![]() |
Naibu rais
wa Kenya, William Ruto.
|
Rais wa
Kenya, Uhuru Kenyatta amesisitiza kuwa haitawezekana yeye na naibu wake William
Ruto kuhudhuria kwa pamoja kwenye mahakama ya ICC kujibu mashtaka
yanayowakabili kwakuwa katiba ya nchi hairuhusu.
Rais
Kenyatta ametoa kauli hiyo hapo jana (Septemba 09,2013) na kudai kuwa kamwe haitatokea yeye na
naibu wake Ruto wahudhurie kwa pamoja vikao vya kesi mjini The Hague kwakuwa
kufanya hivyo ni kuisaliti nchi na kitendo hicho hakikubaliki.
Kauli hiyo
ambayo ni ya kwanza kwa Rais Kenyatta kukitoa toka jopo la mawakili wake
washindwe kurejesha kesi hizo nchini Kenya ama Tanzania, alitoa kauli hiyo kwa
jazba akisisitiza kuwa yeye ndiye Rais wa Kenya na kwamba haiwezekani wote
wawili wakawa mjini The Hague.
Kauli ya
Rais Kenyatta imekosolewa pakubwa na wataalamu wa masuala ya sheria wakidai
kuwa inalenga kutaka kukwepa mkono wa sheria kwa kuwa jinsi kesi itakavyokuwa
ikiendeshwa kuna wakati huenda wote wawili yeye na naibu wake wakalazimika
kuwepo mjini The Hague.
Kauli ya
Kenyatta inakuja wakati huu ambapo naibu wa Rais William Ruto na mwandishi wa
habari Joshua Arap San'g wakiwa wamewasili mjini The hague tayari kuanza
kusikiliza kesi yao ambayo itaanza kuunguruma siku ya Jumanne.
Mwandishi wa
habari Arap San'g mwenyewe alishawasili toka siku ya Jumapili huku naibu wa
rais William Ruto akitarajiwa kuwasili hii leo mjini The Hague na kupokelewa na
balozi wa Kenya nchini Uholanzi.
Wabunge
kadhaa toka muungano wa Jubilee nao wamewasili mjini The Hague kuhudhuria vikao
hivyo vinavyoanza hapo kesho, kwenye kesi ambayo inatarajiwa kuchukua mwezi
mzima.
Kesi hiyo
inaanza wakati huu ambapo wabunge nchini Kenya wamepitisha muswada wa sheria wa
kutaka nchi yao kujiondoa kwenye mkataba wa Roma unaoitambua mahakama ya
uhalifu wa kivita ya ICCm hatua ambayo imezua mjadala mkubwa nchini Kenya.
Ruto
anatuhumiwa na mahakama ya ICC kwa kuhusika kwake na vurugu za uchaguzi wa
mwaka 2007-2008 vurugu ambazo watu zaidi ya elfu moja (1000) walipoteza maisha
na wengine zaidi ya elfu sitini wakikosa makazi.
Wachambuzi
wa mambo wanaona kuwa kesi za Kenya ni moja kati ya kesi ngumu zaidi kuwahi
kushughulikiwa na mahakama ya ICC kwakuwa mashahidi wengi muhimu kwenye kesi
hiyo wamejiondoa huku baadhi ya mashtaka yakiondolewa na jopo la majaji hali
ambayo wataalamu wa sheria wanahoji utayari wa ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu
wa ICC.
Hata hivyo
licha ya pigo ambalo mwendesha mashtaka mpya wa mahakama hiyo Mgambia Fatou
Bensouda kukabiliwa nazo ameahidi kuendelea na kesi hizo na kwamba ana ushahidi
wa kutosha kudhibitisha mashtaka dhidi ya viongozi hao wawili.
Mahakama ya
ICC imekuwa ikikosolewa na viongozi wa bara la Afrika kuwa inaendeshwa kisiasa
kwakuwa kesi nyingi zinawakabili viongozi wa Afrika, jambo ambalo mahakama hiyo
imekanusha.
Hivi
karibuni mataifa ya Afrika yalipiga kura na kupitisha mchakato wa mataifa hayo
kuanza kujiondoa kwenye mkataba wa Roma unaotambua mahakama ya ICC hatua ambayo
ilitokana na shinikizo la rais wa Uganda Yoweri Museveni.






No comments:
Post a Comment