![]() |
| Nape Moses Nnauye. |
Itakumbukwa
tarehe 16/06/2013 ilikuwa ni siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa baadhi ya
kata nchini.
Uchaguzi huo umefanyika kwenye kata ishirini na mbili (22) kati ya kata ishirini na sita (26)
zilizotangazwa kufanya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi wazi.
Matokeo
tuliyoyapata toka kwenye maeneo yaliyofanya uchaguzi yanaonyesha kuwa kati ya
kata 22 zilizofanya uchaguzi CCM tumeshinda kata 16 sawa na asilimia 72.72% na
wenzetu wamechukua kata 6 zilizobaki sawa na asilimia 27.28%.
Tunawashukuru sana kote walikoonyesha imani
yao kubwa kwa Chama chetu kwa kutupa dhamana ya kuendelea kuwatumikia. CCM
inawaahidi utumishi uliotukuka. Hata wale 27.28% walioamua kuwajaribu wenzetu,
tunawatakia kila lakheri, kwani wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua
wanaodhani watawasaidia kufikia malengo yao ya kimaendeleo. Uchaguzi kwenye
kata hizi zote umeisha sasa tuwatumikie wananchi.
Kata nne za
jiji la Arusha hazikufanya uchaguzi baada ya kuahirishwa kufuatia tukio la
kusikitisha la kulipuka kwa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema mjini
Arusha tarehe 15/06/2013.
CCM tunalaani tukio hilo la mlipuko wa bomu na
matukio yanayofanana na hayo katika nchi yetu.
Tunawapa pole wale wote
walioathirika na tukio hilo. Ni vizuri serikali ikalichunguza swala hili kwa
kutumia muda mfupi na kuhakikisha waliohusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua
zinazostahili.
Pamoja na
kulaani na kuitaka serikali kukomesha vitendo hivi nchini, ni wakati muafaka
kwa vyama vya siasa nchini kujitazama upya kwani kuna kila dalili kuwa tukio
hili kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari mhe. Mbowe Mwenyekiti
wa Chadema Taifa kuwa ni la kupangwa, inawezekana limepangwa na Chadema
wenyewe.
Hali ya
kisiasa jijini Arusha kuelekea uchaguzi huo ilikuwa wazi kuwa wana Arusha
walishaamua kuzirudisha kata hizo nne kwa CCM, hasa baada ya kuchoshwa na
maandamano na vurugu za kila siku jijini Arusha. Aidha kauli za kukata tamaa za
viongozi wa Chadema na vitendo vyao ni dalili tosha kuwa tukio hili lilipangwa
na Chadema wenyewe.
CCM
tunaendelea kusisitiza na kulaani juhudi za wenzetu kujaribu kujenga umaarufu
wa chama chao juu ya damu za Watanzania.
Juhudi hizi zinapaswa kulaaniwa na
wazalendo wote ndani na nje ya nchi. Tukumbuke asiyekubali kushindwa, si
mshindani. Si busara wala uungwana na ni kinyume na utu kutumia majanga ya
kutengeneza kama mtaji wa kisiasa.
Lakini CCM
tunalaani pia kitendo cha viongozi wa Chadema kujaribu kutumia baadhi ya misiba
na majeruhi wa tukio hili kisiasa na mwisho wa siku kwenda kuwatelekeza
hospitali baadhi yao baada ya kuwaahidi kubeba gharama zote za matibabu na mazishi.Tunaipongeza
serikali kwa kuingilia kati na kuwasaidia waathirika hawa na kuhakikisha
wanapata huduma inayostahili.
CCM inarudia
kueleza masikitiko yake kwa waathirika wa tukio hili la kinyama na kikatili
lisilostahili kuvumiliwa hata kidogo. Kama Chama tumeguswa sana na tukio hili
pamoja na kulilaani, tunawasihi watanzania tushindane na kutofautiana bila
kupigana na kuvunja tunu ya nchi yetu ya amani na utulivu. Katika demokrasia ya
vyama vingi swala la kuvumiliana ni swala la msingi sana katika kufikia ukomavu
wa demokrasia hiyo.
Imetolewa;
Nape Moses
Nnauye
Katibu wa
CCM Itikadi na Uenezi.
17/06/2013.






No comments:
Post a Comment