefanikiwa kuona waraka
huo, ambao pamoja na mambo mengine, umetoa mapendekezo katika ibara 42 za
Rasimu ya Katiba ya Tume na kupangua hoja nyingi.
Katika miongoni mwa hoja hizo, chama
hicho kimesisitiza muundo wa Muungano wa Serikali mbili lakini kikapendekeza
kuwapo Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu waraka
huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliukana akisema pamoja na
msimamo wa chama hicho kuwa ni Serikali mbili, hakijafikia hatua ya kuwa na
waraka.
Alisema vikao vya juu vya chama huwa
havitoi waraka, bali msimamo na kwamba vyombo vingine vya chama ndivyo hutoa
waraka, lakini hadi sasa havijafikia hatua hiyo.
Alisema kuwa alipoeleza maazimio ya
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alitaja msimamo wa chama hicho kuwa ni
Serikali mbili zilizoboreshwa, lakini hakutaja maboresho hayo hata pale
alipoulizwa na waandishi wa habari kwa sababu hayakuwa yamekamilika.
Hata hivyo, wajumbe watatu wa NEC kwa
nyakati tofauti waliomba wasitajwe gazetini walisema mambo yaliyomo kwenye
waraka huo ndiyo waliyokubaliana lakini hakuwa na uhakika kama ulishasambazwa.
Kwa mujibu wa waraka huo, chama hicho
kinadaiwa kuainisha mambo kiliyopendekeza katika Rasimu ya Kwanza na jinsi
yalivyoshughulikiwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Pia, kimeeleza mambo mengine mapya na
kubainisha kasoro zake, ikiwamo utata katika mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.
Waraka huo pia unazungumzia sura mpya
ya 17 katika Rasimu ya Katiba, ukisema inazungumzia mambo ya mpito kuelekea
kupata Katiba Mpya, lakini gharama za utekelezaji wake hazitabiriki.
Sababu za Serikali mbili.
Katika waraka huo, CCM kinadaiwa kueleza
kuwa mapendekezo yake kuhusu muundo wa serikali mbili hayatokani na sera yake
pekee, bali pia udhaifu uliojionyesha katika pendekezo la muundo wa Serikali tatu.
“Hivyo basi, CCM inapendekeza kwamba
mfumo wa serikali mbili ufanyiwe marekebisho ambayo yatashughulikia changamoto
zilizopo,” imesema sehemu ya waraka huo.
Wakati CCM kikitaka Muungano wa
serikali mbili, Rasimu ya Pili ya Tume inapendekeza serikali tatu, sawa na zile
zinazopigiwa chapuo na vyama vya Chadema na CUF.
Idadi ya Serikali katika muundo mpya wa
Muungano, bado ni changamoto kutokana na hatua ya wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kugawanyika katika makundi yenye mitazamo tofauti.
Makamu wa Rais.
Katika mfumo huo wa serikali mbili,
waraka huo umependekeza Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais bila kujali kama
Rais wa Jamhuri ya Muungano anatoka Bara au visiwani humo.
“Rais wa Zanzibar katika Muungano, awe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa na msaidizi wake kwa
masuala ya Zanzibar na mmoja wa viongozi wakuu wa nchi,” imesema sehemu ya
waraka huo na kuongeza:-
“Hii itaongeza na kuweka wazi madaraka
ya Rais wa Zanzibar ndani ya Serikali ya Muungano na nje ya nchi,” imesema
sehemu ya waraka huo.
Muundo wa Bunge.
Kuhusu Bunge, waraka huo unapendekeza
kuwe na Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara kwa ajili ya kushughulikia
masuala ya Bara tu.
“Katika pendekezo hili, majimbo ya
Jamhuri ya Muungano yaundwe upya na majimbo ya uchaguzi ya Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar yawe ndiyo hayohayo majimbo ya uchaguzi ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano,” ulisema waraka huo.
