Hatimaye Nchi za
Rwanda na Tanzania zimefikia mwafaka kuhusu ushuru wa barabara, ambapo nchi
hizo zimeshusha viwango vya kodi na sasa kutoza dola 152 za Marekani, bila
kujali umbali.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu akiwa Kampala, Uganda jana,
baada ya kumaliza mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango wa Rwanda, Claver
Gatete, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, alisema mwafaka umefikiwa.
“Tumefikia
mwafaka kuhusu suala hili, na wenzetu wamekubali kushusha kodi yao mpya
waliyokuwa wakitutoza Tanzania pekee kutoka dola 500 hadi 152 na sisi pia
tumeshusha kutoka dola 216 hadi 152,” alisema Mgimwa.
Awali
Tanzania ilikuwa inatoza dola 16 kwa kilometa 100 kwa magari yanayosafirisha
mizigokutoka bandari ya Dar es Salaam, kwenda nchi zisizo na bahari.
Alisema
Tanzania imebidi iridhie kushusha kiwango hicho kutokana na ukweli kuwa endapo
Rwanda ingeendelea kutoza kiwango hicho kipya, wafanyabiashara wa Tanzania ndio
wangeathirika zaidi kutokana na wingi wa magari ya mizigo yanayokwenda Kigali,
kuliko yanayotoka Kigali kwenda Dar es Salaam.
“Kwa hesabu
za haraka malori ya mizigo yanayotoka Tanzania kwenda Kigali kwa siku,
yanafikia 200 hadi 300, wakati yanayotoka Kigali kwenda Tanzania ni 20 hadi
30,” alisisitiza.
Awali Tanzania
ilikuwa ikitoza ushuru wa dola 16 kwa lori kwa kilometa 100 na Rwanda ikaamua
kutoza ushuru huo huo. Hata hivyo, baada ya muda Rwanda ilibaini kuwa haipati
faida kama Tanzania.
Tanzania kwa
ushuru huo, kutoka Dar es Salaam hadi Rusumo mpakani mwa Tanzania na Rwanda,
umbali wa kilometa 1,389, ilikuwa ikipata dola 216, wakati Rwanda kwa ushuru
huo, kutoka Rusumo hadi Kigali umbali wa kilometa 139, ilijikuta ikiambulia
dola 22.24 tu kwa gari.
Kutokana na
mazingira yaliyoonekana ya kukosa uwiano sawa na Tanzania, yaliyotokana na
udogo wa nchi husika, Rwanda ilipandisha ushuru na kuwa dola 152 bila kujali
umbali, kwa kuwa kijiografia haukuwa na msaada kwao.
Hata hivyo,
Tanzania haikulalamika kwa ongezeko hilo la ushuru na iliendelea kufanya
biashara na Rwanda kama inavyofanya na nchi zingine zinazopitisha mizigo yao
Dar es Salaam.
Juzi
alipozungumza na gazeti hili (Habari Leo) kuhusu kikao hicho cha kujadili mustakabali wa
kodi hiyo ya barabara Waziri Gatete, alikiri kuwa Serikali yake iko tayari
kupunguza kodi endapo kutakuwa na ushuru linganifu.
Alisema nchi
yake kwa takribani miaka mitatu sasa imekuwa ikilalamikia utofauti wa kodi za
barabara baina yake na Tanzania ambapo kodi inayotozwa Tanzania ni kubwa kuliko
ya Rwanda, jambo lilisababisha wapandishe kiwango hicho ili kupata ulinganifu.







No comments:
Post a Comment