Kalumuna, ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Manispaa ya Bukoba na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi alifungua shauri dhidi ya madiwani hao kuwa wamepoteza sifa za kuendelea kuwa madiwani kwa kushindwa kuhudhuria vikao vya kisheria bila taarifa.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Diwani Yusuph Ngaiza (Kashai), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Deusdedith Mutakyahwa wa Kata ya Nyanga.
Wengine ni Richard Gaspar (Miembeni), Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Israel Mulaki (Kibeta) na Rabia Badru (Viti Maalumu).
Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kusoma taarifa ya ukaguzi kwenye manispaa hiyo, madiwani walitakiwa kuanza vikao mara moja.
Hata hivyo, Kalumuna aliweka pingamizi dhidi ya madiwani hao kutohudhuria vikao mpaka itakaposikilizwa kesi ya msingi aliyofungua dhidi yao.
Baada ya mahakama kupitia hoja za mlalamikaji na walalamikiwa kupitia kwa mawakili wao, Hakimu wa mahakama hiyo, Charles Uisso alisema mahakama hiyo ina uwezo kisheria kusikiliza shauri lao na kutaka upande wa walalamikiwa kupeleka hoja nyingine za msingi kama zitakuwapo.
Upande wa walalamikiwa umetakiwa kuwasilisha hoja mpya za utetezi Machi 3, kwa uamuzi huo vikao vya Baraza la madiwani vitaendelea kusimama kusubiri uamuzi wa mahakama.
Walalamikiwa wanatetewa na Wakili Mathias Rweyemamu, huku mlalamikaji ukiwakilishwa na Wakili Aaron Kabunga.
Chanzo cha kesi hiyo ni mgogoro ambao umechukua muda mrefu na kusimama kwa maendeleo kati ya Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa hiyo, Dk Anatoly Amani.
Habari na:-Mwananchi.
No comments:
Post a Comment