Waraka huo umependekeza Bunge la
Muungano wakati linajadili mambo ya Muungano, wabunge wote washiriki
majadiliano na inapofika kujadili mambo ya Tanzania Bara, washiriki wabunge
wanaotoka Bara tu.
“Kama Spika anatoka sehemu moja ya
Muungano, Naibu wake atatoka upande wa pili na wakati wa vikao vya masuala ya
Bara Spika/Naibu Spika anayetoka Bara ndiye atakayeendesha kikao,” sehemu ya
waraka huo inasema.
Waraka huo umependekeza masuala
yasiyokuwa ya Muungano, kushughulikiwa na wabunge wa Tanzania Bara pekee.
![]() |
Katibu wa
NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akiangalia matembezi ya mshikamano wakati
yakiingia uwanjani kabla hajaanza kuhutubia wakazi wa Shinyanga mjini.
|
Muundo wa Mawaziri.
Waraka huo umependekeza wajumbe wa
Bunge la Muungano kuwa mawaziri wa wizara za mambo ya Muungano tu na wizara
zisizo za Muungano ziongozwe na wabunge wanaotoka Tanzania Bara tu.
Pia umependekeza orodha ya mambo ya
Muungano ambayo yatakuwa katika Katiba na mambo yasiyokuwa ya Muungano
yaorodheshwe katika sheria itakayoainisha pia usimamizi, utekelezaji na gharama
zake.
Mahakama.
Kwa upande wa muundo wa Mahakama ya
Juu, waraka umependekeza ndani ya mahakama hiyo kuwe na kitengo cha masuala ya
Katiba tu.
Kuhusu misaada na mikopo nafuu kutoka
kwa wahisani, umependekeza Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya
Zanzibar, zijadili kwa kina kanuni ya mgawanyo wa fedha zinazotokana na vyanzo
hivyo.
“Kuwekwe utaratibu wa kisheria wa
kutenganisha misaada inayoelekezwa kwenye miradi ya Muungano na isiyokuwa ya
Muungano,” ilisema sehemu ya waraka huo.
Usimamizi wa Muungano.
Waraka huo umependekeza kuwapo kwa Tume
ya Usimamizi na Uratibu wa mambo ya Muungano kikatiba na uendeshaji wake,
kadhalika na mwenendo wa sasa wa vikao vya pamoja vinavyohusu kero za
Muungano.
“Uratibu na usimamizi wa masuala ya
Muungano uwekwe kisheria na Tume ipewe mamlaka ya kuzisimamia taasisi zote za Muungano
katika makubaliano yatakayofikiwa na pande zote mbili,” unasema waraka huo.
Kuhusu Tume ya Pamoja ya Fedha, waraka
huo unasema tume hiyo ambayo imetamkwa katika Katiba na kupitishwa na Sheria ya
Bunge, imeshaundwa na mamlaka yake yanafahamika.
“Tunapendekeza Tume hii ipewe nguvu
zaidi, iwekewe mfumo madhubuti wa kuiendesha na kuisimamia kwa karibu.
Mapendekezo yanayotolewa na Tume yashughulikiwe na serikali zote mbili kwa
haraka ili kama hakuna kikwazo, mapendekezo yake yatekelezwe bila kuchukua muda
mrefu,” unasema.
Pia waraka huo umependekeza kufunguliwa
kwa akaunti ya pamoja ya fedha zitokanazo na mapato ya vyanzo vya Muungano,
kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwapo
kwa utaratibu wa kisheria utakaoelekeza uendeshaji wa akaunti hiyo na kuweka
mgawanyo wa mapato hayo kwa pande mbili za Muungano.
“Hii itasaidia sana kuwianisha uchumi
wa pande hizo mbili. Sheria kuhusu utaratibu huo isimamiwe na Tume ya Uhusiano
na Uratibu kama ilivyopendekezwa katika rasimu,” waraka huo unasema.
Habari Na:-Mwananchi.
No comments:
Post a Comment