![]() |
| Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama hicho jana(Januari 18,2014). |
Leticia
Ghati na Haji Ambar Khamis jana wamechaguliwa kuwa Makamu Wenyeviti wa Chama
cha NCCR-Mageuzi, katika Mkutano Mkuu wa Nane wa chama hicho uliofanyika kwenye
Ukumbi wa Diamond Jubilee jana
Ghati ambaye
amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti (Bara) alikuwa akiwania nafasi hiyo na
Anyimike Mwasakalali, Rakia Abubakar Hassan na Danda Juju ambao walijitoa
kugombea dakika za mwisho.
Kwa upande
wa Ambar Khamis(Makamu Mwenyekiti Bara) alipita bila kupingwa kutokana na
kuwania peke yake nafasi hiyo.
Msimamizi wa
Uchaguzi huo, Moses Machali ambaye pia ni Mbunge wa Kasulu Mjini, aliwatangazia
wajumbe wa mkutano huo kuwa Ghati na Ambar ni wagombea waliokosa upinzani, bila
kufafanua sababu za wapinzani wa Ghati kujitoa.
Awali katika
ufunguzi wa Mkutano huo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe alikitahadharisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuacha mpango wake wa kutaka
kukwamisha Mfumo wa Muungano wa Serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia CCM
kimetakiwa kutambua ya kuwa siku kitakapoondoka madarakani viongozi na
wanachama wake wataendelea kuwa katika hali ya usalama na wala hakuna
atakayelipiza visasi kwa kushindwa kusimamia umwagikaji wa damu za Watanzania
wasiokuwa na hatia.
Akizungumza
kwa niaba ya wenyeviti wa vyama vya upizani waliohudhuria mkutano huo alisema:
“Serikali tatu siyo sera ya chama chao sisemi kwamba ni lazima wakubali
serikali mbili au nne au moja sisemi hivyo, ila kauli kwamba siyo sera yao ni
kiashirio kwamba wanaangalia masilahi ya chama na si ya Taifa,” alisema Mbowe
huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.
Akitoa
salamu za CCM, Mangula alisema hakuhudhuria mkutano huo kwa lengo la kujibu
mapigo, bali kuangalia jinsi uchaguzi huo utakavyokuwa na mmoja wa wanachama wa
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Awali
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema damu za Watanzania
zinazomwagika ardhini bila hatia zinatokana na utawala mbovu wa CCM.
“Tunataka
maridhiano ya kitaifa, tuzungumze, turidhiane pamoja kwa kuweka masilahi ya
Taifa na rasilimali kwanza vyama badaye.” aliongeza
Naye Msajili
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliwataka wajumbe wa mkutano huo
kutumia fursa hiyo kuwachagua viongozi watakaokuwa na taswira ya kuwafikisha
mbali katika siasa.
“Wanachama
hii ndiyo nafasi pekee ya kuwachagua viongozi bora ambao wamekomaa na
wastaarabu watakaowaepusha na migogoro na wenye sura ya utaifa,” alisema Jaji
Mutungi.
Akitoa
salamu kwa niaba ya wageni waalikwa, kada wa CCM, Mustapha Sabodo alisema ili
CCM iondoke madarakani ni lazima vyama vya upinzani vikaungana pamoja kutokana
na CCM kuwa na fedha nyingi.
Pia Sabodo
alisema nchi inatakiwa kuwa makini katika masuala ya siasa ili kujiepusha nchi
kuingia katika machafuko kwani itahatarisha usalama za taifa.
“Mimi naijua
CCM vizuri, kuna mvutano wa nani agombee urais uchaguzi ujao na fedha
walizonazo ili iondoke madarakani ni lazima vyama vya upinzani vikaungana,”
alisema Sabodo
Katika
uchaguzi huo, jumla ya wajumbe wa mkutano mkuu walitakiwa kuwa 289 lakini waliohudhuria
walikuwa 213.
Nafasi
zilizokuwa zikiwaniwa katika uchaguzi huo ni Mwenyekiti Taifa, Makamu
Mwenyekiti (Bara), Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu
(Bara), Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Mweka Hazina, Wajumbe wa Halmashauri Kuu
Taifa na Makamishna wa Mikoa.
Mwenyekiti
wa chama hicho, James Mbatia na Katibu Mkuu wake, Samwel Ruhuza wanatetea
nafasi zao.
Habari Na:-Mwananchi.








No comments:
Post a Comment