![]() |
Rais Dkt.
Jakaya kikwete akifungua rasmi ofisi ya ubalozi wa heshima wa Tanzania jijini
San Francisco nchini Marekani.
|
![]() |
| Dkt.Jakaya Mrisho. |
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiambia
Kamati ya Bunge la Marekani kuwa Tanzania haijafukuza mkimbizi hata mmoja
kutoka nchini na wanaondolewa katika Tanzania ni wahamiaji haramu walioingia na
kuishi nchini bila kufuata taratibu na sheria za Uhamiaji.
Rais amesema
kuwa kamwe Tanzania ambayo imekuwa kimbilio kubwa la wakimbizi katika historia
haiwezi kamwe kuwafukuza nchini wakimbizi kwa kuwa haina sababu ya kufanya
hivyo, na hata kama sababu ingekuwepo, ingefanya hivyo kwa kufuata taratibu za
kimataifa.
Msimamo huo
wa Tanzania umeelezwa kwa mara nyingine tena mchana wa leo, Jumatano, Septemba
18, 2013 wakati alipokutana katika mkutano wa kikazi na Mwenyekiti wa Kamati
Ndogo ya Mahusiano ya Nje na Bajeti ya Miradi ya Maendeleo, Mheshimiwa Kay
Granger na baadhi ya wajumbe wa Kamati yake.
Katika
mkutano huo uliofanyika katika Bunge la Marekani, mjini Washington D.C., Rais
Kikwete amesema kuwa umekuwepo upotoshaji kuhusu amri ya Serikali ya kuwaondoa
nchini wahamiaji haramu ambao wanaishi nchini kinyume cha sheria.
Akijibu
swali ambalo aliulizwa na mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Rais Kikwete
amesema: “Tuna wakimbizi 264,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao wote wako katika makambi yao mkoani
Kigoma. Hakuna mkimbizi ambaye amefukuzwa.”
Ameongeza: “Hata
kama tungetaka waondoke nchini tunajua taratibu za kuwaondoa wakimbizi kwa
sababu Tanzania ina uzoefu wa miaka mingi wa kuwapokea, kuwatunza na kuwajali
wakimbizi. Tungewasiliana kwanza na Umoja wa Mataifa na nchi ambazo walitokea
wakimbizi hao kabla ya kuwashauri kurudi makwao. Wote wako makambini na hivyo
suala la kuwafukuza nchini halipo.”
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Watu ambao tunawaondoa sisi ni wahamiaji haramu
katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita. Wengine wamekuwa nchini kwa muda. Kuna
wakati waliambiwa kuweka vizuri ukaaji wao nchini kisheria lakini hawakufanya
hivyo. Hawa hatuna jingine la kuwafanyia, ni lazima waondoke. Tuliwapa wiki
mbili za kuondoka wenyewe, tumeongeza tena muda wa wiki mbili. Kiasi cha
wahamiaji haramu 34,000 waliondoka wenyewe, sasa waliobakia tunawasaka katika
operesheni maalum.”
Alisema kuwa
baada ya kumalizika kwa muda huo, sasa Serikali imeanzisha operesheni maalum ya
kuwaondoa wale ambao hawakuondoka nchini wenyewe. “Na operesheni hii
itaendelea hadi tutakapomaliza tatizo hili la wahamiaji haramu ambao
wanashutumiwa kwa vitendo vya ujambazi, utekaji nyara mabasi, uvamizi wa misitu
ya asili na hifadhi kwa malisho na kuingiza maelfu kwa maelfu ya mifugo katika
maeneno tengefu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.”
Baada ya
mkutano huo, Rais Kikwete ameshiriki chakula cha mchana ambacho kiliandaliwa
kwa ajili yake na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Bunge la Marekani ya International
Conservation Caucus Foundation (ICCF) katika ukumbi wa chakula wa
Wabunge ndani ya Bunge hilo.
Rais Kikwete
ambaye yuko katika ziara ya kikazi katika Marekani amewasili mjini Washington
D.C., mapema leo asubuhi akitokea mjini San Francisco ambako alikuwa na ziara
ya siku mbili katika Jimbo la California.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES
SALAAM.
18 Septemba,
2013




.jpg)



No comments:
Post a Comment