Mzee Nelson Mandela. |
Taarifa hiyo
ilithibitishwa na Rais Jacob Zuma ambaye kwa mara ya kwanza alikiri hadharani
kwamba hali ya afya ya Mzee Mandela ni mbaya na madaktari wanaendelea na juhudi
za kuokoa maisha yake.
Zuma ambaye
pia ni Rais wa Chama cha African National Congress (ANC), alikiri kufadhaishwa
na hali ya kiongozi huyo wa zamani, alipomtembelea katika Hospitali ya Magonjwa
ya Moyo ya Medi-Clinic mjini Pretoria na kuzungumza na mkewe, Graca Machel
kuhusu hali yake.
Kumekuwa na
taarifa kwamba tangu alipofikishwa hospitali, Mzee Mandela amekuwa hajitambui
na amekuwa akipumua kwa msaada wa mashine.
Pia,
kumekuwa na ulinzi mkali katika hospitali hiyo alikolazwa huku waandishi wa
habari na watu wasiokuwa wanafamilia wakizuiwa kwenda kumwona.
Ilielezwa
pia kwamba ulinzi ulizidi kuimarishwa jana(Juni 24,2013) katika maeneo
yanayozunguka hospitali hiyo.
Rais Mstaafu
wa Afrika Kusini, Bw.Thabo Mbeki
amewatoa hofu wananchi wa nchi hiyo kuwa Mzee Mandela anaendelea vizuri,
ingawa katika siku za hivi karibuni amekuwa akipelekwa hospitali mara kwa mara
kwa ajili ya kutibiwa.
Rais Mbeki
aliyemrithi Mandela mwaka 1999, alisema kuwa ni vizuri wananchi wakadumisha
sala kwa kumwombea mzee huyo badala ya kukata tamaa na kuamini uvumi kwamba
ameshafariki dunia.
Chama cha
ANC, Jumamosi iliyopita, kilitoa tamko kuwa Mzee Mandela inabidi aheshimiwe na
kwamba siyo kila mtu anaweza kuwa msemaji wa maendeleo ya afya yake.
Taarifa hiyo
ilieleza kuwa Ikulu ya Afrika Kusini inabidi ifanye kazi vizuri kuhakikisha
wananchi wanapata taarifa za kweli na zenye uhakika kuhusu kiongozi huyo
aliyeiongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1994 mpaka 1999.
“Chama chetu
cha The African National Congress kwa mara nyingine kinataka pande zinazohusika
zifanye kazi yake. Vilevile tunataka vyombo vya habari na familia, kuheshimu
taarifa za faragha kuhusu Mandela.”
Msemaji wa
chama hicho, Jackson Mthembu aliwataka wananchi wa Afrika Kusini na dunia kwa
jumla kuwaombea Mandela, ndugu zake na madaktari.
Mzee Mandela
ambaye mwezi ujao anatarajiwa kutimiza umri wa miaka 95, kwa muda mrefu sasa
anasumbuliwa na tatizo la mapafu kujaa maji.
Hatua hiyo
imesababisha simanzi na majonzi kwa wananchi wa Afrika Kusini ambao wamekuwa
wakimwombea na kutoa salamu za kumtakia afya njema.
Habari
zinasema kuwa tatizo la mapafu, ni matokeo ya athari alizozipata akiwa gerezani
kipindi alipofungwa miaka 27 jela katika miaka ya 1900.
Mzee Mandela
amekuwa kielelezo chema siyo tu kwa Afrika Kusini, bali Afrika na duniani kote.
Nasi Watanzania kila mtu kwa imani yake ni vema kumuombea salama ili Mungu ampe
nafuu na kumponya maradhi yanayomsibu kwa sasa.
Mzee Mandela
alilazwa katika Hospitali ya Moyo ya Medi-Clinic, Juni 8, mwaka huu kutokana na
maradhi ya homa ya mapafu yanayomsumbua na iliripotiwa kwamba tangu wakati huo
hajitambui.
No comments:
Post a Comment