Serikali ya
Tanzania imetoa zaidi ya Shilingi milioni 45 kwa ajili ya ununuzi wa mashine
mpya ya kusukuma maji ikiwa ni jitihada za serikali katika kutatua tatizo la
maji katika mji wa Ngara mkoani Kagera.
Mkuu wa
wilaya ya Ngara Bw Costantine Kanyasu amemueleza waziri wa nchi ofisi ya rais,
Mahusiano na Uratibu Bw Steven Wasira kuwa mji wa Ngara umekuwa na tatizo kubwa
la maji hali inayosababisha wakazi wa mji huo kukosa maji kwa kipindi cha hadi
wiki mbili.
Amesema kuwa
tatizo hilo lilifikishwa kwa Rais wa Tanzania Dr. Jakaya Kikwete alipofanya
ziara wilayani humo hivi karibuni, hali
iliyosaidia kupatikana kwa Shilingi milioni 45 kwa ajili ya kusaidia kutatua
tatizo hilo.
Kwa upande
wake Waziri Wasira amesema kuwa maeneo mengi ya nchi yanakabiliwa na uhaba wa
maji na kwamba ili kutatua tatizo hilo kuna haja ya kuibuliwa chanzo kipya cha
maji pamoja na kuwepo kwa umeme wa uhakika kwenye maeneo yenye mitambo ya maji.
Aidha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali
yake itaongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya kusambaza huduma za umeme na maji
katika vijiji nchini kwa nia ya kuboresha maisha ya wananchi na kwamba katika
kipindi cha mwaka mmoja ujao, Serikali yake inatarajia kusambaza huduma ya maji
katika vijiji 1,449 katika hatua inayokadiriwa kuwa itawanufaisha watu wapatao
milioni saba.
Source:-Radio
Kwizera-Ngara.






No comments:
Post a Comment