![]() |
|
Kamishna
wa Polisi Zanzibar
Mussa
Ali Mussa
|
Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali uchunguzi wa
mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kusema mtuhumiwa hana kesi
ya kujibu mahakamani.
Padri Mushi
ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili aliuawa kwa kupigwa
risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi mjini Zanzibar akiwa ndani ya
gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu
Theresia, mjini Zanzibar.
Baada ya
mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha maafisa wa FBI
kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo na Machi 17,
mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika
na mauaji hayo.
Uchunguzi wa
NIPASHE umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa mauaji
hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea kumtafuta muuaji wa
Padri Mushi.
Kwa mujibu
wa uchunguzi huo, DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi na kukabidhiwa juzi
ikieleza sababu za ofisi yake kutofungua hati ya mashtaka hadi sasa dhidi ya
mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Jeshi la
Polisi limethibitisha kuipokea barua ya DPP ambayo inaeleza kuwa ushahidi
uliokusanywa katika jalada la kesi hiyo hauna mashiko na kwamba mtuhumiwa
hahusiki na mauaji hayo.
Chanzo cha
habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa DPP hajaridhishwa na uchunguzi
wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa pamoja na watuhumiwa watatu wanaotuhumiwa
kwa mauaji ya askari polisi, Said Abdulrahman aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na
watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu
Zanzibar Oktoba 17, mwaka jana.
Kamishna wa
Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha hatua ya DPP kutupa
uchunguzi wote wa jalada la mauaji ya Padri Mushi na kuwataka waandishi wa
habari kumtafuta DPP azungumzie sababu za uamuzi wake wa kutokubaliana na
uchunguzi wa Polisi.
Hata hivyo,
alisema kwamba Jeshi la Polisi bado linaamini uchunguzi walioufanya kwa
kushirikiana na FBI hauna shaka na kwamba mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu
mahakamani na wataendelea kumshikilia.
Alisema
kwamba kwa mujibu wa sheria, Jeshi la Polisi jukumu lake ni kuchunguza kesi na
ofisi ya DPP jukumu lake ni kufungua hati ya mashtaka na kutetea kesi
mahakamani.
Hata hivyo,
NIPASHE ilipofika katika ofisi ya DPP, Katibu muhtasi wake alisema amepokea
maagizo kutoka kwa bosi wake kuwa waandishi wote wa habari wanaofuatilia suala
hilo, wamuone Kamishna wa Polisi kwa vile kazi aliyopewa ya kupitia jalada la
uchunguzi kabla ya kufungua kesi ameikamilisha.
“Kamishna
ndiye aliyeitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea hatua iliyofikiwa
pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa, sasa awaite tena amalizie kazi yake ya
kuwaeleza hatua iliyofikiwa baada ya Mkurugenzi kurejesha jalada la mauaji,”
alisema Katibu muhtasi huyo.
Katika hatua
nyingine, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Yusuph Ilembo, jana
alifika katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, kufuatia ombi lililofunguliwa
mahakamani na wakili anayemtetea mtuhumiwa wa mauaji, Abdallah Juma Mohamed.
![]() |
|
Waziri
wa Mambo ya Ndani
ya
Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi
|
Abdallah
Juma amefungua ombi katika Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha sheria 390 cha
sheria namba 7 ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004, akitaka Jeshi la
Polisi litoe maelezo kwa nini mteja wake hajafikishwa mahakamani ndani ya saa
24 tangu alipokamatwa Machi 17, mwaka huu.
Wakili
Abdallah Juma akisaidiwa na mawakili Shaban Juma Bakari na Shaibu Ibrahim
Shaibu waliitaka Mahakama Kuu itoe amri ya kuachiwa kwa mteja wao kutoka
mikononi mwa Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, Ilembo alisema kuwa kutokana na uzito
wa kesi hiyo, anaomba kupewa muda wa kutayarisha majibu ya hati ya kiapo kwa
maandishi na kuuwasilisha kwa upande wa utetezi na mbele ya mahakama hiyo kabla
ya ombi hilo kuanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
“Tunaomba
mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na Polisi, wakati tukifanya matayarisho ya
kujibu hati ya kiapo,” alisema Ilembo.
Kwa upande
wake Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema baada ya kusikiliza
pande zote mbili, alimtaka Ilembo awe amejibu kwa maandishi hati ya kiapo ya
maombi hayo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo Aprili 8, mwaka huu.
Aidha, Jaji
alisema wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, ametaka mtuhumiwa huyo afikishwe
mahakamani, baada ya hoja za upande wa mawakili wanaomtetea kutaka dhamana kwa
mteja wao, kwa vile bado hajafikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.
Kutupwa kwa
uchunguzi wa jalada la mauaji hayo pamoja na jalada la uchunguzi wa mauaji ya
Polisi kunadhihirisha kuwapo kwa mvutano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi
Zanzibar na ofisi ya DPP.







No comments:
Post a Comment