Serikali
kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imempongeza Mzee
Muhidini Gurumo kwa mchango wake uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini
pamoja na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
Akiwasilisha barua ya Serikali ya kutambua mchango wa nguli huyo juzi
nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Lilly
Beleko amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wake katika
muziki wa Dansi hapa nchini.
‘Serikali inathamini mchango wako katika Muziki hapa nchini na
itaendelea kuzienzi kazi hizo na inakupongeza kwa kazi nzuri ulioifanya ya
kuelimisha, kuhamasisha na kuburudisha jamii’. Amesema Bibi. Beleko.
Naye Rais wa Shirikisho la Muziki nchini, Bw. Addo Mwasongwe, amesema
kuwa Shirikisho linampongeza kwa kazi zake nzuri na litaendelea kumtumia katika
kazi za muziki ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri katika tasnia hiyo.
Nguli huyo wa muziki wa dansi nchini katika enzi zake za uimbaji
ametunga nyimbo za kuelimisha jamii kufanya kazi kwa bidii, kudumisha usawa,
amani na kuwakumbusha wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea watoto katika
maadili mema.
Mzee Gurumo ambaye ameanza kazi ya muziki mnamo miaka ya 1960 na kustaafu
kazi hiyo mwaka huu amesema kuwa anaishukuru Serikali kwa kutambua kazi yake na
amefarijika kwa kukabidhiwa barua ya kumtambua na kumpongeza kwa kustaafu kazi
hiyo.







No comments:
Post a Comment