Maoni
ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu Muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba wa 2013 yanadaiwa kuwa yalibadilishwa dakika za mwisho na
kwamba suala hilo ndicho kiini cha vurugu zilizotokea bungeni mjini Dodoma
juzi.
Gazeti
hili limefanikiwa kuona nakala inayodaiwa kuwa ni maoni ya awali ya kamati hiyo
ambayo yalikuwa na mapendekezo yanayotaka kuwapo kwa marekebisho kadhaa kwenye
muswada huo, tofauti na yale yaliyowasilishwa bungeni juzi na Mwenyekiti wa
Kamati, Pindi Chana.
Jumatano
na Alhamisi wiki hii kulikuwa na mvutano mkubwa bungeni kiasi cha wabunge wa
upinzani kutoka vyama vitatu vya NCCR -Mageuzi, Chadema na CUF kuungana na
kususia mjadala kuhusu muswada huo.
Imedokezwa
kuwa mvutano mkali kuhusu muswada huo ulianza ndani ya kamati hiyo wakati
wajumbe wake ambao ni wabunge wa CCM walipotumia wingi wao kubadili maoni ya
awali na kuweka maoni mapya, hatua ambayo inadaiwa kuwa ilikuwa na msukumo wa
Serikali nyuma yake.
Ndani
ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, wabunge wa upinzani ambao kwa
idadi yao ni wachache walishindwa kuzuia mabadiliko hayo ya “lala salama”
yanayodaiwa kuwa yaliwekwa Septemba 2, mwaka huu, hivyo waliazimia kuhamasisha
wabunge wote wa upinzani kupinga marekebisho hayo kutokana na sababu kuu mbili.
Sababu
hizo ni kutofanyika kwa mikutano ya wazi kwa umma (public hearing) upande wa
Zanzibar na hatua ya kuwapo kwa mapendekezo ya Rais kurundikiwa madaraka
makubwa ya uteuzi wa wabunge kutoka asasi za kijamii watakaoingia katika Bunge
la Katiba.
Habari
zinasema wakati fulani Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alitembelea kamati hiyo
wakati ikiedelea na vikao vyake na kukuta mvutano mkali kuhusu suala la
marekebisho ya sheria ya sheria hiyo na alishauri kwamba pale ambapo hawataweza
kuelewana basi wasubiri uamuzi ndani ya Bunge.
Jana
gazeti hili lilimtafuta Chana kupitia simu yake ya mkononi na baada ya
kumweleza kuhusu madai hayo alisema: “Tafadhali sana kwa sasa niko kwenye
kikao, kwanza simu yako nimeipokea kwa heshima tu, tutafutane wakati mwingine”.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alikiri kwamba kulikuwa na mapendekezo ya
kuongeza idadi ya wabunge na namna ya kuwapata, lakini Serikali iliyakataa
katika hatua ya majadiliano kabla ya suala hilo kufikishwa bungeni.
Tofauti
ya maoni
Nakala
ya taarifa ya awali ilipendekezwa kuwa katika kuteua wajumbe 166 wa Bunge la
Katiba, Rais azingatie kikamilifu mtiririko wa mapendekezo ya kila kundi
lililoainishwa katika kifungu cha (1) (c).
“Na
endapo Rais hatazingatia mapendekezo ya kundi mojawapo, Rais afanye mrejesho
kwa taarifa kwa kundi husika juu ya sababu za kutozingatia mtiririko wa
mapendekezo yaliyowasilishwa kwake,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo inaongeza kuwa kamati hiyo ilikuwa na maoni kwamba makundi mengine ya
kijamii yaongezwe katika kifungu cha 22(1) (c) cha sheria mama, ili kupanua
wigo wa uwakilishi mpana katika Bunge la Katiba, hivyo kuongeza idadi ya
wabunge hao kutoka idadi ya awali 166 hadi kufikia 201.
“Kamati
inashauri kuwa idadi ya wajumbe iwe 201 badala ya idadi ya wajumbe 166
iliyotajwa katika sheria mama, ili kupata idadi ya wajumbe watakaounda Bunge
Maalumu la Katiba,” inasomeka taarifa hiyo.
Hata
hivyo, maoni hayo yanatofautiana na yale yaliyowasilishwa bungeni juzi na jana,
kwani yanaonyesha kwamba kulikuwa na majadiliano na mashauriano baina ya kamati
na Serikali, hivyo ilikubaliana kuwa “Rais apewe mamlaka ya kufanya uteuzi wa
wajumbe Bunge la Katiba” huku idadi ya wabunge wa kuteuliwa wakibaki 166.
