![]() |
Eneo la
jiko.
|
![]() |
| ...Nyumba za wajukuu pamoja na wageni zikiendelea kujengwa.… |
![]() |
Kibao kinachoonesha taasisi ya Marehemu
Kulola iliyopo katika nyumba yake.
|
![]() |
…Sehemu ya mji wa Chanika, jirani na nyumbani
kwa Askofu Kulola.
|
Askofu
Kulola anajulikana na wengi kama mtu aliye na nia ya dhati kutangaza neno la
Mungu, kutokana na kile kinachoonekana wazi kwamba hakujilimbikizia mali kama
ambavyo tunaona baadhi ya watumishi wa Mungu siku hizi wanavyomiliki majumba,
benki na hata magari ya milioni ya shilingi.
Hali halisi
Kwa namna
inavyoonekana nchini, ni kama kuna kundi kubwa la watumishi wanaohubiri kwa
lengo la kushibisha matumbo yao zaidi; Hawana mpango thabiti wa kusaidia yatima
wala maskini, badala yake waumini ndio wanaonyonywa kwa kutoa zaka na sadaka
ambazo baadhi yake hata matumizi yake yamekuwa yakizua maswali.
Utumishi wa
Mungu na mali
“Hakuna
shaka kwamba kama kila nyumba ya ibada Tanzania ingekuwa na mpango thabiti wa
kusaidia watu maskini, yatima na watu wengine wenye hali ngumu, hali ya maisha
ingekuwa nzuri zaidi kwa wengi.
Lakini wapi, baadhi ya watumishi wako ‘bize’
kujaza matumbo, wanaendesha magari ya kifahari yenye thamani ya mamilioni ya
shilingi badala ya kutumia fedha hizo kutangaza neno la Mungu au kusaidia
wasiojiweza,” anasema Charles Mtanga, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam.
Mtanga
anawashauri viongozi wa nyumba za ibada kuwa na mkakati wa kusaidia yatima na
watu wengine wasio na uwezo, huku wakiendelea kutangaza neno la Mungu, ili wote
waweze kuufurahia ulimwengu.
Utanuzi wa
huduma
Kwa mujibu
wa Askofu wa EAGT Sengerema,
Joshua Wawa, Askofu Kulola alizaliwa Juni 2, 1928 katika Kijiji cha Nyahonge
wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ameacha mjane, watoto 10, wajukuu 44 na vitukuu
16.
Katika uhai
wake, Askofu Kulola alifungua makanisa 4,600 ya EAGT ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Zambia, Malawi, Rwanda na
Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) na ameacha wosia kwamba makanisa
yafunguliwe kadiri inavyowezekana.
Hata hivyo,
licha ya kuwa na wingi wote huo wa makanisa, Askofu Kulola anamiliki nyumba
moja iliyoko mkoani Mwanza aliyojengewa na waumini.
Askofu Moses
Kulola
“Yoooh!
Unapenda niseme?” hicho ndicho kilikuwa ‘kibwagizo’ cha Askofu Moses Kulola wakati wa uhai wake hasa
alipokuwa akihubiri mikutano ya injili.
Askofu
Kulola alifariki Agosti, 29 mwaka huu
katika Hospitali ya AMI (African Medical Investments) iliyopo Slipway
jijini Dar es Salaam.
Mikakati
mingine
Askofu huyo
mkuu wa EAGT, ameelezewa kuwa amewahi
kwenda Ikulu mara kadhaa kuombea nchi kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya
Kikwete alishuhudia hayo wakati wa maziko yake yaliyofanyika Bugando, jijini
Mwanza kwamba kwa namna inavyoonekana Askofu Kulola alikuwa ana maanisha
kuifanya kazi ya Mungu.
Kufungwa na
kunusurika kuuawa
Askofu
Kulola amewahi kufungwa gerezani kwa ajili ya kuhubiri injili, pia amewahi
kunusurika kifo katika ajali. Rais Kikwete anamzungumzia kama mchungaji
aliyekuwa mkweli na aliyeutumia muda wake kusaidia wote bila kujali imani zao
za dini.
Maisha yake
Katika
maisha yake, Kulola alisoma Shule ya Msingi ya Ligsha Sukuma, mwaka 1939
baadaye akajiunga na taasisi ya usanifu mwaka 1949. Alibatizwa mwaka 1950
katika Kanisa la AIC Makongoro. Alimwoa Elizabeth.
Mwaka 1959
alianza kufanya kazi serikalini, wakati huo huo akihubiri injili katika miji na
vijiji. Utumishi wake serikalini ulifika mwisho mwaka 1962, aliamua kujitolea
moja kwa moja katika kazi ya kutangaza neno la Mungu.
Mwaka 1964
alijiunga na chuo cha theolojia na kuhitimu 1966. Aliendelea na masomo ya
theolojia ndani na nje ya nchi.
Alihudumu
kama mchungaji katika Kanisa la AIC kabla ya kuhamia madhehebu ya Pentekoste
mwaka 1961-1962 na alifanya kazi katika Kanisa la TAG 1966 mpaka 1991 alipoamua
kuanzisha Kanisa la Evangelistic Assemblies God (EAGT) baada ya kutokea mgogoro
wa kiuongozi.
Kisa cha
Askofu Kulola kuanzisha kanisa lake
Katika
kitabu cha Historia ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God, mwandishi Dk
Jotham Mwakimage anasimulia kiini cha mtafuruku uliolikumba kanisa hilo miaka
ya 1980 kiasi cha kusababisha mgawanyiko mkubwa. Anasema kulikuwa na mikutano
mikuu ya kanisa hilo kati ya mwaka 1980 na 1982.
“Mkutano
mkuu wa mwaka 1980 ulikuwa wa kipekee kwa wale waliohudhuria, kwani ulitawaliwa
na ujumbe wa kinabii zaidi, ulifanyika kwenye jengo la udongo lililoko Chuo cha
Biblia Dodoma,” kinasema kitabu hicho na kuongeza:
“Kwa mtazamo
wangu, mkutano huu haukuonekana kama mkutano wa shughuli za kikanisa, bali kama
kusanyiko la uamsho wa kiroho katika kuwatia nguvu wachungaji wa TAG kwa ajili
ya huduma za kichungaji.”
Dk Mwakimage
anaendelea kusema kuwa kulikuwa pia na mkutano wa aina hiyo pia mwaka 1982. Lengo
la mkutano huo uliofanyika pia Dodoma lilikuwa ni kuchagua viongozi wakuu wa
kanisa hilo na hapo ndipo kanisa lilipopasuka.
“Sababu ya
mgawanyiko ilitokana na ule mtafaruku uliokuwa kati ya wainjilisti wawili
mashuhuri waliokuwa na mvuto ambao ni Emmanuel Lazaro aliyekuwa Askofu Mkuu wa
TAG na Moses Kulola. Ushawishi wa viongozi hao kiroho ulikuwa mkubwa na uligusa
watu wengi,” anasimulia.
Anasema
ushawishi huo uliwagusa siyo waumini tu wa kanisa hilo, bali hata wamisionari
waliolisaidia kanisa hilo.
“Viongozi
hawa hawakukubaliana katika mambo ya msingi na mgongano wao ukawagusa watu
wengi na matokeo yake hayakuweza kuepukika.”
“Kabla ya
mwaka 1982, sheria ndogo ya uhamisho iliongezwa katika Katiba ya TAG. Katika
mwaka huo, uongozi wa TAG chini ya Askofu Lazaro ulitumia mamlaka ya kikatiba
kuwahamisha baadhi ya wachungaji muhimu ndani ya mfumo wa huduma ya kanisa
hilo,”
“Uhamisho
huo haukueleweka vizuri… hasa uhamisho wa Mchungaji Calist Masalu wa Kanisa la
Temeke ambalo lilikuwa ndiyo kituo kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya
shughuli za Moses Kulola.”
“Wachungaji,
washirika na hata wamisionari hawakuelewa sababu za kuwahamisha wachungaji hao,
hivyo wakatafsiri kwamba kumhamisha Mchungaji Masalu kulilenga kuharibu huduma
ya uinjilisti za Kulola.
Kwa sababu hiyo Mchungaji Masalu akagoma kuhama,
akisubiri uamuzi wa mkutano mkuu”. Dk Mwakimage aliyekuwa mjumbe katika mkutano
huo uliotawaliwa na minong’ono ya uhamisho wa wachungaji anasema uchaguzi
ulifanyika na Lazaro kuchaguliwa kuwa askofu mkuu na Kulola kuwa msaidizi wake.
Hata hivyo mambo yakazuka tena.
“Siku
iliyofuata wakati wa kipindi cha shughuli, suala la uhamisho wa Mchungaji
Masalu likajitokeza tena na hoja kama sharti la Kulola kuikubali nafasi yake
hiyo ikaibuka. Kulola alinukuliwa akisema, “Kama uhamisho wa Mchungaji Calist
Masalu kwenda Bugando Mwanza hautatangazwa, kuondolewa au kufutwa, basi siko
tayari kupokea wadhifa mlionichagua.”
“Huo ndiyo
ulikuwa msimamo wa Kulola,” anasema Dk Mwakimage na kuongeza:
“Baada ya
hapo Askofu Mkuu Lazaro akasimama kujibu hoja akimpinga Kulola akisema;
“Uhamisho wa Mchungaji Masalu utabakia na kamwe hautafutwa wala kubadilishwa”.
Ni kutokana
na kauli hizi mbili zilizosigana ikawa ndiyo sababu ya mgawanyiko kutokea.
Mgawanyiko huo kwanza ulizaa chuki na kashfa endelevu kati ya makundi hayo
mawili hadi leo. Lakini kwa upande mwingine umeyaimarisha makundi hayo, kwani
hadi sasa ni madhehebu yaliyokua.
TAG bado
yaidai EAGT
Akizungumzia
uhusiano kati ya TAG na EAGT hivi karibuni Askofu Mkuu wa TAG, Dk Barnabas
Mtokambali, licha ya kusema kuwa makanisa hayo yana uhusiano mzuri, anaongeza
kuwa bado kanisa lake linaidai mali zake EAGT.
Anaongeza kuwa mwaka 1991 kabla
Askofu Kulola hajasajili kanisa lake, Serikali ilimpa sharti la kurejesha mali
za TAG ili apate usajili, ndipo alipoweka ahadi ya kurudisha jambo ambalo
hakulifanya hadi anafariki.
EAGT
haidaiwi
Hata hivyo
madai hayo yamekanushwa na Katibu Mkuu wa EAGT, Brown Mwakipesile akisema
mgogoro uliopo ni wa kikatiba:
“Hakuna mali
yoyote tunayodaiwa na TAG, tatizo letu lilikuwa ni la kikatiba tu,” anasema
Mwakipesile.
Kanisa la EAGT chini ya Askofu Kulola limeendelea kukua kwa kasi.
Tofauti ya uongozi kati ya makanisa hayo mawili ni kwamba, EAGT imekuwa chini
ya Askofu Kulola hadi mauti yanamkuta huku TAG ikibadilisha uongozi, kutoka
Askofu Lazaro kuja kwa Ranwel Mwenisongole hadi askofu wa sasa Dk Barnabas
Mtokambali.
Chanzo:Mwananchi.



.jpg)







No comments:
Post a Comment