Washtakiwa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) jela miaka 13. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, September 28, 2013

Washtakiwa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) jela miaka 13.


Washtakiwa wa EPA, Bahati Mahenge (kulia), Manase Mwakale (katikati) wakiwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, baada ya kuhukumiwa.Mahenge alihukumiwa kwenda jela miaka saba wakati Mwakale akihukumiwa miaka mitano.

Picha na Venance Nestory 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kwenda jela jumla ya miaka 13, washtakiwa watatu katika kesi ya wizi wa Sh1.1 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Akitoa hukumu hiyo jana kwa niaba ya wenzake, Jaji Sekela Mushi na Sam Rumanyika,Msajili Lameck Mlacha alisema mshtakiwa Bahati Mahenge atatumikia kifungo cha miaka saba jela.

Mshtakiwa Manase Makale atatumikia kifungo cha miaka mitano jela na mkewe ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo, Edda Makale atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu.

Washtakiwa wawili kwenye kesi hiyo iliyosikilizwa kwa miaka mitano, Davis Kamungu na Godfrey Mushi waliachiwa huru baada ya mahakama kuwaona hawana hatia.

Mbali na kutoa hukumu hiyo, aliamuru mshtakiwa Bahati Mahenge na Manase Makale kurejesha kiasi cha Sh1,186,534,303.27 walichodaiwa kukiiba katika akaunti EPA,iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Mlacha aliwaachia huru washtakiwa Davis Kamungu na Godfrey Mushi baada ya kuwaona hawana hatia kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka mashtaka dhidi yao. 

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro aliiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka hauna rekodi za uhalifu za washtakiwa hao.

Kimaro aliiomba mahakama kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 348(1) na cha 358(1) cha mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20 kuwaamuru washtakiwa waliotiwa hatiani kurejesha fedha walizochukua na kuisababishia Serikali hasara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad