![]() |
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba.
|
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amesema Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013
uliopitishwa na Bunge hivi karibuni unalenga kuifuta tume hiyo kabla ya
kumaliza muda wake.
Muswada huo
ambao ulipitishwa na wabunge wa CCM pamoja na Augustine Mrema wa TLP (Vunjo),
ulisusiwa na wabunge wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kutokana na kuchakachuliwa
baadhi ya vipengele huku Zanzibar ikiwa haijashirikishwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana (Septemba 26,2013) jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema miongoni
mwa vipengele vilivyofanyiwa marekebisho kwenye sheria hiyo ni kile kinachotaka
tume yake ivunjwe baada ya kuanza kwa Bunge la Katiba.
Hoja za
Warioba ndizo hizo zinazopigiwa kelele na vyama hivyo vitatu pamoja na makundi
ya asasi za kiraia huku viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM),
wakiwabeza na kudai muswada huo ulipitia taratibu zote.
Alisema
marekebisho hayo yanakwenda kinyume cha sheria mama iliyounda tume hiyo ambayo
inaweka wazi kwamba majukumu ya tume yatafika ukomo baada ya kupigwa kura ya
maoni.
Kwa mujibu
wa Jaji Warioba, uamuzi wa wabunge hao utaleta mkanganyiko endapo watashindwa
kuelewana kwenye baadhi ya vipengele, kwani hapatakuwa na mtu wa kuwafafanulia,
kwa kuwa tayari tume itakuwa imevunjwa.
“Sheria
iliyounda tume hii inasema wazi kwamba ukomo wa tume ni baada ya wajumbe wa
tume hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu kura ya maoni na mchakato wa kupiga kura
hiyo utakapokamilika.
“Wao hawaoni
sababu ya sisi kuendelea kuwapo hapa, nawaomba watafakari kipengele hicho,”
alisema Warioba aliyepata kuwa waziri mkuu wa Tanzania.
Kabla ya
kuhitimishwa kwa mkutano wa 12 wa Bunge mjini Dodoma, wabunge wa upinzani
walitoka nje wakisusia kupitishwa kwa mabadiliko ya sheria hiyo, wakidai
kufutwa kwa baadhi ya vipengele vilivyobadilishwa dakika za mwisho bila
kuwahusisha.
Kususa huko
wakati kikao kinaendelea kuliambatana na vurugu baada ya Naibu Spika, Job
Ndugai, kuwataka askari wa Bunge kumtoa nje Kiongozi wa Kambi ya Upinzani,
Freeman Mbowe, jambo lililowafanya wabunge wa vyama hivyo vitatu kutoka wote.
Pamoja na
madai hayo, wabunge hao walilalamikia utendaji wa Kamati ya Bunge
inayoshughulikia Katiba na Sheria chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Viti Maalumu,
Pindi Chana, kwa kubadili vipengele hivyo kabla ya kuupitisha bungeni.
Baada ya
wabunge wa upinzani kususa, wabunge wachache wa CCM waliokuwapo ukumbini hapo
na Mrema, walipitisha mabadiliko hayo na kuyapeleka kwa rais ili asaini na
kuifanya kuwa sheria.
Nje ya Bunge
Moto
uliowashwa nje ya Bunge na viongozi wa upinzani pamoja na makundi ya asasi za
kiraia umebadili upepo kwani kelele za kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutousaini
muswada huo zimezidi kuongezeka.
Ni katika hatua
hiyo, mawaziri kadhaa, William Lukuvi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), Stephen Wasira na Mathias Chikawe wa Katiba na Sheria, wamekuwa
wakiendelea kuwabeza wapinzani.
Hivi
karibuni Waziri Chikawe alifikia hatua ya kumtisha Rais Kikwete akisema kuwa
endapo hatausaini muswada huo kuwa sheria atakuwa ametangaza mgogoro na Bunge.
Pia Wasira
naye amenukuriwa akisema kuwa wanaopinga muswada huo usisainiwe lazima wampe
rais sababu za kutofanya hivyo, kwa vile hana, na kwamba milango ya Ikulu kwa
wapinzani hao kujadiliana na mkuu wa nchi imefungwa.
Matamshi
hayo ndiyo yamewaleta pamoja viongozi wa vyama hivyo na makundi mengine
wakizunguka kwa wananchi kuwaeleza karoso zilizomo kwenye muswada huo ambao CCM
inataka kutumia turufu hiyo kuhodhi mchakato wa Katiba mpya.
Angalizo la
Warioba
Mwenyekiti
huyo aliwataka wanasiasa kuacha malumbano katika mchakato wa upatikanaji wa
Katiba mpya, huku akikanusha uvumi kwamba baadhi ya wajumbe wa tume hiyo
wametishia kujiuzulu.
Badala yake
aliwataka waketi pamoja na kukubaliana kuhusu vipengele wanavyotofautiana
kwenye rasimu hiyo, kisha kuwaeleza wananchi manufaa ya kuwa na Katiba ya wote.
“Huu si
wakati wa Tanzania kutengana, wanasiasa wanapaswa kutumia fursa walizonazo
kukaa pamoja na kushirikiana ili tupate Katiba bora, hatuwezi kupata Katiba kwa
maandamano, mikutano na mivutano baina ya vyama vya siasa,” alisema.
Kwa mujibu
wa jaji huyo, kilichopo kwenye rasimu hiyo ni maoni ya wananchi, hivyo hakuna
haja ya kubadili, bali kuboresha ili kila Mtanzania anufaike na uwepo wa Katiba
hiyo.
Alifafanua
kuwa kuna baadhi ya wajumbe wa mabaraza walidiriki kuwakashifu wajumbe wa tume
yake, hasa kutokana na wanasiasa kutoa matamshi ya kuwalenga wajumbe hao wa
tume.
“Hilo
limetusikitisha, matamshi hayo yalitolewa kwa lengo la kuwadhalilisha wajumbe
wa tume na kuishushia thamani kazi kubwa wanayoifanya ndani ya tume,” alisema.
Jaji Warioba
alisema pamoja na changamoto hizo, tume ilifanikiwa kukamilisha mchakato huo
ambapo kwa kupitia mikutano 179 ambayo ilihudhuriwa na wajumbe 19,337 wa
mabaraza ya Katiba walipata maoni.
Mbali na
hatua hiyo, Jaji Warioba alisema tume imepokea maoni kutoka kwa makundi, asasi
na taasisi mbalimbali 600 kuhusiana na rasimu ya Katiba mpya.
Alisema
baada ya kukusanya maoni hayo, tume inatarajia kuanza mchakato wa kuchambua ili
kuandaa ripoti itakayokuwa na maboresho na kuikabidhi kwa rais kwa ajili ya
kuendelea kwa mchakato mwingine.
“Tumewahoji
wawakilishi wa wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania Bara na Visiwani,
zaidi ya vikundi 176 vyenye uwakilishi wa watu tofauti tulikusanya maoni yao.
“Naamini
Watanzania wanataka Katiba inayoheshimu utu wa mtu, umoja na kuvumiliana,”
alisisitiza Jaji Warioba.
Source:-Tanzania Daima.






No comments:
Post a Comment