Rais Jakaya
Kikwete amesema wale wote wanaombeza kuhusu utendaji wake, wataona aibu
atakapomaliza muhula wake 2015 huku akiwananga baadhi ya wanaCCM kwa kushindwa
kuyaelezea mafanikio ya Serikali chini ya chama hicho.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita
unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), Rais Kikwete alisema:
"Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza
kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu.
"Nataka
waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili
kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015
umeme utakuwa umesambaa nchi nzima.
"Serikali
yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme katika vijiji vingi nchini...Tumejenga
mtandao wa barabara kwa sasa, hali yetu ya barabara ni bora Afrika Mashariki,
tuliahidi meli Bukoba naomba niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli
mbili.
"La
umeme leo nazindua nataka kuwaeleza walionibeza waje waone sasa ahadi
zangu...hayo yote niliyasema kwenye ahadi zangu 2010," alieleza Kikwete
huku akishangiliwa na wananchi.
Mradi huo
umegharimu Dola za Marekani 15.54 milioni sawa na Sh24.87 bilioni kwa Mwanza na
Geita pekee, fedha ambazo ni asilimia 25 ya Dola za Marekani 62.6 milioni sawa
na Sh103.24 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 225 ya
upanuzi wa njia za kusambazia umeme katika mikoa kumi nchini.
Rais Kikwete
alisema Serikali inajipanga kusambaza umeme na kufikiwa vijiji vyote na
kubainisha kuwa mpango huo unakwenda sambamba na uanzishaji wa vyanzo vya umeme
ili viweze kuzalisha megawati 3,000 ifikapo 2015 na kwamba ziada itauzwa nje ya
nchi.
Septemba 2
mwaka huu, Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ilitangaza kuanza
kwa awamu ya pili ya usambazaji wa umeme vijijini, mpango ambao utagharimu
Sh881 bilioni na kukamilika Juni 2015.
Katika
utekelezaji wa mradi huo, huduma za jamii zitakazopewa kipaumbele katika
kuunganishiwa umeme ni shule, zahanati, misikiti, makanisa na visima vya maji.
Mpango huo
unatarajiwa kuinufaisha mikoa 24 ya Tanzania Bara, huku wateja 250,000 wa awali
wakiunganishwa pamoja na kuhusisha kazi ya usambazaji umeme kwenye makao makuu
ya wilaya 13 zisizokuwa na umeme.
Mwenyekiti
wa Bodi ya REA, Balozi Ami Mpungwe alisema tayari mikoa 14 imepata makandarasi
na ujenzi wa vituo sita vya usambazaji umeme, wakati mchakato wa kuwapata
wajenzi katika mikoa 13 iliyokosa wakandarasi awali, unaendelea.
Awananga
viongozi wa CCM
Rais Kikwete
amewananga baadhi ya viongozi wa chama chake na kusema kuwa ni dhaifu katika
uongozi kwani wameshindwa kueleza mafanikio ya Serikali chini ya CCM.
"Baadhi
ya viongozi wa CCM pamoja na wanachama wamezubaa kiasi cha kushindwa
kuzungumzia mafanikio ya Serikali inayoundwa na CCM, lakini wamekuwa mahodari
wa kujadili wanapobezwa na wapinzani.
"Tatizo
lenu CCM mmezubaa, huo ndiyo udhaifu wenu mkubwa, kupata maji ya bomba ni hatua
kubwa na maendeleo, lakini viongozi wa CCM nyie mmezubaa na ni dhaifu, hamuwezi
kueleza mafanikio haya, lazima niliseme hili na ujumbe uwafikie," alieleza
na kuongeza.
"Kwa
nini mnasubiri mimi nifike hapa ndipo mje kwenye miradi kama hii, mimi nikija
huku siji nikiwa nimebeba miradi hii mgongoni, kwa nini mmekuwa dhaifu wa
kuyasema haya na badala yake mmekuwa hodari wa kushupalia dosari zinazosemwa na
wapinzani na kuacha mazuri haya?" alisema Kikwete.
Alisema Tanzania ni
nchi kubwa kuliko nchi zingine za Afrika Mashariki, lakini ina mtandao mkubwa
wa barabara kuliko nchi kama Kenya, lakini akawalaumu watu wanaoisifia nchi
hiyo jirani na kubeza mafanikio ya Serikali yake.
Azungumzia
Elimu
Wakati
huohuo, Rais Kikwete amewaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha kila sekondari ya
kata inakuwa na maabara zenye vifaa viliyokamilika na kwamba atakayeshindwa
kufanya hivyo atamwajibisha.
Alisema
vijana lazima wasome katika shule zenye vifaa na kusisitiza kuwa, kwa sasa
Serikali imekamilisha mpango wa kusambaza walimu ili kukabiliana na uhaba
uliopo.
Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali inajiandaa kukamilisha mpango wa
Tehama kwa shule zote nchini kutokana na kuwapo kwa mtandao wa mawasiliano
kupitia mkongo wa taifa.
Chanzo:Mwananchi






No comments:
Post a Comment