Kifungu
hicho kiliondoa haki ya kila taasisi kuteua jina la mjumbe wake katika Bunge hilo
na badala yake, ikapendekezwa kuwa Rais atapelekewa matatu ili ateue moja kati
ya hayo.
Hata
hivyo, jana wakati Bunge lilipoketi kama kamati kwa ajili ya kupitia vifungu
vya marekebisho ya muswada huo, Serikali iliwasilisha marekebisho ya nyongeza
ambayo yanazitaka asasi za kiraia ziteue majina tisa na kati ya hayo Rais
anaweza kuteua jina moja na kama asiporidhika anaweza kuteua mtu kutoka nje ya
orodha hiyo.
Kuhusu
suala hilo Chikawe alisema: “Tangu awali ilikuwa inaonyesha wajumbe ni 166. Ni
kweli Kamati ilipendekeza wajumbe hao waongezeke hadi 201 lakini pendekezo hilo
halikukubaliwa, ikabakia wajumbe watakuwa 166.”
Ushiriki
wa Zanzibar
Itakumbukwa
kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilipewa wiki nne za kuendesha vikao
vyake kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika jana, tofauti na
kamati nyingine ambazo zilipewa wiki mbili.
Baadhi
ya wabunge (hasa wa upinzani) wanasema madhumuni ya kupewa muda huo ni kama
hayakutimia kwani hawakuweza kupokea maoni kutoka kwa makundi muhimu hasa ya
upande wa Zanzibar kama ilivyokusudiwa.
Hata
hivyo, jana Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
Balozi Seif Ali Idd, alilihakikishia Bunge kuwa upande wa Zanzibar
ulishirikishwa katika kutoa maoni ya muswada huo.
Hatua
ya Balozi Idd kutoa ufafanuzi ilitokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa
Sikonge, Said Nkumba(CCM) aliyeomba kwa vile Balozi Seif yuko ndani ya Bunge
basi apewe fursa kufafanua utata huo.
Kauli
ya Balozi Idd inapingana na ile iliyotolewa juzi jioni na Mnadhimu wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye alisema ni kosa kubwa kamati kutochukua
maoni ya Wazanzibar.
Lissu
alisema kulikuwa na njama tangu mwanzo za kuhakikisha kuwa Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala haichukui maoni ya Wazanzibari na hilo
linathibitishwa na ratiba zilizokuwa zimeandaliwa na kamati.
“Katika
orodha ya wadau wote 22 waliokuwa wameorodheshwa katika kutoa maoni yao juu ya
muswada huu hakukuwa na Mzanzibari hata mmoja…tulipoipitia tukasema hapana
Wazanzibari wako wapi,” alisema.
Lissu
alisema yeye, Mwenyekiti wa Kamati, Chana na Makamu Mwenyekiti, William Ngeleja
walikwenda kumwona Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na kumweleza azma yao
ya kwenda kuzungumza na wadau wa Zanzibar.
“Katibu
akatwambia kwamba yeye ana fedha za kutuwezesha kukaa Zanzibar hata wiki moja,
kwa hiyo tukarudi kwenye kamati tukatengeneza ratiba mpya na tukaongeza wadau
sita wa Tanganyika na Wazanzibari wanane,” alisema Lissu.
Aliwataja
wadau hao kuwa ni Chuo cha Taifa Zanzibar, Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chama cha
Mawakili Zanzibar, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar, Chama cha Walemavu
Zanzibar na Profesa Abdul Shariff.
Wadau
wengine walikuwa ni Shirikisho la Vyama visivyo vya Kiserikali Zanzibar
(Angoza) na Jumuiya ya Misikiti Zanzibar na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, lakini
hatukuwahi kukutana nao na kupokea maoni yao.
“Tukakubaliana
kuwa tutakaa Zanzibar kwa siku tatu kuanzia Julai 14 hadi Julai 16 mpaka leo
hatujawahi kuambiwa kwa nini tulizuiwa kwenda Zanzibar, lakini maneno
yaliyokuwa yakisikika eti kwa sababu za kiusalama,” alisema.
Lissu
alisema wakati kamati yao ikiambiwa haiwezi kwenda Zanzibar kwa sababu za
kiusalama, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge hilo ilikuwa Pemba ikiendelea
na ziara zake.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi.







No comments:
Post a Comment