Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo,
Alhamisi, Septemba 5, 2013, amekutana kwa faragha na Rais wa Rwanda, Mheshimiwa
Paul Kagame katika mazungumzo yaliyokwenda vizuri na kuwaridhisha viongozi hao
wawili wa nchi jirani.
Viongozi
hao wamekutana kwa zaidi kidogo ya saa moja katika mkutano uliofanyika kwenye
Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa Kampala, Uganda.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Rais Kagame wamekubaliana kuendelea
kushirikiana katika kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya nchi
hizo mbili.
Viongozi
hao wawili wako nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa
Kimataifa wa Maziwa Makuu – “International Conference on the Great Lakes Region
(ICGLR)” unaofanyika leo Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort.
Viongozi
wengine ambao wanahudhuria Mkutano huo ni pamoja na Rais Yoweri Museveni wa
Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR na mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Silva
Kiir wa Sudan Kusini, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC) na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
Rais
Kikwete na ujumbe wake amewasili Kampala asubuhi ya leo akitokea mjini Dodoma
ambako aliwasili jana jioni kwa ajili ya hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu
watatu na Naibu Makatibu Wakuuu wawili iliyofanyika Ikulu Ndogo, Dodoma.
Rais Kikwete aliwasili Dodoma akitokea Mwanza
ambako alihudhuria mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Evangelistic
Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu Mkuu Dkt. Moses Samwel Kulola
yaliyofanyika kwenye Kanisa la Bugando Calvary Temple, mjini Mwanza.
Imetolewa
na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
05 Septemba, 2013












No comments:
Post a Comment