Zaidi ya wanafunzi 9,000 wilayani Karagwe hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Hali hiyo
imebainika kutokana na utafiti uliofanywa na halmashauri ya wilaya hiyo mwaka
jana.
Ofisa Elimu
Shule za Msingi, Gidion Mwesiga, alibainisha hayo jana(Januari 18,2014) alipozungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake.
Mwesiga
alisema utafiti wa kubaini wanafunzi hao ulifanyika Mei katika shule mbalimbali
za wilaya hiyo kwa kushirikisha walimu, waratibu wa elimu kata na viongozi wa
Idara ya Elimu.
Alisema
utafiti huo ulibaini wanafunzi 9,786 wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu
ambapo wasichana ni 4,729 na wavulana ni 5,057.
Mwesiga
alisema wanafunzi hao ni wa darasa la pili hadi la sita katika shule 108 za
serikali na kata 22 zilizopo wilayani hapa.
Alitaja
baadhi ya kata ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika
ni Bweranyange (356), Nyakasimbi (386) na Chanika (453).
Alisema
tatizo kubwa la wanafunzi hao kutojua kusoma na kuandika ni kutokana na utoro,
baadhi ya wazazi kutokuwa na mwamko wa elimu na watoto wengine kutoanzia
madarasa ya awali.
Alitaja
baadhi ya mikakati iliyoandaliwa na halmashauri hiyo ili kukabiliana na tatizo
hilo kuwa ni kuwakaririsha wanafunzi wote wasiojua kusoma na kuandika,
kutengewa madarasa maalumu na muda maalumu baada ya saa za masomo kwa ajili ya
kufundishwa.
Chanzo:-Tanzania
daima.






No comments:
Post a Comment