Unyama wa Al-Shabaab wabainika ndani ya Jengo la Westgate jijini Nairobi, Kenya. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, September 28, 2013

Unyama wa Al-Shabaab wabainika ndani ya Jengo la Westgate jijini Nairobi, Kenya.




Mabaki ya jengo la Westgate lililoporomoka
baada ya shambulizi la kigaidi jijini Nairobi,
Kenya.Picha na Daily Mail.
Wiki moja baada ya shambulizi la kigaidi kwenye jengo la Westgate jijini Nairobi, Kenya, unyama wa kutisha uliofanywa na magaidi wa Al-Shabaab dhidi ya raia waliokuwa wametekwa umebainika.

Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Daily Mail la uingereza zikiwakariri wanausalama wa Kenya zinadai kuwa magaidi waliwatesa, kuwakata vidole, kuwanyofoa macho, kuwahasi wanaume na kisha kuwaning’iniza darini.

Baadhi ya mateka walinyofolewa kucha kwa koleo na maiti za watoto zilikutwa ndani ya majokofu zikiwa na zimechomwa visu.

Askari walieleza kuwa matukio hayo yalibainika muda mfupi baada ya kuingia kwenye jengo hilo lililokuwa likishikiliwa na magaidi kwa siku tatu, na baadaye kuporomoka kutokana na mashambulizi baina ya magaidi na majeshi ya Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, miili ya magaidi iliyopatikana ilikutwa imeungua na kubaki majivu, tukio lililotafsiriwa kuwa ilikuwa njia ya kuficha utambulisho wao.

Inaelezwa kuwa miili hiyo iliteketezwa na gaidi mmojawapo aliyebaki kwa ajili ya usimamizi wa kufika utambulisho wao.

Hata hivyo wapelelezi wa Kenya wanaoshirikiana na wenzao kutoka Shirika la Kijasusi la Marekani (FBI) na Police wa Kimataifa wanaendelea kuchunguza mabaki ya jengo hilo huku ikikadiriwa kuwa itachukua wiki moja kumaliza kazi hiyo.


Jengo la Westgate kabla ya Kushambuliwa.
Idadi ya vifo kuongezeka

Baada ya vifuso vya jengo hilo kufukuliwa, idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye shambulio hilo imeelezwa inaweza kuongezeka kufikia 130 kutoka 61.

Hata hivyo, hadi jana takwimu zilizotolewa na serikali ya nchi hiyo, zilikuwa zinaonyesha kuwa watu waliopoteza maisha walikuwa 67, saba kati yao wakiwa ni wanausalama.

Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, limesema kuwa watu 63 walikuwa hawajulikani walipo.

Kama watu hao watakuwa chini ya kifusi ambacho tayari kimeanza kufukuliwa, uwezekano wa vifo kuongezeka na kufikia 130 ni mkubwa.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Mail la Uingereza, idadi hiyo ikiongezeka itafanya pia raia wa Uingereza waliopoteza maisha kufika 10 kutoka sita waliothibitishwa kufa hadi sasa.

Al Shabaab wametoa taarifa kupitia mtandao wa Twitter wakisema katika tukio hilo waliuawa watu 137.


Waziri wa usalama wa ndani wa Kenya
Bw.Joseph Ole Lenk.
Bunge kuwahoji wanausalama

Viongozi wakuu wa ujasusi nchini Kenya wametakiwa kufika mbele ya Kamati ya Ulinzi ya Bunge la nchi hiyo ili kutoa maelezo kuhusu shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye jengo la Westgate.

Kamati ya bunge inataka maofisa wanaohusika na masuala ya usalama wafike mbele ya tume hiyo Jumatatu ili waweze kuwajibishwa kutokana na tukio hilo lililo sababisha vifo vya watu 67 na wengine 175 kujeruhiwa.

Uhamiaji Tanzania yakanusha

Wakati kukiwa na taarifa kuwa mwanamke anayedaiwa kupanga mashambulizi hayo, Samantha Lewthwaite alipita katika mpaka wa Namanga hapa nchini, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya amekanusha taarifa hizo.

Irovya amesema hakuna kumbukumbu za mwanamke huyo katika mipaka iliyotajwa kwa kuwa ina mitambo ya kisasa ya kuhifadhi taarifa na pia kugundua paspoti bandia.

Huyu mwanamke hajawahi kutumia mipaka hiyo kwa kuwa hakuna kumbukumbu zake, kama angepita tungeziona, na hata hiyo pasipoti yake ni bandia kwa mujibu wa Serikali ya Afrika Kusini, hivyo kwa vyovyote angekamatwa tu katika mipaka hiyo,” anasema Irovya.

Taarifa za Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol) zinasema mwanamke huyo aliwahi kupita Tanzania mwaka 2011 akitumia mipaka ya Lunga Lunga na Namanga mkoani Arusha akitumia jina la Webb Natalie Faye.

Chanzo:Mwananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad