Mti wenye
matunda, ndio unaopigwa mawe. Wahenga waliona mbali walipotunga usemi huu. Sina
shaka kuwa hakuna mtu anayepoteza muda wake kumhangaika mtu kwa maneno ya hapa
na pale kama hakuna kitu kinachomuumiza.
Wiki chache
zilizopita mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond’ alikumbana na magumu mengi, hata
hivyo alionekana kuwa imara kwa kutotetereka. Nyota huyu aliendelea kufanya
kazi kwa bidii na kila Mtanzania ameiona na sasa mambo ni tofauti.
Haikuwa
rahisi kwa mtu kufikiria kama ipo siku atatokea msanii wa hapa nchini kwenda
kufanya matengenezo ya video yenye thamani kubwa kama alivyofanya mwanamuziki
huyu. Mengi yamezungumzwa, lakini hatimaye kazi ya mtu ndiyo inayomuuza yeye na
sanaa yake.
Diamond
ambaye bado anatumikia mkataba na Coca Cola, sasa amesaini mkataba na Kampuni
ya Vodacom na RBT (Ring Back Tone). Kama haitoshi, ameanzisha Shindano la Dansi
ya Ngololo, ambayo pia ina sehemu utakayoweza kuchati na mwanamuziki huyo ijulikanayo
kama Vodacom Ngololo Chart.
Licha ya
hayo, ameweza kupata fursa nyingi zilizomwezesha kutengeneza fedha ya chapchap.
Haya yote ni matunda ya kujituma, kujua kile unachokifanya, kunyenyekea na
kuangalia soko la muziki pamoja na ubunifu vilivyomwezesha kufika alipo.
Katika
kumbukumbu zangu miaka minne iliyopita nilipokuwa nikimhoji msanii huyu, wakati
huo akiwa ndiyo kinda katika muziki wa kizazi kipya, alikuwa ni mtu
aliyeonyesha umakini wa hali ya juu, hata alipokuwa akinijibu niliyomuuliza.
Hata hivyo,
ahadi yake kuhusu matarajio ya baadaye ilikuwa ni kuwa mwanamuziki mkubwa
Tanzania na barani Afrika, ndoto alizoanza kutimiza hivi sasa.
Mafanikio ya
msanii huyu ni vyema yakawa chachu kwa wasanii wengine nchini badala ya kuwa
mwanzo wa chuki na masimango kwake, ambaye anajitahidi kuutangaza muziki wa
Tanzania kimataifa.
Kuna kila
sababu ya kuwafanya wasanii hapa nchini kuiga mfano wa mwanamuziki huyu kwa
kufanya kazi kwa bidii na kujituma, ili kuweza kufikia hatua hiyo. Hakuna shaka
kuwa wapo walioanza muziki kabla yake, lakini hawakuweza kufikia mafanikio
hayo.
Idadi kubwa
ya wasanii wamekuwa ni wapuuzaji wa mambo ya msingi na wenye majivuno hasa
mbele ya vyombo vya habari.
Kwa maoni
yangu moja ya siri zilizompa mafanikio Diamond ni jitihada zake za kumheshimu
mkubwa na mdogo, vyombo vya habari, watayarishaji wa kazi zake na mashabiki
wake pia, jambo ambalo wengi wa wasanii limewakwamisha.
![]() |
| Naseeb Abdul ‘Diamond’. |
Licha ya
hayo, Diamond aliamua kuwa na wasimamizi rasmi wa kazi zake, tofauti na wasanii
wengine walioamua kuwa watasimamia kazi zao wao wenyewe huku wenye uwezo huo
wakiwa ni wachache hivyo wengi kushindwa kufikia malengo yao kutokana na sababu
nilizozitaja hapo juu.
Ulevi wa
kupindukia imekuwa sababu mojawapo iliyowafanya wasanii wengi washindwe kufikia
mafanikio waliyojiwekea. Utakuta msanii hana meneja, mlevi na mtu asiye na
ratiba maalumu. Hii ni sababu ya wengi kushindwa kwenda na wakati hata kutimiza
majukumu ya kazi zao ili kufanikiwa.
Kuna idadi
kubwa ya wasanii walisimama kidete na kusema hawataki watu wa kusimamia kazi
zao, idadi kubwa wamepotea maana walikuwa ni watu wa kujiamulia mambo
wanavyotaka wao.
Jiulize
tangu uanze muziki umefikia mafanikio gani? Tuache kulalama kwamba kuna wizi,
kuna kuibiana nyimbo, jiulize umefanya nini katika kazi ya mikono yako
kuhakikisha unafikia nafasi ya juu?
Wengi wanatengeneza
kazi zenye kiwango cha chini cha ubora unamkuta msanii ana wimbo mzuri lakini
anaamua kutengeneza video ya wimbo huo kwa gharama ndogo sana kiasi kwamba
inakuwa haina ubora wa kutosha.
Bado msanii huyuhuyu anatarajia kupata
mafanikio kimataifa inawezekana vipi?
Nijuavyo
mimi wasanii walioiva na wanaoujua muziki wapo makini na huhitaji kufanya kazi
yenye ubora kwa kulenga soko la kimataifa.
Ni kweli
kwamba unaweza kufanya muziki wa gharama ya chini lakini ukazingatia kanuni na
kuwekeza nguvu kubwa katika kile unachokifanya ni lazima ufanikiwe bila shaka.
Wasanii
mnahitaji kubadilika ili kwenda sambamba na mabadiliko yaliyopo hivi sasa
katika sanaa ya muziki. Ni vyema kufanya kazi kubwa hata kama itakugharimu
kiasi kikubwa cha pesa kwani itakuwa ni sehemu ya ubora wa kazi yako, ndivyo
hivyo itakavyoweza kukulipa vizuri.
Source:
Mwananchi .







No comments:
Post a Comment