![]() |
|
Shekhe Mkuu
wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba, ametaka Waislamu kuacha kulalamika,
kwamba Wakristo wamekuwa wakipewa upendeleo, badala yake watumie fursa
wanazopata kuondokana na malalamiko hayo.
|
Akitoa mfano,
alisema Waislamu wanapaswa kupeleka watoto wao kusoma elimu zote mbili na
kuwaandaa kushika nafasi za kiutendaji ambazo wanalalamikia kuwa zimetolewa kwa
upendeleo kwa Wakristo.
Alisema hata
katika kukamata maeneo ya uwekezaji, Waislamu wamebaki nyuma kutokana na
kushindwa kujitolea kuchangia fedha za kutosha za kuanzisha miradi ya maendeleo
kwa ajili ya kuimarisha dini na kuendesha maisha yao.
“Msilalamike,
tunisheni mifuko katika misikitini yenu muwe na fedha za kutosha zitakazokuwa
kichocheo cha ninyi kushiriki katika shughuli muhimu za kiuchumi. Kosa ni lenu,
msilalamikie Wakristo hawana tatizo hata kidogo katika hilo,” alisema Mufti
Simba.
Madaraka
misikitini Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Taifa, Ally Mkoyogore, alitaka
Waislamu kuongeza bidii katika elimu na uchumi, badala ya kutumia muda mwingi
kupigania madaraka misikitini.
Alisema
kurudi nyuma kwa Waislamu, kunasababishwa nao wenyewe kushindwa kufuata maadili
na misingi ya dini yao, badala yake wanagombea uongozi misikitini kwa ajili ya
maslahi binafsi.
Maadhimisho
hayo ya Maulid yalihudhuriwa na viongozi wa dini kutoka mikoa mbalimbali
nchini, mashekhe kutoka Burundi huku Serikali ikiwakilishwa na Mkuu wa Mkoa
Kigoma, Issa Machibya.
Katika
salamu zake za siku hiyo, Alhaji Mwinyi alisema dini zote ukiwamo Uislamu,
hazikatazi waumini kushirikiana katika masuala mbalimbali, hivyo ni wajibu wa
kila upande kuusikiliza mwingine.
“Nchi
zinaijua Tanzania kuwa kisiwa cha amani kisicho na utofauti wa dini, kabila
wala rangi. Sote ni ndugu wamoja, tunapaswa kuendelea kuishi kwa usalama na
amani.
“Pale
inapotokea hali ya kutofautiana, tukae pamoja na kuzungumza ili tufikie mwafaka
na si kugombana,” alisema Mwinyi.
Alisema
Mtume aliongoza dini kwa kuhubiri mshikamano, kupenda wengine na kuthamini utu
na si vurugu kama ambavyo wengine wanadhani.
Akimkaribisha
Mwinyi kutoa salamu hizo, Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salumu,
alisema amani na utulivu nchini ndio ujumbe wa sherehe hizo na kukumbusha
Watanzania kuishi kwa umoja na kuwa watu wa Taifa moja lisilo na uvunjifu wa
amani.
Kutokana na
umuhimu huo, Shekhe Alhad alisema ndiyo maana sherehe hizo zikapewa kaulimbiu
ya ‘Uislamu ni amani kwa wote’ lengo likiwa kukumbusha wanaofikiri kuwa misingi
ya dini hiyo ni vurugu na kuhatarisha usalama au kujenga uadui kwa watu
wengine.
Katiba mpya
Shekhe Alhad pia alimpongeza tena Rais Kikwete kwa kufanikisha kwa kiasi
kikubwa mchakato wa Katiba mpya ambao hivi karibuni utaingia katika hatua ya
uundwaji wa Bunge Maalumu.
“Kama ni
safari basi tayari mchakato wa Katiba umevuka Nungwi na karibu unaingia
bandarini. Ni jambo la kumpongeza kwa sababu si mataifa yote yangeweza kufika
hadi hapa tulipo bila vurugu, ila sisi tumeweza na hata pale palipotokea
changamoto fulani, alikabiliana nazo,” alisema Shekhe Salum.
Alisema ni
vema Watanzania wazidi kumwombea kiongozi huyo ili akamilishe salama mchakato
huo na kumalizia muda wa uongozi na kumkabidhi mtu mwingine kuongoza Taifa.
Miongoni mwa wageni waliokuwepo ni Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi na
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Imeandikwa
na Fadhili Abdallah, Kigoma na Oscar Job, Dar
Sorce:-Habari Leo.







No comments:
Post a Comment