|
Mamia ya
wakazi wa Ngara waliojitokeza katika mkutano wa Operesheni Pamoja Daima
uliohutubiwa na Mh Freeman Mbowe.
|
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amekionya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kuacha hila zozote zile ambazo
zitasababisha kuvunjika kwa mchakato wa katiba mpya unaoelekea hatua ya Bunge
Maalumu la Katiba.
Alisema
waache kufikiria kufanya hivyo kwani kwa hatua iliyofikia, Watanzania hawako
tayari kurudi nyuma kuendelea na katiba ya sasa.
Mwenyekiti
huyo wa CHADEMA taifa aliyasema hayo juzi jioni wakati akihutubia maelfu ya
wakazi wa Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya Operesheni ya
Movement For Change (M4C) iliyopewa jina la Pamoja Daima, ambayo inaendeshwa na
viongozi wa chama hicho nchi nzima, wakigawanyika katika timu sita – tatu
zikitumia usafiri wa helkopta na nyingine zikiwa ardhini.
Mbowe
alisema kuwa yupo tayari kuwa wa kwanza kufungwa kwa kosa la kudai katiba mpya
iwapo serikali itaweka mazingira ya hila ambayo yatalazimisha kukwamisha
mchakato wa kupata katiba mpya, hivyo Watanzania kulazimika kuendelea na katiba
ya zamani ya mwaka 1977.
Alisema kuwa
watawala wasitumie hila na mwanya wowote kuitia nchi majaribuni kwa kulazimisha
watu ‘kuishi’ na katiba ya sasa aliyosema imekosa uhalali wa kisiasa na
kisheria, bali wanatakiwa kuhakikisha mazingira mazuri yanapatiana kwa
Watanzania kujiamulia wanavyotaka kuongozwa, huku akisisitiza kuwa katiba ni
uhai wa taifa, si matakwa ya chama chochote cha siasa wala mtu binafsi.
Mbowe
alisema kuwa Watanzania wengi wamependekeza kuwapo kwa shirikisho la serikali
tatu katika rasimu ya katiba mpya, lakini akadai kuwa zipo njama zinazofanywa
za kuchakachua maamuzi hayo ya wananchi kwa ajili ya kuilinda CCM.
Alisema
iwapo hila hizo za kupindua maoni ya wananchi zitafanikiwa kupenyezwa kupitia
bungeni, yuko tayari kuungana na Mtanzania yeyote kuzunguka nchi nzima
kuwahamasisha wananchi waikatae rasimu hiyo.
Alisisitiza
kwa kusema kuwa endapo wananchi wataikataa katiba hiyo, pia hawatakuwa tayari
kurudi kuendelea kutumia katiba ya zamani inayotumika hivi sasa kama ambavyo
serikali imekwishasema.
“Watawala
lazima wajue. Watanzania hawa ambao wameipigania na kuililia katiba mpya kwa
muda mrefu sasa, hawako tayari tena kurudi nyuma.
Maana kuna kipengele cha
sheria kimewekwa kwamba mchakato huu wa sasa ukishindikana kwa maana kwamba
wananchi wakipiga kura ya maoni kuikataa rasimu itakayokuwa imepitishwa
bungeni, eti tunaendelea na katiba ya zamani.
“Kwa hiyo
kwa kutumia mwanya huo, kuna watu, tena wanaongozwa na chama kilichoko
madarakani, wamejipanga kuhakikisha kwamba wanachakachua maoni ya wananchi
yaliyotolewa ili ikifika wakati wa kura ya maoni wananchi waikatae, na hivyo
mchakato wote unafeli, tunarudi kwenye katiba ya zamani na hivyo kuanza mwanzo
tena mchakato wote.
“Kwa kweli
Ngara ninawaambia kwa hilo hatuko tayari. Wananchi wametoa maoni yao mengi
mengi kuhusu siasa, uchumi na jamii yazingatiwe kwenye katiba mpya, lakini
watawala wako tayari kuingiza nchi majaribuni kwa sababu tu wanataka kuendelea
kulinda ulaji wao. Wanataka uhai wa chama chao. Hatutakubali.
“Tena
wanaojipanga kuchakachua ni wale wanaokataa serikali tatu, eti sio sera ya
chama chao, alaah! Wanapata wapi jeuri hii ya kutaka katiba ya nchi iongozwe na
sera za vyama vya siasa na kwa nini chama chao ndiyo kielekeze katiba iweje
badala ya wenye katiba ambao ni wananchi wenyewe?
“Niko tayari.
Nitakuwa wa kwanza kufungwa endapo katiba inayoandaliwa sasa itachakachuliwa na
baadhi ya watu kwa sababu tu hawataki serikali tatu, kwani nitazunguka nchi
nzima kuhamasisha wananchi kuikataa na baada ya kuikataa pia hatutakuwa tayari
kurudia ile ya zamani.
“Haiwezekani
Watanzania walio wengi wakatoa maoni kuhusu siasa za nchi, kuhusu uchumi wa
nchi na mambo ya kijamii ili watengeneze mazingira ya fursa za maendeleo kwa
katiba wanayoitaka wao, halafu wengine, kikundi kidogo kwa maslahi ya chama
chao waichakachue eti tu kwa sababu ya maslahi yao binafsi ya kutaka
kujitengenezea mazingira ya ulaji.
“Katiba ni
uhai wa taifa hili. Ni uhai wa Watanzania wote siyo ya chama chochote cha siasa
au ya mtu fulani, mbona Zanzibar wenyewe wametengeneza katiba yao kwanini na
sisi tusingeneze ya Tanganyika? Walikuwa wapi wakati masuala yote yanayotishia
kabisa Muungano yanazidi kukomaa?” alisema Mbowe.
Aliongeza
kuwa haiwezekani kutumia muda mwingi na gharama kubwa ya fedha kuandaa katiba
hiyo halafu watu wengine wakaichakachua, na kwamba hata kama katiba hiyo
itakataliwa, haiwezekani kuendelea kutumika ile ya zamani inayotumika sasa,
bali ni lazima itaipasa serikali kuangalia utaratibu mwingine wa kuhakikisha
katiba mpya inapatikana.
“Wazo la
kurudi katika katiba ya zamani halipo kabisa, kama Serikali ya CCM
inajidanganya kwamba watachakachua katiba inayoandaliwa sasa halafu tukarudi
kutumia ile ya zamani, hiyo haipo na itawagharimu,” alisisitiza.
Kadhalika
Mbowe alisema kuwa watazunguka nchi nzima kuwahamasisha Watanzania kususia
zoezi la upigaji kura ya maoni ya katiba endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
itashindwa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Alisema
kupiga kura ni haki ya msingi ya Watanzania, na kwamba hadi sasa zaidi ya
Watanzania milioni tano na laki tatu hawana uwezo wa kupiga kura kwa sababu
hawana shahada ya kupigia kura.
Chanzo:
Tanzania Daima





No comments:
Post a Comment