Soma tathimini ya hali ya usalama 2013 iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Kigoma. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, January 03, 2014

Soma tathimini ya hali ya usalama 2013 iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Kigoma.


Jeshi la polisi Mkoani Kigoma limetoa ripoti ya tathimini ya hali ya usalama mkoani humo katika kipindi cha Januari hadi Disemba 27 mwaka 2013 ambapo makosa ya jinai yameongezeka kwa asilimia 20% kutoka makosa 20,305 yaliyoripotiwa mwaka 2012 hadi kufikia makosa 20,756.

Akitoa tathimini hiyo kwa waandishi wa habari mkoani Kigoma, Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma,Kamishina mwandamizi msaidizi wa polisi, SACP Frasser Kashai alisema sababu kubwa ya ongezeko la makosa yaliyoripotiwa ni uelewa wa wananchi wa jinsi ya kuripoti uhalifu na wahalifu na matokeo ya operation nyingi zilizofanyika kulinganisha na mwaka 2012

Alisema idadi ya watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya jinai katika kipindi cha Januari hadi disemba 27 mwaka 2013 imeongezeka mara tatu zaidi ambapo watuhumiwa 7,657 walikamatwa ukilinganisha na watuhumiwa 2, 353 waliokamatwa kwa makosa hayo mwaka 2012.

Makosa yaliyotia fora mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012 ni kupatikana na silaha na unyang’anyi wa kutumia silaha kosa ambalo linatokea zaidi maeneo ya vijiji vya mpakani mwa nchi jirani ya Burundi huku matukio ya mauaji na ubakaji yakipungua.

Katika ripoti yake kamanda wa polisi mkoani Kigoma, SACP Kashai alisema gram 810 za madawa ya kulevya aina ya Cocaine,Bangi kilo 585.5, pombe haramu ya moshi lita 3,520 na mitambo 29 ya kutengenezea Gongo vilakamatwa katika kipindi cha mwak 2013.

Idadi ya watuhumiwa waliokamatwa ni 514 ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo ilikamatwa pombe ya moshi lita 3,846 na mitambo 22, Bangi kilo 792 na watuhumiwa 372 dhidi ya makosa hayo.

Idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa mwaka 2013 imeongezeka ambapo jumla ya wahamiaji haramu 6,181 ikilinganishwa na wahamiaji haramu 598 waliokamatwa mwaka 2012.

Wahamiaji haramu waliokamatwa mwaka 2013 kati yao 5,135 ni kutoka nchini Burundi, 1,045 kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Congo DRC na 1 kutoka Rwanda 1 hivyo kuwepo ongezeko la ukamataji wa wahamiaji haramu 5,583 katika mkoa wa Kigoma.

Aidha kamanda Kashai alitaja matokeo ya makosa makubwa na madogo na hatua zilizofikiwa ukilinganisha na mwaka jana kuwa waliohukumiwa mwaka 2013 kwa makosa makubwa ni watu 201 ikilinganishwa na watu 310 mwaka 2012.

Kesi zilizofungwa na Polisi mwaka 2013 ni 346 ikilinganishwa na kesi 388 mwaka jana, Kesi zilizoko mahakamani mwaka 2013 ni 1,170 ikilinganishwa na kesi 966 mwaka jana.

Zilizoshindwa mahakamani ni kesi 124 ikilinganishwa na kesi 57 mwaka jana wakati zilizoko mahakama kuu ni kesi 22 ikilinganishwa na kesi 9 za mwaka jana.

Makosa madogo waliohukumiwa ni watu 1,052 mwaka 2013 ikilinganishwa na watu 1,414 mwaka jana. Kesi zilizofungwa na polisi mwaka 2013 ni 3,407 ikilinganioshwa na 4,463 mwaka jana, zilizoko mahakamani mwaka jana zilikuwa kesi 1,383 na mwaka 2013 ni kesi 1,052.

Upande wa makosa ya usalama barabarani kamanda Kashai alisema jeshi la polisi mkoani Kigoma kupitia kikosi cha usalama barabarani katika kipindi cha mwaka 2013 limekamata jumla ya makosa 12,987 ikilinganishwa na makosa kama hayo 10,920 yaliyokamatwa mwaka jan.

Kati ya hayo makosa 12,917 yalitozwa faini na kuiingizia serikali kiasi cha shilingi milioni 387.5 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo makosa 10,870 yaliyotozwa faini yaliingizia serikali kiasi cha shilingi milioni 326, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 19%.

Aidha alisema ajali za barabarani zilipungua kwa asilimia 7% kutoka ajali 289 mwaka jana hadi kufikia ajali 268 mwaka 2013 huku makosa makubwa yaliyoripotiwa kusababisha vifo na majeruhi  ni 140 ambapo kutokana na makosa hayo kesi 127 zilipelekwa mahakamani na zilizotolewa hukumu ni kesi 55 na kesi 72 bado hazijatolewa hukumu.

Takwimu hizo zimetaja kuwepo kwa ongezeko la watu waliofariki kwa ajali za barabarani kwa asilimia 31% ambapo mwaka 2013 kuna vifo 102 ikilinganishwa na mwaka jana watu 78 na kuna ongezeko la majeruhi kwa asilimia 26% kutoka majeruhi 57 mwaka jana hadi kufikia majeruhi 279 mwaka 2013.

Kuhusu matukio ya ajali za Pikipiki kwa mwaka 2013 kamanda Kashai alisema kulikuwepo na ajali 58 zilizosababishwa na pikipiki ambapo jumla ya pikipiki 77 zilihusika na katika ajali hizo wapanda pikipiki 24 walipoteza maisha na wapanda pikipiki 33 walijeruhiwa.

Aidha kamanda Kashai alisema jeshi la polisi mkoani Kigoma linawahakikishia wananchi hali ya amani na utulivu katika kipindi cha mwaka 2014 kutokana na mikakati iliyopo katika kupambana na uhalifu na wahalifu ikiwa ni pamoja kuendelea kutoka elimu ya usalama barabarani na ulinzi shirikishi kwa wananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad