|
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa mshtuko taarifa za tukio la
kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke,
Josephat Yona Patrick.
|
Chama
kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano, mbali ya kukemea kwa nguvu zote
tukio hilo la kihuni na mengine ya namna hiyo yenye lengo ya ukatili dhidi ya
binadamu, katika hatua ya sasa kinapenda kusema yafuatayo juu ya tukio hilo ovu
;
1. Jeshi la
Polisi lifanye uchunguzi juu ya tukio hilo la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti
wa CHADEMA Wilaya ya Temeke ili ukweli
ujulikane na haki itendeke, kwa sheria kuchukua mkondo wake.
2. Chama
kinawataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kutulia, hasa pale ambapo watu
wenye hila na malengo yao, wanaanza kukihusisha chama na tukio hilo. Watambue
kuwa pamoja na mtu yeyote kuwa kiongozi wa chama, bado anayo maisha yake na
uhusiano na watu wengine katika jamii.
3. Jeshi la
Polisi linapaswa kuyachukulia uzito mkubwa na unaostahili matukio ya namna hii
ambayo yanaanza kuota mizizi kutokana na watu waovu wanayoyatekeleza
kutochukuliwa hatua za kisheria ambazo zingesaidia kuzuia yasitokee tena.
4.
Watanzania bado wanakumbuka kwamba hadi sasa Jeshi la Polisi limeshindwa kutoa
taarifa za kina na kuchukua hatua za kisheria ambazo zingesaidia ukweli
kujulikana na haki kutendeka katika matukio ya kutekwa na kuteswa kwa kiongozi
wa madaktari Dk. Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom
Kibanda. Hivyo ingesaidia kuzuia matukio mengine kutokea.
5. Ni
kutokana na jeshi hilo kushindwa kuwajibika ipasavyo katika matukio mengine ya
namna hiyo, watu waovu wanaweza kutumia mwanya wa kinachoendelea ndani ya
CHADEMA kwa chama kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanachama wasio
waadilifu, kufanya matukio ya namna hiyo iii kujenga taswira ya kukihusisha
chama na uhuni huo unaobeba kila sifa ya kuitwa ukatili dhidi ya binadamu.
6. Aidha
kushindwa kwa Jeshi la Polisi kuwajibika ipasavyo katika kufanya uchunguzi wa
matukio hayo (yaliyotolewa kama mfano hapo juu) na mengine ya namna hiyo, jeshi
hilo linazidi kujiweka katika wakati mgumu wa kukwepa tuhuma za baadhi ya
watendaji wake kujua na kushiriki masuala haya, hususan kwa kurejea tukio la
kutekwa kwa Dkt. Ulimboka.
Imetolewa
leo Jumanne, Januari 7, 2014 na;
Kurugenzi ya
Mawasiliano na Uhusiano
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)







No comments:
Post a Comment